LBL yafutiwa usajili Tanzania

Dar es Salaam. Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) umezifutia leseni kampuni 11 za Leo Beneath London (LBL) zilizosajiliwa katika mikoa mbalimbali kuanzia Februari 27, 2025.

Brela imechukua hatua hiyo baada ya kuwapo kwa malalamiko ya baadhi ya watu kutapeliwa fedha zao huku baadhi na viongozi wa kampuni hiyo wakishikiliwa na vyombo vya dola kwa kuendesha shughuli zao bila kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kwa mujibu wa Brela, kampuni hizo zote usajili wake ulionyesha kuwa na kazi zinazofanana za uzalishaji wa vipindi mbalimbali na matangazo, lakini kilichokuwa kikifanyika ni tofauti.

Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Godfrey Nyaisa  amezifuta kampuni hizo 11 kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 400A cha Sheria ya Kampuni Sura 212.

Amesema sababu ya kufuta kampuni hizo ni kukiuka masharti ya kifungu cha 400A (1) (e) cha sheria tajwa hiyo, kwa kufanya shughuli za kibiashara nje ya madhumuni yaliyoainishwa katika katiba za kampuni hizo na miongozo ya uendeshaji wa kampuni wakati wa usajili.

“Kifungu hiki kikikiukwa, sheria inamtaka msajili kuchukua hatua chini ya mifungu hicho 400A (1) (e) ambazo ni kuijulisha kampuni kuhusu ukiukwaji na hatua anazokusudia kuzichukua kwa kampuni husika,” amesema Nyaisa leo wakati wa mkutano wake na waandishi wahabari.

Sheria hiyo pia kabla ya kutekelezwa kwake inasema endapo kampuni itashindwa kutoa maelezo, au kutoa maelezo yasiyoridhisha, msajili atafuta kampuni husika kwenye rejista ya kampuni.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 400A (1) (e) msajili alizijulisha kampuni husika kuhusu kusudio la kuzifuta kupitia notisi zilizotolewa kati ya Januari 2 na Januari 26, 2025 na kwa kuwa kampuni hizo hazikuwasilisha maelezo yoyote kama zilivyotakiwa chini ya kifungu 400A (2), msajili amezifuta rasmi kampuni hizo kwenye rejista ya kampuni kuanzia Februari  27, 2025,” amesema.

Kampuni za LBL zilizofutwa ni  Mtwara Media Company Limited (Na. 181289972), LBL Morogoro Media Company Limited (Na. 179770873), LBL Geita Advertising Media Limited (Na. 180439242), LBL Mbeya Media Limited (Na. 179978326).

Nyingine ni  LBL Future Vision Advertising Agency Company Limited (Na. 181302259), LBL Mbezi Advertising Media Company Limited (Na. 180582835), LBL Ubungo Media Limited (Na. 180960333), LBL Mabibo Media Company Limited (Na. 181117346), LBL Mbagala Media Company Limited (Na. 181248874), LBL Gongo la Mboto Media Advertising Company Limited (Na. 181513438) na LBL Dar es Salaam Kigamboni Advertising Company Limited (Na. 180046992).

Kampuni hizo zilisajiliwa na watu tofauti kwa mujibu wa Brela, zikiwa na utofauti katika baadhi ya maneno kwenye jina, ili kufanikisha usajili huo.

Brela imesema kampuni hizo zilisajiliwa kati ya Novemba mwaka jana hadi Februari mwaka huu katika maeneo tofauti.

Kuhusu kuchelewa kuchukua hatua licha ya kuwapo kwa malalamiko, Nyaisa amesema wakati mwingine utendaji kazi wao ni sawa na Wakala wa Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita) ambao hutoa vyeti kwa watoto na kuwaacha waendelee kukua bila kujua wanaendeleaje.

“Napenda kuukumbusha umma kuwa hakuna sheria wala taasisi yenye mamlaka ya kutoa vibali wala leseni za kufanya biashara za upatu hapa nchini  kwa sababu biashara ya upatu ni kinyume na sheria,” amesema Nyaisa na kuongeza

“Msajili anaendelea na ufuatiliaji wa kampuni nyingine zinazofanya shughuli za kibiashara nje ya katiba zake na kinyume na sheria na taratibu, na ataendelea kuzichukulia hatua stahiki ikiwemo kuzifuta kwenye rejista ya kampuni.

Amewataka wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika, zikiwemo taasisi za kiserikali na Jeshi la Polisi, ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya kampuni au watu wanaofanya au kujihusisha na biashara hiyo.