
Ni ukweli ulio dhahiri kuwa Tanzania tuko katika mkwamo wa safari ya kuandika Katiba mpya na ukichunguza sana utabaini maslahi ya kisiasa ndio kizingiti cha mchakato huu, ndio maana nauliza, mnaonaje Katibampya ikiandikwa na wasomi?
Nasema hivyo kwa sababu ukichunguza mkwamo tulio nao, kwa sehemu kubwa unatokana na wahafidhina (conservatives) ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambao wanahofu isiyo na maana yoyote, kuwa Katiba mpya ni kifo cha CCM.
Mchakato wa kuandika Katiba ulioanzishwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, kupitia salamu zake za mwaka mpya 2011, ulianza vizuri sana, lakini ghafla matumaini ya watanzania, yakazimwa katika Bunge Maalum la Katiba 2014.
Ukweli una sifa moja kuu kwamba hata ukiuchukia au kuukataa, haugeuki kuwa uongo, hivyo kamwe hatuwezi kupata Katiba mpya katika mazingira ambayo CCM inahofia maslahi yake ya kushika Dola, upinzani nao wanavutia maslahi yao.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba ilifanya kazi yake ya kutukuka na hadi leo, rasimu ya pili ya Katiba ya Tume hiyo ndio inaonekana kuwa bora na hata ukiisoma leo huoni tatizo labda katika muundo wa muungano.
Bunge Maalum la Katiba, likiwa na wajumbe wengi kutoka CCM, lililazimisha na kutuletea Katiba Inayopendekezwa ikiondoa mapendekezo muhimu yaliyobeba maoni ya wananchi, kwa sababu tu yalikuwa yanatishia maslahi ya CCM.
Kosa kubwa ambalo tutalijutia na pengine ni kiini cha mchakato wa Katiba mpya kukwama, ni kuruhusu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuteua wajumbe na kuruhusu wanasiasa kuwa sehemu ya wajumbe wa Bunge hilo.
Lilikuwa ni kosa kubwa sana sheria namba 8 ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, kuwateua wabunge wa Bunge la Jamhuri na wale kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuwa wajumbe na wengi walitokana na chama tawala CCM.
Ndio maana nimetangulia kushauri kuwa ili tutoke katika mkwamo huu, kwanza kunahitajika utashi wa kisiasa na nguvu ya umma halafu pili wanasiasa wakae pembeni na nafasi yao ichukuliwa na wanazuoni wasio na upande wa kisiasa.
Nashauri hivyo kwa sababu, kwanza CCM imekuwa na mbili katika suala hili, kwanza Katiba Mpya sio kipaumbele chao, lakini Juni 2022 ikabadili gia angani na kukubali mchakato huo, lakini kikataka maslahi mapana ya Taifa yazingatiwe.
Tangu CCM kitoe kauli hiyo Juni 22, 2022, sasa zimepita siku 969 hadi kufikia leo na hakuna matumaini ya mchakato huo kuanza wala uwepo wa mabadiliko madogo katika Katiba ya sasa, ili kuruhusu mifumo ya uchaguzi huru na haki 2025.
Ni kukosekana kwa mifumo hiyo ambayo ni pamoja na sheria bora za uchaguzi na Tume Huru ya Uchaguzi yenye sifa na vigezo vya kuwa Tume huru, ndio maana Chama Kikuu cha Upinzani (Chadema), kinasema “no reforms, no election.”
Pamoja na msimamo huo wa Chadema unaoungwa mkono na vyama makini, CCM kupitia makamu mwenyekiti wake, Steven Wassira kinasema uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 uko pale pale licha ya vyama vya upinzania kulalamikia mifumo.
Kwa mazingira ya kisiasa tuliyonayo, sioni CCM watakubali kwenda kwenye uchaguzi mkuu na katiba mpya au kukubali uchaguzi usogezwe mbele ili kuruhusu kupatikana kwa katiba mpya itakayozaa Tume Huru, sababu nini? Hofu ya maslahi ya kisiasa.
Nimejaribu kueleza mazingira tuliyonayo ili kujenga msingi wa kuonyesha kuwa tunashindwa kufikia ndoto ya kuwa na Katiba mpya kwa sababu tu ya wanasiasa, walituvuruga Bunge Maalum na sasa wanayumbisha kufufua mchakato huu.
Ni lazima tutambue kuwa ili tutoke hapa tulipo, ni lazima tuuondoe mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya kutoka mikononi mwa Rais na Serikali ya CCM na uwe ni mali ya watanzania, wala isionekane ni fadhila kutoka kwa Rais au CCM.
Bila kufanya hivyo, tutaendelea kuhadaiwa kuwa Katiba mpya haileti chakula na huduma za kijamii lakini wakati ukweli ni kuwa Katiba mpya itatuletea mifumo bora na taasisi imara ikiwamo Tume Huru, Mahakama Huru na Bunge Huru.
Kwa mujibu ripoti inayochapwa na Economist Intelligence Unit (EIU), inaonyesha kwa mwaka 2024, nchi 10 zilizokuwa na Katiba bora ni Maritius, Botswana, Cabo Verde, Afrika Kusini, Namibia,Lesotho, Malawi, Zambia, Liberia, Ghana na Kenya.
Katiba za nchi hizo walau zinatoa hakikisho la kuwa na utawala wa sheria, Tume Huru ya Uchaguzi inasimamia uchaguzi huru, haki na unaoaminia, Mahakama Huru na Bunge Huru lisilofungamana na Serikali iliyopo madarakani.
Ukisoma ripoti hiyo, zinakuambia nchi hizo ndizo zenye Katiba bora zinazotoa hakikisho la demokrasia ya kweli, uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya Habari, Haki za Binadamu na Uwazi katika uendeshaji wa Serikali za kidemokrasia.
Tunaweza kupita njia waliyopita majirani zetu Kenya, katika safari ya kuisaka Katiba mpya ambayo ilikuwa shirikishi na ilianza kwa kuunda Kamati ya wataalamu ambao ndio waliandika rasimu ya Katiba na kuitoa kwa umma Novemba 17, 2009.
Umma wa wana Kenya ulipewa siku 30 kuipitia rasimu hiyo, kutoa maoni yao na kupendekeza marekebisho kama yapo na baada ya hatua hiyo, rasimu hiyo ya Katiba ilipelekwa kwenye kamati ya Bunge ya masuala ya Katiba, Januari 8, 2010.
Kamati hiyo ya Bunge ndiyo ilipitia, kuifanyia maboresho na kuirudisha kwa kamati ya wataalamu, ambapo Kamati ili ilichapisha Katiba inayopendekezwa Februari 23, 2010 ambayo ilipelekwa Bungeni kwa ajili ya marekebisho ya mwisho.
Kwa hiyo, kwa pamoja, wanasiasa na wanazuoni walifanya kazi kubwa ya kuiweka vizuri Katiba na ujue kamati ya wataalamu ilihusisha watu kutoka fani mbalimbali na huu mchanganyiko ulizaa Katiba bora iliyokuwa na utashi wa kisiasa na wasomi.
Lakini ulikuwa na uhalali wa kisiasa kwa sababu maoni ya wananchi yalizingatiwa na kutengeneza msingi wa Katiba ya Kenya, hapa kwetu tulitanguliza mguu vibaya, tukawapa madaraka makubwa wanasiasa kupitia Bunge Maalum la Katiba.
Bila kuwaondoa wanasiasa katika mchakato wa kuandika Katiba mpya, na ninaposema wanasiasa ni pamoja na Rais, kamwe Tanzania isitegemee kuandika Katiba mpya, labda tuandike baada ya kulazimishwa na nguvu ya umma.
Ninataka niseme, tunachokifanya ni kuchelewesha tu kupatikana kwa Katiba mpya, bali utafika wakati tutaiandika tupende wala tusipende maana ni kama kuzuia mafuriko kwa mikono. Umma utakapoamua, Katiba itaandikwa tu.
Nitahadharishe, kuna gharama kubwa kusubiri shinikizo la umma, kwani linaweza kuja na madhara makubwa ambayo yanaweza kuepukika, kwanini tusiiandike Katiba sasa wakati nchi bado ina upendo, amani, umoja na mshikamano?
Ninayasema haya kwa sababu tupo katika kizazi cha Gen-Z ambacho wala hakimfahamu Nyerere, kitatumia nguvu ya umma kudai haki ya ajira, haki za binadamu, hali bora ya maisha na hapo ndipo tutakumbuka shuka kumepambazuka.
0656600900