
KOCHA Mkuu wa TMA FC ya jijini Arusha, Mohamed Ismail ‘Laizer’, amesema moja ya changamoto kubwa kwenye kikosi hicho ni kutokuwa na balansi nzuri katika eneo la uzuiaji na ushambuliaji, ingawa kwa sasa muhimu ni kupata pointi tatu.
Akizungumza na Mwanaspoti, ‘Laizer’ alisema mwenendo wa kikosi hicho hadi sasa sio mbaya ingawa changamoto ya kuruhusu mabao ndiyo kazi kubwa anayopambana nayo katika michezo tisa iliyobakia, ili kujiweka kwenye mazingira mazuri mwishoni.
“Ni kweli hali hiyo imekuwa ikitugharimu kwa baadhi ya michezo kwa sababu kuna wakati unaona tuna nafasi ya kushinda ila mwishoni wapinzani wetu wanasawazisha, hii ni kazi tunayopambana nayo ingawa kupata pointi tatu ndio kipaumbele chetu.”
Kocha huyo aliyejiunga na timu hiyo Januari 20, mwaka huu akichukua nafasi ya Maka Mwalwisi aliyeanza nayo msimu kisha kujiunga na Mbeya Kwanza, ameiongoza katika michezo sita na kati yake ameshinda mitatu, sare miwili na kupoteza mmoja.
TMA FC imecheza michezo 22 hadi sasa na kati ya hiyo imeshinda 12, sare mitano na kupoteza pia mitano, ikiwa nafasi ya tano na pointi 41, ambapo eneo la ushambuliaji ya kikosi hicho imefunga mabao 32 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 20.