Lebanoni: Gari la UNIFIL limechomwa moto karibu na Beirut, mkutano wa dharura waitishwa

Mamlaka ya Lebanoni imeitisha mkutano wa dharura Jumamosi (Februari 15) baada ya maafisa wawili kujeruhiwa wakati gari la kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon lilipochomwa moto kwenye barabara iliyokuwa imefungwa na wafuasi wa Hezbollah karibu na Beirut. Shambulio hili limelaaniwa vikali na mamlaka ya Lebanon. Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini humo kinataka uchunguzi wa haraka ufanyike na kukemea uwezekano wa uhalifu wa kivita.

Imechapishwa:

Dakika 3

Matangazo ya kibiashara

“Siku ya Ijumaa jioni, msafara wa UNIFIL uliokuwa ukisafirisha askari wa kulinda amani kwenye uwanja wa ndege wa Beirut ulishambuliwa vikali, na gari likachomwa moto. “Naibu Kamanda wa Kikosi cha UNIFIL anayeondoka, ambaye alikuwa akirejea nyumbani baada ya kumaliza kazi yake, alijeruhiwa,” UNIFIL imesema katika taarifa. “Tunataka uchunguzi kamili na wa haraka wa mamlaka ya Lebanoni na kwamba wale wote waliohusika wafikishwe mahakamani,” imeongeza UNIFIL, iliyotumwa kusini mwa nchi hiyo tangu mwaka 1978 kufanya kama kinga dhidi ya Israel, ikilaani “ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa” ambao unaweza kufananishwa na “uhalifu wa kivita.” “Tumeshtushwa na shambulio hili la kutisha dhidi ya walinda amani wanaofanya kazi ya kurejesha usalama na utulivu kusini mwa Lebanon katika wakati huu mgumu,” UNIFIL imeongeza.

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanoni, Jeanine Hennis-Plasschaert, kwa upande wake amelaani “shambulio lisilokubalika ambalo linatishia usalama wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.” Katika mazungumzo na Jeanine Hennis-Plasschaert na Kamanda wa Unifil Jenerali Aroldo Lazaro, Waziri Mkuu wa Lebanoni Nawaf Salam amelaani vikali “shambulio hilo la uhalifu” na kuwaahidi “hatua za haraka za kutambua washambuliaji, kuwakamata na kuwafikisha mbele ya mamlaka ya mahakama yenye uwezo.” “Kwa upande wake, Rais wa Lebanoni Joseph Aoun “amelaani shambulio hilo” na “amesisitiza kuwa washambuliaji wataadhibiwa,” ofisi ya rais imesema kwenye mtandao wa kijamii wa X, na kuongeza kuwa “vikosi vya usalama havitaonyesha upole wowote kwa mtu yeyote ambaye anajaribu kuvuruga utulivu na amani ya raia. “

Jeshi la Lebanoni laapa kuchukua hatua thabiti

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Lebanoni, ambaye amewatembelea maafisa wawili waliojeruhiwa wa UNIFIL hospitalini, ametangaza Jumamosi kukamatwa kwa zaidi ya watu 25. “Hii haimaanishi kuwa wafungwa hawa walifanya shambulizi,” waziri amewaambia waandishi wa habari baada ya mkutano wa dharura wa usalama. Uchunguzi, ameongeza, “umeonyesha nani anahusika na ni nani aliyefanya kitendo hiki. Uchunguzi utaendelea kwa umakini mkubwa.”

Kwa upande wake, jeshi la Lebanoni limeahidi kuchukua hatua “kwa uthabiti kuzuia shambulio lolote dhidi ya amani ya raia na kuwakamata wavurugaji. “Watu waliochoma gari hilo bado hawajajulikana.

Hezbollah haikujibu mara moja lakini mshirika wake, vuguvugu la Amal linaloongozwa na kiongozi wa bunge Nabih Berri, limeshutumu “mashambulizi dhidi ya kusini mwa Lebanoni”. “Vizuizi vya barabarani, popote vinaporipotiwa, vinajumuisha shambulio dhidi ya amani ya raia,” vuguvugu hilo limeongeza katika taarifa.

Gari la UNIFIL limechomwa moto

Shambulio hilo limetokea huku makumi ya wafuasi wa Hezbollah wakifunga barabara ya kuelekea uwanja wa ndege wa Beirut katika viunga vya kusini mwa mji mkuu, ngome ya vuguvugu hilo linalounga mkono Iran, kwa usiku wa pili mfululizo siku ya Ijumaa. Video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha waandamanaji, wengine wakiwa wamevalia vazi na kubeba bendera za Hezbollah, wakimshambulia mtu aliyevalia sare za kijeshi na mwingine aliyevalia kiraia karibu na gari la UNIFIL lililoungua. Mwandishi wa habari wa shirika la habari la AFP ameona gari lililoteketea likiwa na nembo ya Umoja wa Mataifa kwenye barabara ya kuelekea uwanja wa ndege, ambapo jeshi limetumwa.