
Wizara ya Afya ya Lebanon imeushutumu utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kufanya ilichokiita “msururu wa jinai za kivita” katika mauaji ya kuwalenga makusudi wafanyakazi wa afya na kubomoa na kuharibu vituo vya afya.
Hii ni baada ya mashambulizi ya anga yaliyofanywa hivi karibuni na jeshi la utawala haramu wa Israel kumuua shahidi mkurugenzi wa hospitali kaskazini mashariki mwa Lebanon na wahudumu watano kusini mwa nchi hiyo.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza katika ripoti yake mpya kuwa, wahudumu wa afya na wagonjwa 226 wameuawa shahidi nchini Lebanon katika kipindi cha kuanzia Oktoba 2023 hadi mwanzoni mwa wiki hii.
Tangu wakati vilipoanza vita vya kinyama na mauaji ya kimbari ya Ghaza yanayoendelezwa na jeshi la utawala wa Kizayuni, huko Lebanon pia watu wasiopungua 3,645 wameuawa shahidi na 15,355 wamejeruhiwa katika mashambulizi yaliyofanywa pia na jeshi hilo la utawala huo haramu.
Wakati huohuo, vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani nchini Lebanon UNIFIL vimetangaza kuwa, uharibifu uliofanywa na jeshi la Israel nchini humo ni mkubwa.
Walinda amani hao wanasema wameshuhudia uharibifu mkubwa kutokana na mashambulio ya jeshi hilo kulenga miundombinu ya raia zikiwemo nyumba, barabara, skuli, hospitali na mitambo ya huduma nyingine muhimu kwa raia…/