
BEKI wa Coastal Union, Lameck Lawi amesema huu ni msimu dume kwake na timu kwa ujumla lakini wanapambana kuhakikisha msimu ujao wanacheza tena ligi kwa ubora zaidi.
Coastal ipo nafasi ya tisa katika msimamo baada ya mechi 22, ikishinda tano, sare tisa na kupoteza mara nane ipo nafasi ya kumi kwenye timu iliyoruhusu nyavu zake kutikiswa mara nyingi wakifungwa mabao 23 na kukusanya pointi 24.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lawi ambaye aliziingiza vitani Simba na Yanga kwenye madirisha yote mawili ya usajili msimu huu alisema ni kweli hajawa na msimu mzuri lakini inachangiwa na changamoto ya timu nzima kwa ujumla kupambana kupata matokeo.
“Huu ni msimu dume kweli kweli hatujawa na msimu bora tangu ligi imeanza hadi sasa lakini hatutakuwa sehemu ya wachezaji watakaoishusha Coastal Union zaidi tunaendelea kupambana kuona tunapata nafasi ya kucheza tena msimu ujao,” alisema na kuongeza;
“Siwezi kuwa bora peke yangu kwenye kikosi cha wachezaji 11 uwanjani hili la makosa yanayofanyika nalibeba mimi pamoja na wenzangu na tumekuwa tukizungumza kila tunapodondosha pointi ili kujitengenezea mazingira mengine bora kwa mechi zinazofuata na ndio siri ya matokeo mazuri kwenye mechi za karibuni.”
Lawi alisema hakuna mchezaji anaefanya makosa kwa makusudi bali inakuwa ni sehemu ya mchezo na wanapamba kuhakikisha wanakuwa bora ili kuirudisha timu yao kwenye ushindani pamoja na changamoto ya ugumu wa ligi msimu huu hasa mzunguko huu wa lala salama.
“Sio muda wa kulauminiana sasa tunacheza kitimu kila mmoja anatakiwa kufanya majukumu yake kwa usahihi bila kumuangalia fulani anakosea wapi na mara baada ya mchezo ndio tunafanya tathimini na kuelekezana nini kifanyike ili kuondoa makosa na kuongeza utulivu, kikubwa ni kuona Coastal Union inakuwa bora na inamaliza msimu ikiwa katika nafasi nzuri.”