Kwa mara nyingine Ronald Lamola ataka kukomeshwa vita mara moja Ghaza

Kwa mara nyingine tena, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini ametaka kukomeshwa vita mara moja katika Ukanda wa Ghaza huko Palestina na kufikishiwa misaada wakazi wa eneo hilo haraka iwezekanavyo.

Ronald Lamola alitoa mwito huo jana mjini Cairo Misri baada ya mazungumzo yake na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Badr Abdelatty.

Alisema hayo mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa: “Usitishaji mapigano wa mara moja na wa kudumu unahitajika huko Ghaza na juhudi zinapaswa kufanywa kutafuta utatuzi madhubuti wa amani kuhusu kadhia ya Palestina kwa msingi wa suluhisho la serikali mbili.” 

Afrika Kusini ilifungua kesi dhidi ya Israel mwezi Disemba, ikiituhumu kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina huko Ghaza.

Mahakama ya kimataifa yenye makao yake mjini The Hague Uholanzi, hadi sasa imeshatangaza awamu tatu za hatua za dharura na kuiamuru Israel kusitisha mashambulizi yake huko Rafah na kufungua vivuko zaidi vya ardhini kwa ajili ya kufikishiwa misaada wakazi wa Ghaza.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Afrika Kusini iliwasilisha ushahidi zaidi wa kutilia nguvu shauri lake dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye mahakama hiyo ya kimataifa.