Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah, kwa mara ya kwanza, imeshambulia kwa makombora kambi kubwa ya jeshi la anga la utawala wa Kizayuni wa Israel, ikiwa ni sehemu ya ulipizaji kisasi dhidi ya ukatili unaofanywa na utawala huo ghasibu.
Hizbullah imetangaza kuwa imeilenga kambi ya HaHotrim, ambayo ni kituo muhimu sana cha makazi ya asakri wa jeshi la anga la utawala wa Kizayuni, kinachojumuisha miundo ya usafirishaji na kiwanda cha injini.
Kituo hicho kiko kusini mwa mji unaokaliwa kwa mabavuu wa Haifa, yapata kilomita 40 kutoka mpaka wa Lebanon na Palestina.
Taarifa ya Hizbullah imesema, shambulio hilo ni sehemu ya mfululizo wa operesheni za Khaybar, ambazo zinavilenga vituo nyeti vya kijasusi vya utawala wa Kizayuni na maeneo yake mengine ya kimkakati.
Mbali na operesheni hiyo, Hizbullah imeshambulia pia kwa msururu wa ndege zisizo na rubani kituo cha kamandi ya Brigedi ya Ramim kwenye kambi ya Hunin, na kuzilenga kwa usahihi shabaha zilizokusudiwa.

Ndege hizo zisizo na rubani zimekilenga kituo cha vifaa cha Kitengo cha 146 kilichoko kaskazini mwa kijiji cha Sheikh Dannun, mashariki mwa Nahariya.
Wanamapambano wa Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon wameshambulia pia kwa makombora kambi ya Shraga iliyoko kaskazini mwa mji unaokaliwa kwa mabavu wa Akka.
Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimeripoti kuwa walowezi wawili wabeba silaha wameuawa huko Nahariya na wengine kadhaa wamejeruhiwa kutokana na mashambulio hayo.
Operesheni za mashambulizi za Hizbullah ni jibu kwa uvamizi wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Lebanon, ambao umepelekea Walebanon zaidi ya 3,000 kuuawa shahidi tangu Oktoba 2023.
Harakati hiyo ya Muqawama wa Kiislamu imeshadidisha operesheni zake za kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa Kizayuni tangu Katibu Mkuu wa harakati hiyo Sayyid Hassan Nasrullah alipouawa shahidi mwezi Septemba katika shambulio la kinyama lililofanywa na jeshi la Kizayuni…/