Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vimeendelea kuyatwanga kwa makombora maeneo tofauti ya utawala wa Kizayuni na kuzidi kuifedhehesha na kuidhalilisha mifumo ya ulinzi wa makombora ya Israel iliyogaiwa na madola ya kibeberu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, vyombo vya habari vya Kizayuni leo asubuhi vimetangaza habari ya kufanyika shambulio jipya la Yemen dhidi ya mji wa Beit Shemesh wa kusini mwa Baytul Muqaddas na kusababisha moto mkubwa.
Jeshi la Israel limedai kuwa, limetungua kombora hilo la Yemen lakini duru za ndani ya utawala wa Kizayuni zimesambaza picha na mikanda ya video inayoonesha kuwa kombora hilo la Yemen limepiga shabaha iliyokusudiwa katika mji wa Beit Shemesh na kusababisha moto mkubwa.

Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vimetangaza kuwa vimeutwanga mji huo wa Kizayuni kwa kombora la hypersornic ikiwa ni sehemu ya kuwaunga mkono wanamapambano wa Palestina na Lebanon na kuongeza kuwa, kombora lililotumika kuupiga mji huo wa Wazayuni ni la “Palestina 2.” Taarifa hiyo imefafanua zaidi kwa kusema, kombora hilo la “Palestina 2” limepiga kambi ya kijeshi ya Nahal Surik ya Israel huko kusini mashariki mwa Yafa.
Amma lililo muhimu zaidi ni kwamba mifumo yote ambayo madola ya kibeberu ya Magharibi yameipa Israel ili ijikinge na mashambulizi ya makombora, imedhalilishwa tena na Yemen kwa kushindwa kuzuia kombora hilo.