
LICHA ya KenGold kuendelea kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja haijawa ishu kwa kiungo Zawadi Mauya anayeamini bado timu hiyo ina nafasi kubwa ya kusalia Ligi Kuu.
Mauya amesema kinachotakiwa kwa sasa wao kama wachezaji kuongeza umakini katika kusaka ushindi kwenye mechi zilizosalia.
Timu hiyo ambayo jana ilicheza dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, baada ya hapo itakuwa na mechi sita za kujitetea kuepuka kushuka daraja kwani kabla ya mchezo dhidi ya Azam ilikuwa mkiani mwa msimamo na pointi 16.
Mauya anayeitumikia KenGold kwa mkopo akitokea Singida Black Stars, anaamini kutokana na hivi sasa msimamo kuonesha timu kupishana pointi chache sana, lolote linaweza kutokea kwa aliyeko chini kupanda nafasi za juu.
“Japokuwa ni mara yangu ya kwanza kucheza timu inayopambania kushuka daraja, ila naona bado tuna nafasi ya kusalia Ligi Kuu, kama wachezaji kazi yetu ni moja kujitoa kwa kadri tuwezavyo,” alisema Mauya na kuongeza.
“Timu zilizopo juu yetu zingine tumepishana nazo pointi mbili kama Tanzania Priosns, Kagera Sugar wana pointi 19, Pamba Jiji 22, kwa hesabu hizo unaweza kuona hakuna timu iliyo na uhakika wa kusalia.”
KenGold ambayo imepanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu huu, katika mechi sita zijazo itacheza tatu nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons, Pamba Jiji na Simba, huku zingine za ugenini dhidi ya Dodoma Jiji, Coastal Union na Namungo.