Dar es Salaam. Mwimbaji K-Lynn aliingia katika Bongofleva na kutikisa na kibao chake, Nalia kwa Furaha (2004) akiwa tayari ni maarufu kufuatia kutwaa taji la Miss Ilala kisha Miss Tanzania 2000 na kushiriki Miss World iliyofanyika London, Uingereza.
Wimbo huo uliomtoa uliandikwa na Bushoke baada ya kuagizwa kufanya hivyo na Ruge Mutahaba, kisha wakaenda kurekodi wote studio ya Sound Crafters huko Temeke chini ya mtayarishaji Enrico Figueiro na mengine sasa ni historia.

Hata hivyo, huwezi kuzungumzia historia ya K-Lynn kimuziki na mafanikio yake kwa ujumla bila kugusia uamuziki wake mgumu wa kuachana kabisa na tasnia hiyo baada ya kushindwa kuwa mkubwa kama Mariah Carey.
K-Lynn alichukua uamuzi huo baada kuachia wimbo wake, She Ain’t a flirt (2009) uliotengenezwa Bxtra Records, zamani B’Hits Music Group chini ya Hermy B, na ndio ukawa mwisho wa utumishi wake katika Bongofleva.
“Huwa naulizwa sababu ya kuacha muziki, moja wapo ilikuwa ni ukandamizaji na kutopewa haki kama msanii. Natumaini waliobaki watapigania haki,” alisema K-Lynn mnamo Juni 2013 kupitia mtandao wa X, zamani Twitter.

Ikumbukwe K-Lynn alianza muziki mwaka 1997 katika bendi ya Tanzanite, aliimba hapo kama msanii na mmoja wapo wa viongozi kwa kipindi cha miaka miwili na nusu kisha akaibukia katika mashindano ya Miss Tanzania.
“Baada ya kutwaa Miss Tanzania, nikaacha kuimba na bendi kwa sababu mwaka huo mzima ilibidi kutumikie taji tukifanya shughuli mbalimbali za kijamii,” alisema K-Lynn katika mahojiano yake na Chill na Sky 2018.
“Mwaka 2003 ndipo nikarejea tena kwenye muziki na kuanza kurekodi albamu. Nafikiri nilikuwa na bahati sana kwa sababu nilipotoa tu wimbo wa kwanza ‘Nalia kwa Furaha’ nikiwa na Bushoke ulipokelewa vizuri sana,” alisema.
Ilichukua miaka zaidi ya 10 hadi mrembo mwingine mwenye taji la Miss Tanzania kuingia katika muziki baada ya K-Lynn, na huyu ni Genevieve Emmanuel, Miss Tanzania 2010 ambaye alikuja na wimbo wake wa kwanza, Nana (2017).

Hadi anafikia uamuzi wa kuachana na muziki, K-Lynn alikuwa ametoa albamu mbili, Nalia kwa Furaha (2004) na Crazzy Over You (2007) ambazo zilifanya vizuri na kumtangaza kama mmoja wa waimbaji wakali wa kike Bongo.
Wengi wanamkumbuka K-Lynn kwa nyimbo zake maarufu kama Nikipata Wangu ft. Jay Moe, Nipe Mkono ft. Mr. Blue, Chochote Utapata ft. Noorah, Crazy Over You ft. Squeezer, Nalia kwa Furaha ft. Bushoke, Nipe Chance n.k.
Nyimbo hizo zilimpa umaarufu ila haiondoi ukweli kwamba muziki haukutimiza ndoto yake ya tangu utotoni, nayo ni kuwa mkubwa kama Mariah Carey kutokea Marekani ambaye ameuza rekodi zaidi milioni 200 duniani na kushinda tuzo tano za Grammy.
“Tangu nikiwa mtoto nilitaka sana kuwa mwanamuziki, hiyo ndio ilikuwa ndoto yangu ya kwanza, nakumbuka nilikuwa nikiangalia video za Mariah Carey na Whitney Houston, nikawa natamani siku moja nisimame mbele za watu niimbe na washangilie,” alisema.
“Hivyo nilipokuwa nataka kufanya muziki, kiukweli ndoto yangu ilikuwa kuimba nyimbo za Kiingereza maana niliamini hizo ndizo zitanitambulisha duniani lakini kwa mazingira yaliyokuwepo ilikuwa ngumu kidogo,” alisema K-Lynn.

Ndoto ya K-Lynn katika muziki ilikuwa ni kufikia viwango vya kina Mariah na Whitney na ndio sababu kutoa nyimbo za Kiingereza kama She Ain’t a flirt (2009) ila hakufanikiwa kufika huko kutokana na mazingira ya muziki wa Tanzania.
“Wakati huo maisha ya muziki yalikuwa tofauti na sasa hivi, nawakubali sana watu wanaofanya muziki sasa, mapokezi ni mazuri, fursa ni nyingi, nina furaha kuona vijana wanafanya muziki na unaelekea mbali nje ya nchi ya Tanzania tofauti na zamani,” alisema K-Lynn.
Hivyo hadi anaacha muziki hakuwa amefikia ile ndoto yake ya kuwa wanamuziki mkubwa wa kimataifa, na sababu ni kwamba soko la Bongofleva halipo tayari kumfikisha msanii huko na kile alichodai ni ukandamizaji uliopo katika tasnia.
Na hata katika soko la ndani kuna mambo mengi hayakwenda sawa wake, mathalani licha ya kufanya vizuri hakuwahi kushinda tuzo yoyote ya muziki kuanzia zile za Tanzania Music Awards (TMA) na hata pia za kimataifa.
Mwaka 2008 alichaguliwa kuwania tuzo za TMA kama Msanii Bora wa Kike na ushindi ukaenda kwa Lady Jaydee, vilevile aliwania Wimbo Bora wa Kushirikiana (Crazy Over You) akiwa na Squeezer, ila ushindi ukaenda kwa wimbo wa Mwana FA na AY, Habari Ndio Hiyo.