Kwanini mikataba ya uwekezaji ipitiwe upya Tanzania?

Katika miaka kadhaa iliyopita Tanzania iliingia hasara ya mabilioni ya shilingi iliyolipa kama fidia kwa kampuni mbalimbali kutokana na kushitakiwa kwenye mahakama za usuluhisi za kimataifa kuhusu mikataba ya uwekezaji.

Mfano, Oktoba 2023, mgogoro kati ya kampuni ya Winshear Gold Corp ya nchini Canada ulitamatika kwa suluhu nje ya mahakama, baada ya Tanzania kukubali kulipa Dola za Marekani 30 milioni (wastani wa Sh75 bilioni).

Kampuni hiyo iliishitaki Tanzania baada ya kufutiwa leseni yake kwenye mradi wake wa SMP Gold, uliokuwepo kusini mwa Tanzania. Leseni za Winshear zilifutwa baada ya serikali kurekebisha Sheria ya Madini ya mwaka 2010, kanuni zake zilifuta leseni zote za uhifadhi wa madini.

Tanzania ilishitakiwa kwa kutumia mkataba wa uwekezaji kati yake na Canada (Canada -Tanzania BIT).

Kesi nyingine ni ya Sunlodges (T) Ltd dhidi ya Serikali ya Tanzania iliyotokana na uamuzi wa Serikali wa mwaka 2011 kunyang’anya umiliki wa ardhi ya mlalamikaji mkoani Mtwara. Sunlodges ilidai kuwa hatua hiyo ilikiuka mkataba wa uwekezaji kati ya Tanzania na Italia.

Mahakama iliamua Sunlodges BVI ilipwe dola milioni 8.91 (Sh22.34 bilioni) na Sunlodges Tanzania dola 2.34 milioni (Sh5.85 bilioni), zote zikiwa na riba, tangu mwaka 2011.

Serikali ya Tanzania ililipa Sh50.1 bilioni mwaka 2021 kumaliza kesi hiyo. Kesi nyingine maarufu ni ile ya kampuni ya Symbion dhidi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na zaidi ya Sh350 bilioni, zililipwa.

Kesi nyingine tatu zilizoigharimu nchi zaidi ya Sh800 bilioni ni ile ya Mikindani Estate ya Sunlodge na mbili dhidi ya benki ya Standard Chartered Hong Kong. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtandao wa asasi za kiraia na vyama vya wafanyakazi unaofanya chambuzi za biashara, sera na uwekezaji (TATIC), kuna zaidi ya kesi 12 zinazojulikana ambazo zimekamilika na nyingine kwenye hatua mbalimbali.

Kwa nini BIT?

Uchambuzi wa TATIC ulisema BITs imekuwa ikizingatiwa kama nyenzo ya kuvutia Uwekezaji wa Moja kwa Moja wa Kigeni (FDI) katika nchi zinazoendelea.

Mikataba hii inayosainiwa kati ya nchi mbili, inalenga kutoa ulinzi wa kisheria kwa wawekezaji na kuunda mazingira thabiti ya uwekezaji.

“Hata hivyo, nchini Tanzania, ufanisi wa BITs katika kuvutia wawekezaji wa kigeni unazua mjadala,” inanukuu taarifa ya TATIC.

Ingawa Tanzania imesaini mikataba mingi ya aina hiyo, uchambuzi wa mwenendo wa uwekezaji unaonyesha kuwa mambo mengine kama “uthabiti wa kiuchumi, mifumo ya udhibiti na ushirikiano wa kikanda yana mchango mkubwa zaidi katika kuvutia uwekezaji”.

Mikataba ya BITs imeundwa ili kutoa ulinzi kwa wawekezaji, ikiwa ni pamoja na haki ya kutendewa kwa usawa, ulinzi dhidi ya utaifishaji wa mali na fursa ya kusuluhisha migogoro katika mahakama za kimataifa.

Dhana ya msingi nyuma ya mikataba hii ni kwamba wawekezaji wa kigeni wako tayari kuwekeza katika nchi ambazo zinatoa ulinzi wa kisheria dhidi ya mabadiliko yasiyotarajiwa ya sera za serikali.

