Kwa nini muhimu shule kuwa na wanasaikolojia?

Lengo la adhabu huwa ni kutokomeza au kuondoa tabia isiyofaa kwa mwanafunzi au mtoto.

Fimbo inapotumika mara nyingi huambatana na karipio, ambalo huondoa hali ya kujiamini kwa mwanafunzi au mtoto.

Utafiti mwingi unaonesha mtoto anayekaripiwa mara nyingi huwa katika hatari ya kupoteza uwezo wa kujiamini na kujifunza kwa uhuru, kwa sababu anakuwa kwa sehemu kubwa ametawaliwa na hofu ya kukosea na hivyo kuchapwa.

Ikiwa hatutaki wanafunzi wakosee ni sawa na kusema tunataka wawe maroboti; wapatie muda wote jambo ambalo kitaalamu siyo sawa katika ujifunzaji.

Wataalamu wa saikolojia ya elimu kama B.F.Skinner, wanasisitiza sana kutumia njia chanya kama vile zawadi na motisha kwa wanafunzi na watoto kama sehemu ya kuwafanya wapende shule na wafanye vizuri katika kile ambacho kinaonekana kuwa ni tatizo au siyo kizuri katika jicho la jamii na kielimu. Wanasaikolojia wanasema adhabu inapotolewa lazima iangalie mambo makubwa manne:

Mosi, aina ya kosa na aina ya adhabu. Huna sababu ya kumchapa mtoto au mwanafunzi fimbo kumi kwa kosa la kuchelewa kufika shule au kutofanya kazi fulani.

Kwanza msikilize, ukiona sababu hazina mashiko, jaribu kutengeneza jambo litakalomwezesha kuwahi na kujua madhara ya kuchelewa.

Kwa mfano, wanafunzi watakaowahi wiki hii hawatafagia darasa au watakunywa chai vikombe viwili badala ya kikombe kimoja. Kumbuka motisha izingatie mazingira na muktadha.

Pili, muda wa kutoa adhabu: Adhabu iendane na muda ambao mtoto amefanya kosa. Mtoto au mwanafunzi hatakiwi kuchapwa leo kwa kosa la juzi.Adhabu inatakiwa iendana na maelezo ya kosa alilolifanya mwanafunzi ili ajue kosa lake na madhara yake ili ajifunze.

Tatu, ni muhimu kujua afya ya mwanafunzi kabla ya kumuadhibu kwa sababu watoto wa zama hizi wana matatizo mengi ya kiafya kutokana na aina ya maisha tunayoishi.

Unaweza kuwa na lengo zuri tu la kumuadhibu mtoto kwa lengo la kumfunza, lakini ukajikuta unaishia kuitwa muuaji kwa sababu ulivuka mipaka na kushindwa kudhibiti hasira yako, hivyo ukawa ni sababu ya kifo cha mtoto au ukamsababishia madhara makubwa na hivyo akaichukia hata hiyo elimu yenyewe.

Nne, maeneo ya kupiga.Unapotoa adhabu zingatia sehemu ambazo siyo hatarishi kwa mtoto au mwanafunzi kama vile kichwani, mgongoni, usoni miguuni na kifuani.

Haya ni maeneo hatari kwa mwanafunzi kwa sababu hujui afya yake ikoje.Siku zote toa adhabu huku ukibaki kuwa salama kwa kutoa adhabu ya kisheria na kuchapa sehemu zilizoruhusiwa.

Wanafunzi wana changamoto za ukuaji(balehe) ambao ni aina fulani hivi ya uchizi.

Wanafunzi wetu wamekua kimwili na kihisia lakini kiakili na kifikra bado ni wachanga sana na hivyo wanahitaji sana uangalizi wa kimalezi.

Hisia zinaweza kuwasababishia waone kuwa wanaweza kufanya chochote na wakati mwingine hisia hizo hizo zinaweza kuwasukuma na kuona kama wako sawa tu na walimu wao kwa sababu wanalingana urefu au maumbile

Ni muhimu sana kutumia saikolojia ya ualimu na saikolojia ya malezi, kukabiliana na changamoto za tabia zisizofaa kwa wanafunzi kuliko kukabiliana nao kwa aina ya makosa wanayoyafanya.

Wanafunzi wanakulia katika mazingira na familia tofauti, hivyo wanahitaji uangalizi wa kimalezi zaidi.

Ni wakati sahihi sasa kwa Serikali kuajiri wanasaikolojia wa mambo ya kielimu (educational psychologists) ili kukabiliana na changamoto za wanafunzi shuleni.

Ni ukweli usiopingika kuwa walimu wanafundishwa saikolojia ya kuwajua wanafunzi wapokuwa vyuoni na namna ya kukabiliana na tabia zao, lakini bado saikolojia hiyo wanayofundishwa walimu imekaa kiujumla sana na siyo toshelezi kimalezi.

Tutapiga hatua kubwa sana kielimu kama utafika wakati ambao kila ofisi ya nidhamu shuleni, itakuwa na mwanasaikolojia atakayejua wakati gani utumike ushauri na unasihi, viboko au adhabu nyingine.