Kwa mara nyingine UK yatakiwa iache kuipa silaha Israel inayofanya jinai Ghaza na Lebanon + Picha

Kwa mara nyingine tena waandamanaji waliomiminika mitaani huko Uingereza wameitaka nchi hiyo ya kifalme ambayo ni muungaji mkono mkubwa wa jinai za utawala wa Kizayuni, iache kuipa silaha Israel na isishiriki katika jinai zinazofanywa na dola hilo pandikizi hasa huko Ghaza na Lebanon.

Press TV imetangaza habari hiyo na kuandika kuwa, ndani ya eneo la makazi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, kumefanyika maandamano ya dharura ya kuunga mkono Palestina yakiwa ni moja kati ya maandamano mengine mengi yaliyofanyika nchini humo yakimtaka Keir Starmer aache kuipa silaha Israel kama njia ya kukomesha jinai zake huko Palestina na Lebanon.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Uingereza imekuwa ikishiriki moja kwa moja katika vita na mauaji ya halaiki huko Ghaza na sasa Lebanon. Jambo hilo linalotisha limekuwa likifanywa na Uingereza kwa kuipa Israel mamia ya ndege za upelelezi na kufanya ujasusi dhidi ya wakazi wa Ghaza.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Uingereza na nchi kadhaa za Ulaya zinaendelea kuupa utawala wa Kizayuni silaha zilizopigwa marufuku ambazo inazitumia kufanya jinai dhidi ya Wapalestina na Walebanon. 

Mwezi Septemba mwaka huu, serikali ya chama cha Leba cha Uingereza ilisitisha leseni 30 kati ya 350 za kuiuzia silaha Israel. Chama hicho kilisema kuwa leseni hizo zilikiuka sheria za kimataifa za kibinadamu.

Baada ya miezi kadhaa ya maandamano makubwa ya kupinga jinai za Israel, hatimaye serikali ya Uingereza imesitisha chini ya asilimia 10 ya leseni hizo na haitarajiwi kama itapiga marufuku kikamilifu. Waandamanaji wanaendelea kurudi mitaani kwa idadi kubwa na ndogo, ili kushinikiza kukomeshwa kabisa kupewa silaha utawala wa Kizayuni. 

Hapa chini tumeweka picha za maandamano hayo:

Uingereza inalaumiwa kwa kushiriki moja kwa moja kwenye jinai za Israel huko Ghaza na Lebanon