Tanzania imesaini BITs 11 na nchi mbalimbali, zikiwemo Canada, China, Ujerumani na Uingereza. Mikataba mingi ilisainiwa katika miaka ya 1990 na 2000, ikiwa na masharti yanayotoa haki kubwa kwa wawekezaji, wakati mwingine kwa gharama ya mamlaka ya serikali katika kusimamia uchumi wake.

Dhana ilikuwa kwamba mikataba hii ingeongeza uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni kwa kuunda mazingira salama ya uwekezaji. Hata hivyo, uchambuzi uliowahi kufanywa na Policy Forum mwaka 2016 na mwaka 2018 ulionesha kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya mikataba hiyo na uwekezaji nchini.

Kwa maana nyingine ni kwamba hakuna ushahidi unaoonesha kuwa utiaji saini wa makubaliano haya unachochea biashara kati ya Tanzania na nchi mbia.

Je, ni kweli BITs zinavutia uwekezaji?

Kwa mujibu wa Ripoti ya Uwekezaji Tanzania 2022 – Uwekezaji Binafsi wa Kigeni, iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), karibu robo ya uwekezaji wa moja kwa moja (FDI) ilitoka kwenye visiwa vya Cayman. Visiwa hivyo vilichangia Dola za Marekani 344.1 milioni (Sh825 bilioni) mwaka 2022.

Kwa miaka mitatu mfululizo kabla ya 2022 nchi hiyo iliongoza kwa uwekezaji, huku uwekezaji karibu ya nusu (asilimia 45) mwaka 2020 ulitoka kwenye visiwa hivyo.

Mwaka 2022, nchi iliyofuata ilikuwa Uholanzi. Nchi zote mbili hazina BITs na Tanzania. Baada ya hapo zilifuata nchi za Canada, Mauritius na Uingereza (UK) ambazo zina BIT na Tanzania, lakini mpaka sasa nchi 10 kwenye uwekezaji hazina mikataba ya aina hiyo.

Takwimu hazina tofauti kubwa kwa miaka yote mitatu, kwani ni nchi tatu au nne pekee kati ya 10 ndio zenye mikataba ya BIT na Tanzania.

Vilevile, uchambuzi wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wa FDI nchini kati ya 2010 na 2021 uliofanywa na TATIC, unaonyesha matokeo mchanganyiko ya ufanisi wa BITs katika kuvutia uwekezaji.

Uchambuzi huo wa TATIC unazitaja nchi kama Canada, Uingereza na Mauritius, ambazo zina BITs na Tanzania, zimechangia kiasi kikubwa cha uwekezaji, zikifikia takribani dola bilioni 2.29, bilioni 2.64 na bilioni 1.20 mtawalia.

Hii inaashiria kwamba BITs zinaweza kuwa na mchango fulani katika kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na nchi hizo.

Hata hivyo, takwimu pia zinaonyesha kuwa nchi zisizo na BITs kama Afrika Kusini, Nigeria na Kenya zimewekeza kiasi kikubwa nchini Tanzania. Kwa mfano, Afrika Kusini imewekeza takribani dola 2.21 bilioni, huku Nigeria na Kenya zikiwa na uwekezaji wa dola bilioni 1.05 na milioni 724.9 mtawalia.

Hili linaibua swali ikiwa BITs ndizo kichocheo kikuu cha FDI, kwa nini nchi zisizo na mikataba hiyo zinawekeza kwa kiwango kikubwa Tanzania?

“Hii ina maana kwamba wawekezaji huzingatia mambo mengine zaidi ya BITs, kama ukaribu wa kijiografia, uhusiano wa kibiashara, upatikanaji wa malighafi na mazingira thabiti ya kisheria,” uchambuzi wa TATIC ulibainisha. Aidha, baadhi ya wawekezaji wanaoweza kuathiriwa zaidi na mifumo ya ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda ni kama Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), badala ya mikataba ya nchi mbili.

Matatizo zaidi ya BITs

Ingawa BITs zinalenga kuvutia uwekezaji, pia zina changamoto zinazoweza kudhoofisha uhuru wa kiuchumi wa nchi mwenyeji.

Moja ya vipengele vyenye utata zaidi ni mfumo wa Usuluhishi wa Migogoro kati ya Wawekezaji na Nchi (ISDS), unaowapa wawekezaji wa kigeni haki ya kuwasilisha mashitaka dhidi ya serikali katika mahakama za kimataifa.

Uchambuzi wa TATIC ulieleza, Tanzania kama nchi nyingine zinazoendelea, imekumbwa na mashauri kadhaa ambapo wawekezaji wanadai fidia kubwa kutokana na mabadiliko ya sera au migogoro ya kibiashara. Mifano tuliyotaja mwanzo ni baadhi.

Zaidi ya hayo, mikataba mingi ya Tanzania ni ya zamani, ambayo haina vipengele vya kutosha vya kulinda maslahi ya taifa.

Umoja wa Mataifa kupitia Shirika linaloshughulikia Biashara, Uwekezaji na Maendeleo (UNCTAD) umesisitiza umuhimu wa kuiboresha mikataba hii ili kuhakikisha uwiano kati ya ulinzi wa wawekezaji na vipaumbele vya maendeleo ya kitaifa.

Kwa kuzingatia athari mchanganyiko za BITs kwenye FDI, Tanzania inapaswa kuwa makini katika mikataba ya uwekezaji. TATIC wanashauri umuhimu wa kupitia upya mikataba iliyopo ili kujadili upya vipengele visivyo na manufaa kwa nchi.

“Hatua hii inapaswa kujumuisha kuhakikisha kuwa masharti ya BITs yanatoa ulinzi wa haki kwa wawekezaji bila kuzuia mamlaka ya serikali, kupunguza utegemezi wa mfumo wa ISDS, na kuimarisha nafasi ya mahakama za ndani kushughulikia migogoro ya uwekezaji,” ulisisitiza uchambuzi wa TATIC.

Pamoja na BITs, Tanzania inapaswa kuimarisha mazingira yake ya ndani ya uwekezaji kwa kurahisisha taratibu za kibiashara na kuhakikisha uwazi wa sheria. Uwekezaji katika miundombinu, hususan usafirishaji na uhakika wa nishati, ni muhimu katika kurahisisha shughuli za biashara. Vilevile, serikali inapaswa kuimarisha mifumo ya kisheria inayolinda wawekezaji wa ndani na wa nje.

Badala ya kutegemea BITs pekee, uchambuzi huo unasisitiza kwamba nchi inapaswa kutumia fursa za mikataba ya kiuchumi ya kikanda kuvutia uwekezaji. Kuimarisha biashara na uwekezaji ndani ya EAC na SADC kunaweza kuleta manufaa makubwa zaidi kwa uchumi wa nchi.

Ili kupunguza hatari zinazotokana na ISDS, Tanzania inapaswa kuimarisha mifumo ya usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji katika ngazi ya kitaifa na kikanda. Kuhamasisha wawekezaji kutumia mahakama za ndani au vituo vya usuluhishi vya Kiafrika kunaweza kupunguza gharama za kisheria na kuhakikisha maamuzi ya haki.

Uchambuzi wa mazingira ya uwekezaji Tanzania unaonyesha kuwa ingawa BITs zinaweza kuchangia FDI, si kigezo pekee cha uwekezaji.

Nchi zisizo na BITs kama Afrika Kusini na Nigeria zinaonesha uwekezaji mkubwa, hivyo kupinga dhana kwamba BITs pekee zinaweza kuongeza mtiririko wa FDI. Aidha, masharti yasiyo na uwiano katika baadhi ya BITs yanazua maswali kuhusu manufaa yake kwa muda mrefu.

Ili kuhakikisha uwekezaji wa kigeni unaleta manufaa kwa taifa, Tanzania inapaswa kuimarisha mazingira yake ya uwekezaji, kushirikiana na mataifa ya kikanda na kusasisha mikataba yake ya uwekezaji. Kwa kufanya hivyo, nchi itaweza kupata faida zaidi kutokana na uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni, huku ikilinda uchumi wake.