Kwa mastaa hawa ni zaidi ya mahusiano 

Dar es Salaam. Katika tasnia ya burudani Bongo hasa upande wa muziki, kuna ‘couple’ nyingi za mastaa ambazo mahusiano yao wamekuwa na nguvu kubwa ya ushawishi kitu kinachorahisisha kukubalika kwa kazi zao kwa kiasi fulani.

Kutokana na hilo, wamekuwa wakishirikiana sana katika kazi zao, mfano unakuta mmoja ni mwanamuziki hivyo anamtumia mwenzake katika video ya wimbo wake au wote ni wanamuziki hivyo wanashirikiana katika nyimbo zao kama ifuatavyo.

Diamond & Zuchu

Kwa mujibu wa Zuchu, uhusiano wake na Diamond Platnumz una miaka minne sasa, ila ilichukuwa muda mrefu hadi wenyewe kuja kuweka wazi licha ya tetesi nyingi, kwao kazi ndiyo inaongea zaidi kuliko uhusiano wao.

Ndani miaka hiyo minne wametoa pamoja nyimbo tano, Cheche (2020), Litawachoma (2020), Mtasubiri (2022), Raha (2024) na Wale Wale (2024), huku Diamond akitokea katika video ya wimbo wa Zuchu, Utaniua (2023).

Rayvanny & Fahyma

Takribani miaka 10 sasa wapo pamoja, Fahyma alikuwa na Rayvanny tangu anatoka na wimbo wake wa kwanza, Kwetu (2016) chini ya WCB Wasafi na alionekana katika video yake na mwaka uliofuta wakapata mtoto wao wa kwanza.

Kwa jumla Fahyma ambaye anafanya mitindo na filamu, ametokea katika video za mpenzi wake huyo sita ambazo ni Kwetu (2016), Natafuta Kiki (2016), Siri (2017), Forever (2023), Habibi (2023) na Mwambieni (2023). 

Nahreel & Aika (Navy Kenzo)

Walikutana miaka 16 iliyopita na kupendana na sasa wana watoto wawili, hadi mwaka 2013 ndipo Nahreel na Aika wakaanzisha kundi la Navy Kenzo, mradi ambao umefanikiwa na sasa wanatazamwa na wengi kama mfano bora kwa jinsi walivyodumu muda mrefu.

Tayari Navy Kenzo wametoa albamu tatu, AIM (Above Inna Minute) (2016), Story Of The African Mob (2020) na Most People Want This (2023), huku wakianzisha lebo, The Industry ambayo ilimtoa Rosa Ree, mshindi wa tuzo mbili za muziki Tanzania (TMA) 2022.

Marioo & Paula

Tangu Aprili 2023, ndipo tetesi za wawili hawa kutoka pamoja zilianza, Marioo na Paula wameendelea kuwa wote kwa utulivu mkubwa wakiwa tayari wamejaliwa mtoto mmoja, Princesss Amarah, huku wakishirikiana kimuziki.

Paula ambaye ni binti wa Kajala Masanja na P-Funk Majani, tayari ametokea katika video tatu rasmi za Marioo ambazo ni Lonely (2023), Tomorrow (2023), Sing (2023), na ambazo sio rasmi (visualizer) ni mbili, Hakuna Matata (2024) na Unachekesha (2024)

Jux & Priscilla

Wawili hawa waliweka wazi uhusiano wao Julai 2024 na kuja kufunga ndoa Februari mwaka huu, Jux na Priscilla ambaye ni binti wa mkongwe wa Nollywood, Iyabo Ojo, wamekuwa wakishirikiana katika kazi zao na zaidi wamekuwa wakisafiri sana pamoja.

Kwa kipindi kifupi cha uhusiano wao, Priscilla akiwa kama mshawishi wa chapa mtandaoni ametokea katika video mbili za mume wake ambazo ni Ololufe Mi (2024) na Si Mimi (2025) ambayo kwa sehemu kubwa imeonyesha tukio la kuvinjwa pete ya uchumba.

Billnass & Nandy

Wakiwa wote ndio wanaanza kupata umaarufu, mwaka 2016 waliitwa katika tamasha la Fiesta, wakaenda kutumbuiza Sumbawaga ila wakaenda kulala Mbeya na huko ndipo uhusiano ulianza hadi walipokuja kufunga ndoa Julai 2022 na sasa wana mtoto mmoja.

Kimuziki tayari wameshirikiana katika nyimbo tano ambazo ni Bugana (2019), Do Me (2020), Party (2021), Bye (2022) na Totorimi (2024) huku Billnass akitokea katika video ya wimbo wa Nandy, Napona (2022) akimshirikisha Oxlade wa Nigeria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *