Marekani. Rapa Snoop Dogg, 53, ameendelea kulaumiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Death Row Records, Suge Knight, 59, kwa madai amechagia kuharibu historia ya lebo hiyo maarufu na hata muziki wa Hip Hop kwa jumla.
Suge ambaye yupo gerezani kwa tuhuma za mauaji ya bila kukusudia, alisema badala ya Snoop kuifanya lebo hiyo kuwa kubwa, umeukatisha tamaa ulimwengu kwa kufanya kila kitu kishuke huku akihoji mchakato wa kuinunua.
Ikumbukwe Death Row Records ilianzishwa mwaka 1991 na The D.O.C., Dr. Dre, Suge Knight na Dick Griffey, lebo hii ilivuma sana kwa kutoa albamu nyingi za Hip Hop zilizofikia mauzo ya platinum mara nyingi, yaani nakala zaidi ya milioni 1.
Wasanii wa West Coast walilishika soko chini ya Death Row, miongoni mwa waliotoa albamu hapo ni Dr. Dre, The Chronic (1992), Snoop Dogg, Doggystyle (1993), 2Pac, All Eyez on Me (1996) n.k.
Hata hivyo, baadaye Dr. Dre na Snoop Dogg walikuja kuondoka Death Row, huku Dre akianzisha Aftermath Entertainment, na Snoop akiendelea kusaini mikataba na lebo nyingine kama No Limit Records na Interscope Records.

Katika mahojiano na The Art of Dialogue kutoka gerezani mwishoni mwa wiki, Suge alisema anaamini asili ya tamaduni ya Hip Hop inaharibiwa na alidai Snoop pia anaua uaminifu wa lebo hiyo ya West Coast iliyokuwa ikiogopwa.
“Unajaribu kutengeneza kitu ambacho tayari Suge Knight alishakiunda, lakini badala ya kutengeneza kitu kikubwa, unaukatisha tamaa ulimwengu kwa kufanya kila kishuke. Nilipoisimamia waliuza rekodi, ulipoisimamia, hawakuuza chochote,” alisema na kuongeza.
“Hatupaswi kuwazungumzia watu wachache; watu watatu au wanne, hiyo sio kubwa kuliko Hip Hop, tunapaswa kujaribu kufikiria jinsi ya kufanya muziki huo kuwa bora zaidi. Kama una Death Row halafu unaiharibu, jua umeharibu jina la Hip Hop,” alisema Suge.
Utakumbuka Snoop alipata umiliki wa chapa ya Death Row Records kutoka katika kundi la MNRK linalosimamiwa na Blackstone, zamani eOne Music kwa mkataba waliosaini hapo Februari 2022.
“Ninajisikia vizuri kuwa na umiliki wa lebo niliyokuwa sehemu yake mwanzoni mwa kazi yangu na kama mmoja wa wanachama waanzilishi. Huu ni wakati wa maana sana kwangu. Natarajia kujenga sura mpya ya Death Row,” alisema Snoop katika taarifa yake.

Hata hivyo, Suge bado haamini iwapo Snoop ameinunua lebo hiyo na kumtaka kutoa uthibitisho usio na shaka ndiye mwenye umiliki halali kabla ya kumpa heshima yake.
“Snoop, unasema nimechukia kwa sababu umeinunua Death Row?, kipi hasa umenunua?. Nionyeshe mahali ulipolipa fedha kuinunua. Nionyeshe karatasi ya mkataba, nionyeshe unachomiliki,” Suge alihoji wakati akiongea na The Art of Dialogue.
Bado Suge Knight yupo jela akitumikia kifungo cha miaka 28 kwa makosa ya kuua bila kukusudia ambayo yalisababisha kifo cha mfanyabiashara Terry Carter na majeraha kwa hasimu wake wa muda mrefu, Cle ‘Bone Sloan ambaye ni mwanaharakati.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 59 sasa ambaye alikuwa maarufu katika ulimwengu wa Hip Hop miaka ya 1990, anatarajiwa kutoka jela kwa msamaha (parole) hapo Oktoba 2034.
Huyu ndiye alimsaini 2Pac kwenye lebo ya Death Row Records tangu mwaka 1995 na kusimamia albamu zake mbili, All Eyez on Me (1996) na The Don Killuminati: The 7 Days Theory (1996) zilizofanya vizuri sokoni.

Baada ya kusaini Death Row, 2Pac aliwakilisha West Coast na kuingia katika vita na wakali wa East Coast, The Notorious B.I.G na Diddy kutoka Bad Boy Records kitu kilichokuja kuwa na matokeo mabaya ikiwemo vifo vya 2Pac na B.I.G.
Desemba 2024, Snoop Dogg akiongea na Associated Press alisema rafiki yake na mshirika wake kibiashara kwa muda mrefu, Dr. Dre hakukubaliana naye alipoinunua Death Row kutokana na kuwa na historia ya migogoro ya kila mara.
“Dr. Dre hakupenda, ilikuwa kama unanunua mfuko wa matatizo wakati unaishi maisha ya mafanikio na si lazima kukabiliana na matatizo hayo!, kwa nini arudishe hilo maishani mwako?,” alisema Snoop Dogg.
Hata hivyo, licha ya mashaka ya Dre, Snoop aliendeleza mpango wake kwani alihisi ununuzi huo ungekuwa na matokeo muhimu katika safari yake ya muziki na kukamilisha sehemu ya ndoto zake.
“Hawakuona nilichokiona, niliona urithi wangu, niliona mambo fulani ambayo yaliunganishwa nami ambayo yalihitaji kukamilika, kuhusu biashara ambayo haijakamilika,” alisema Snoop na kuongeza.

“Na pia nilifanya hivyo ili kulinda urithi wangu kwa kuweka muziki mzuri ndani ya Death Row na kuweka nyakati za furaha maishani na baada ya kifo ndani ya Death Row,” alisema rapa huyo wa kibao, Drop It Like It’s Hot (2004).
Ikumbukwe miaka michache baada ya kuachana na Death Row, Dr. Dre, mshindi wa tuzo saba za Grammy alitengeneza albamu ya pili ya Eminem, The Slim Shady LP (1999) ambayo ilimfanya rapa huyo kuwa tishio duniani baada ya kumsaini Aftermath Entertainment.