Lamar alivyofungua milango ya mastaa wengi Bongo 

Dar es Salaam. Lamar ni jina la mtayarishaji muziki Bongo alianza kazi hiyo akiwa kijana mdogo sana na kulishika game kipindi hicho kwa kufanya kazi na wasanii wengi wakubwa kuanzia waimbaji hadi wale wanaochana, yaani Hip Hop.

Lamar ambaye amepita Bongo Records, 41 Records hadi kufungua studio yake Fishcrub, ni mshindi wa tuzo za muziki Tanzania (TMA) 2010 kama Mtayarishaji Bora wa Mwaka. Na huyu ndiye Lamar.

Lamar alianza kujifunza utayarishaji muziki akiwa masomoni Uganda, mwaka 2001 akarejea Tanzania na kuanza kutafuta nafasi studio, 2006 akaingia Bongo Records baada ya Dunga kumshawishi P-Funk Majani kumpa nafasi.

                   

Kabla ya kuingia Bongo Records, Lamar alikuwa anaenda internet cafe na kukaa kwenye kompyuta kisha anafanya mazoezi ya kuandaa muziki, pia alifanya mazoezi Mambo Jambo Records. 

Moja ya nyimbo ambazo Lamar alishiriki kuandaa kipindi yupo Bongo Records ni pamoja na ule wa Keysha ‘Sikuhitaji’ akimshirikisha Mwana FA. Wasanii hawa kwa sasa ni wabunge huku pia Mwana FA akiwa ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Hata hivyo, hakudumu kwa kupindi kirefu Bongo Records kwani mwaka 2007 alihamia 41 Records na alifanya kazi na Dunga kutokea Kenya ambaye ndiye alimjenga sana kwa kumfundisha vitu vingine katika utayarishaji muziki.

Ni Dunga ambaye ndiye alileta mtindo wa muziki wa Bounce hapa Bongo na wasanii kama Professor Jay, Q Chief, Noorah, Black Ryno, JCB, Mh. Temba n,k. wakapita nao.

Wimbo wa Joh Makini, Mfalme (2007) uliotengenezwa 41 Records ndio ulikuwa wa kwanza kwa Lamar kuuandaa wote pekee na kuachiwa rasmi. Hapa alitengeneza mdundo yeye na kufanya mixing na mastering tofauti na awali alikuwa anashirikiana na wenzake.

Lamar alipata wazo la kutengeneza mdundo huo wa wimbo wa Joh Makini katika wimbo wa Jay Z ‘Public Service Announcement’ kutoka katika albamu ya nne, The Black Album (2003) chini ya Roc-A-Fella na Def Jam Recordings.

                       

Joh Makini ambaye tayari alikuwa ametoka na wimbo wake, Chochote Popote (2006) uliotengenezwa na Dunga na kujumuishwa katika albamu yake ya kwanza, Zamu Yangu (2007), alirekodi kazi nyingi na Lamar kabla ya huo ‘Mfalme’ uliotoka.

Studio ya Bob Junior, Sharobaro Records ilianzia nyumbani kwa Lamar na walikuwa wanatumia vifaa vya studio pamoja ila baadaye ikatokea kutoelewana na kila mmoja kushika njia yake na ndipo Lamar akaja kuanzisha studio yake, Fishcrab.

Utakumbuka Sharobaro Records ndiyo iliyokuja kumtoa Diamond Platunumz kimuziki kupitia wimbo wake, Kamwambie (2009) uliobeba jina la albamu yake ya kwanza iliyotoka 2010.

Fedha za kununua vifaa vya kuanzisha Fishcrab alizipata baada ya kwenda kusoma uandisi sauti (sound engineering) huko Amsterdam, Uholanzi na alikuwa akipatiwa Euro50 kila siku kwa ajili ya kujikimu na ndipo akajichanga na kununua vifaa.

Ndani ya Fishcrab Lamar alifanya kazi na wasanii kama Lady Jaydee, Alikiba, Diamond, TID, Mrisho Mpoto, Chid Benzi n.k.

                         

Wazo la kuweka kisauti cha kujitambulisha (sign tune) katika kila wimbo aliotengeneza, Lamar alilipata kutoka kwa Diddy, nyimbo nyingi za Bad Boys Records zilikuwa na utambulisho fulani wenye sauti ya Diddy.

Ruge Mutahaba ambaye alikuwa anamsimamia Mwasiti hakuukubali wimbo wa Mwasiti, Hao (2007) ambao ulitayarishwa na Lamar huku Chid Benzi akishirikishwa, hivyo ilikaa sana ndani ila ulipokuja kutoka ulifanya vizuri sana.

Ngoma hiyo ambayo ilitoka mwaka mmoja baada ya Chid Benzi kushinda TMA 2006 kama Msanii Bora wa Hip Hop, Professor Jay ndiye alitakiwa kushirikishwa ila akakosekana ndipo Chid ambaye naye alikuwa anafanya vizuri akapewa nafasi hiyo.