
Bado ninajiuliza na sijapata majibu ya ni kwa sababu gani tunatunga sheria ya kuwapa kinga wasimamizi wa uchaguzi ambao wanapaswa kutenda kazi kwa kuzingatia haki na weledi ili kuufanya uchaguzi uwe huru wa haki na unaoaminika.
Ni kama nchi yetu imekumbwa na kirusi fulani cha kuwakinga watendaji wanaohusika na haki za raia kwa sababu tulizoea kinga ya kumshitaki Rais iliyopo katika Ibara ya 46(1) ya Katiba ya 1977,lakini sasa ni kama tumeanza kunogewa.
Tukatoka kutoka kwenye kinga ya Rais, mwaka 2020 tukaja na marekebisho ya sheria ambayo inatoa kinga ya kushitakiwa moja kwa moja kwa viongozi wa kitaifa, na badala yake atashitakiwa mwanasheria mkuu wa Serikali (AG).
Kwa hiyo kifungu cha 18(A) kikaongezwa ili kuwezesha mashauri yanayofunguliwa dhidi ya uamuzi wa viongozi wa kitaifa kwa maana ya Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika na Naibu wake na Jaji mkuu yaelekezwe kwa AG.
Nimesema tumeanza kunogewa kwani Kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 uliofanyika Novemba 27 ambao licha ya mapungufu ya dhahiri kabisa na mengine ya kijinai, sheria imefunga milango kwa raia kuwashitaki wahusika.
Sitarajii na naamini wadau wa haki na demokrasia nchini Tanzania, hawatakubali Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kutunga kanuni zenye maudhui kama hayo, kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na Madiwani wa Oktoba 2025.
Ninasema hivyo kwa sababu kifungu cha aina hiyo kinakiuka Katiba na kuifunga mikono na miguu, mhimili wa Mahakama uliopewa dhamana ya kutoa haki kupitia Ibara ya 107(A)(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.
Ibara hiyo inasema mamlaka ya utoaji haki Tanzania itakuwa mikononi mwa Idara ya Mahakama na kwa hiyo hakuna chombo cha Seriikali wala cha Bunge au Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kitakachokuwa na kauli ya mwisho katika utoaji haki.
Tena Ibara ndogo (2) ikasema katika kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia sheria, Mahakama zitafuata kanuni zifuatazo ya kutenda haki kwa wote bila ya kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi na kutochelewesha haki.
Pia mahakama imepewa mamlaka ya ya kutoa fidia ipasayo kwa watu wanaoathirika kutokana na makosa ya watu wengine, na kwa mujibu wa sheria mahususi iliyotungwa na Bunge na kukuza na kuendeleza usuluhishi.
Sasa pamoja na mamlaka hayo ya Kikatiba, waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, akaja na Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 zikaja na kifungu kinachofunga milango raia kudai haki.
Kifungu cha 49 cha Kanuni hizo kikaja na kinga dhidi ya msimamizi wa Uchaguzi, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Msimamizi wa Kituo, Wajumbe wa Kamati ya Rufani au mtumishi yeyote wa umma aliyehusika na usimamizi wa uchaguzi.
Kanuni ikasemawatendaji hao hawatawajibika kwa jinai au madai au kuchukuliwa hatua za kinidhamu au kiutawala kwa jambo lolote alilolifanya au kuacha kufanya kwa nia njema wakati wa kutekeleza majukumu yake chini ya Kanuni hizi.
Uwepo wa vifungu vya aina hii na vingine vyenye maudhui kama haya katika suala nyeti kama uchaguzi ni kukaribisha vurugu kwa sababu uchaguzi unapokuwa sio wa huru na haki na ndio umekuwa kiini cha machafuko katika baadhi ya nchi.
Wapo raia wamejumlisha moja jumlisha moja na kupata mbili kuwa kifungu hicho kiliwekwa kwa makusudi kabisa ili kukinga madudu yote ambayo yalijitokeza na hali hii imewakatisha tamaa baadhi ya wapiga kura kushiriki uchaguzi mbeleni.
Katika uchaguzi mkuu ujao, ni vyema kama nchi, ikatunga sheria na kanuni ambazo hazitaonekana zina vifungu vimewekwa mahsusi ili kulinda maslahi ya Chama Tawala (CCM), kwani ndio itakuwa mwanzo wa vurugu nchini.
Tunayasema haya kwa nia njema kabisa, hasa tukitilia maanani kauli na misimamo ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na viongozi wao kuwa bila kuwepo kwa mabadiliko ya sheria za uchaguzi, uchaguzi mkuu hautafanyika.
Utungaji wa sheria na Kanuni unapaswa uwe shirikishi na uwe wa maridhiano baina ya wadau wa siasa, lakini tukitunga sheria huku mmoja ameficha panga kwa nyuma, hakika tunatengeneza bomu ambalo halina muda mrefu litalipuka.
Tunapotunga sheria tumtizame mama Tanzania, sio maslahi yetu ya kisiasa kwa sababu kinga dhidi ya wasimamizi wa uchaguzi ni kuwapa kibali cha kufanya wanayoyataka na kujiona wako juu ya sheria. Ni hatari kwa nchi.
0656600900