
Dar es Salaam. Maisha yanaendelea, hayasimama! Pale Jangwani na Msimbazi katika mitaa miwili iliyopo kwenye eneo maarufu la Kariakoo jijini Dar es Salaam kuna mambo yanaendelea kupikwa, ambapo watani wa jadi Yanga na Simba wanatarajiwa kukutana katika mchezo wa dabi ya 114, Jumamosi, wiki hii.
Timu hizo mbili zinatarajiwa kukutana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Lakini, achana na mchezo huo uwanjani, lakini nyuma ya pazia vichwa vinawauma viongozi, wachezaji na hata mashabiki wakiwaza nini kitakachotokea siku hiyo ambayo itakuwa ya kipekee kwa timu hizo na huenda ikatoa mwelekeo wa ubingwa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Wakati ukitafakari hayo, pale Msimbazi miongoni mwa maswali wanayojiuliza mashabiki wa Simba katika kikosi chao hasa eneo la ushambuliaji ni nani atakayeongoza safu hiyo kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi dhidi ya watani zao, Yanga.
Ni Steven Mukwala, mshambuliaji mwenye kasi aliyefunga hat trick dhidi ya Coastal Union, au Leonel Ateba ambaye alianza mechi ya duru la kwanza?
Hii ni changamoto kubwa kwa Kocha wa Simba, Fadlu Davids, ambaye anahitaji kufanya uamuzi mgumu katika mchezo huo wa kihistoria.
Katika michezo ya hivi karibuni, Fadlu ameonekana kuwa na mbinu tofauti kwenye safu ya ushambuliaji, huku akimtumia zaidi Ateba lakini mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Coastal alimpumzisha, akimpa nafasi Mukwala ambaye aliendeleza ubora wake kwa kufunga hat trick, hivyo kufikisha mabao manane.
Hali hii inaonyesha washambuliaji hawa wawili wanakutana kwa idadi sawa ya mabao, lakini kila mmoja amepitia njia tofauti kufikia hapo, jambo linalomfanya Fadlu kuwa na changamoto kubwa katika kufanya uamuzi kuhusu nani ataanza dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Mukwala, ambaye amekuwa akicheza kwa muda mfupi, ameonyesha uwezo wa kufunga mabao kwa haraka zaidi kuliko Ateba. Katika dakika 833 tu, Mukwala amefikisha mabao manane.
Hii ni tofauti na Ateba ambaye amecheza dakika 1168 kufikia idadi hiyo, akionyesha ni mchezaji anayehitaji muda mrefu zaidi ili kufikia kiwango cha juu. Hata hivyo, tofauti hii ya muda haimanishi Mukwala ni bora zaidi ya mwenzake kwani Ateba pia amekuwa na mchango mkubwa kwa timu.
Licha ya kuwa wote ni washambuliaji wa mwisho, wachezaji hawa wawili wanajivunia sifa za kipekee zinazowatofautisha. Ateba ni mchezaji mwenye nguvu na uwezo wa kutumia mabavu kwa ufanisi, jambo ambalo linamfanya kuwa hatari katika hekaheka na mashambulizi ya moja kwa moja.
Mukwala, kwa upande mwingine, anajivunia ufundi mkubwa mguuni, akiwa na uwezo wa kuchezea mipira kwa ufanisi na kutumia kasi yake kwenye mashambulizi ya kushtukiza. Katika mchezo wa duru la kwanza dhidi ya Yanga na Simba ilipoteza kwa bao 1-0, Ateba alishindwa kufurukuta mbele ya mabeki wa Yanga, Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ alipocheza kwa dakika zote.
Ikumbukwe kabla ya mchezo huo, Ateba alitamba kuifunga Yanga akibainisha hakuona beki wa kumbabaisha jambo lililowafanya Job na Bacca kuwa makini naye.
Kabla ya hapo, Mukwala naye alianza katika Kariakoo Dabi ya Ngao ya Jamii ambayo Simba ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga akicheza dakika zote 90, huku ile ya pili akitokea benchi na kuingia dakika za mwishoni.
Washambuliaji hao kila mmoja amepewa nafasi ya kuanza na kocha Fadlu katika Kariakoo Dabi na kushindwa kufunga.
MSIKIE FADLU
Akizungumzia safu yake ya ushambuliaji kwa sasa, Fadlu amesema inampa matumaini na mwanga katika mpango wa kukijenga kikosi hicho kuwa tishio kwa miaka mingi ijayo kuanzia katika mashindano ya ndani hadi kimataifa.
“Nafurahia kuona kila mchezaji akifanya vizuri katika kila nafasi na kila mmoja ana mchango wake kwenye timu, ni ngumu wote kucheza kwa wakati mmoja, hivyo kila ambaye anapata nafasi anapaswa kuonyesha,” amesema kocha huyo.