
Parstoday- Mtaalamu wa masuala ya kimataifa na mtumiaji wa mtandao wa kijamii wa X, ameitambua hatua ya utawala wa Kizayuni kumuua shahidi “Mohammed Afif Al Nabulsi” aliyekuwa Mkuu wa vyombo vya habari vya Hizbullah ya Lebanon, ni ishara ya kuwa chungu operesheni za vyombo vya habari vya Hizbullah dhidi ya utawala huo.
Mohammad Afif, afisa wa habari wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon aliuawa shahidi juzi Jumapili katika shambulio la utawala wa Kizayuni huko Ras al-Naba, Beirut mji mkuu wa Lebanon.
Kulingana na Parstoday, Shahidi Muhammad Afif Al Nabulsi, ambaye alijulikana kama “Haj Muhammad” ndani ya Hizbullah Lebanon, alijiunga na vuguvugu hili mnamo 1983 na alichukuliwa kuwa mmoja wa wanachama waanzilishi wa Hizbollah. Tangu mwanzo, alikuwa na nafasi muhimu na athirifu katika muundo wa Harakati ya Hizbullah, na baada ya muda, akawa mmoja wa watu muhimu wa harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu.
Mwaka 2014, Shahid Afif aliteuliwa kuwa afisa wa uhusiano wa vyombo vya habari wa Hizbullah na akawa na nafasi muhimu katika kufikisha ujumbe na uratibu wa vyombo vya habari vya harakati hiyo ndani ya Lebanon na katika uga wa kimataifa hususan katika nyakati za migogoro na mizozo na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Katika jinai zilizofanywa na utawala wa Kizayuni baada ya tarehe 7 Oktoba 2023, Shahidi Afif alitangaza uungaji mkono madhubuti wa Hizbullah kwa muqawama wa Palestina na kusisitiza kuwa, harakati hiyo itaendelea kusimama pamoja na mataifa ya Kiislamu.
Katika wiki za hivi karibuni, kutokana na kushadidi mashambulizi ya jeshi la Israel dhidi ya Lebanon hususan baada ya kuuawa shahidi Seyed Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa harakati hiyo, mkuu huyo wa vyombo vya habari wa Hizbullah ya Lebanon amekuwa akifanya mkutano na waandishi wa habari karibu kila siku na kujibu maswali yao.
Hivi karibuni Shahid Afif alivipa changamoto vitisho vya utawala wa Kizayuni na kusema katika mkutano na waandishi wa habari: Hatuogopi shambulio lenyewe, achilia mbali vitisho, irada yetu ni thabiti na muqawama wetu umesimama imara.
Kuuawa shahidi Mohammad Afif na utawala wa Kizayuni kumeibua hisia kubwa kutoka kwa watumiaji wa mtandao wa X wa Iran wakiwemo watu mashuhuri.
Mohammad Saeed Ahadian, msaidizi wa kisiasa na vyombo vya habari wa Spika wa Bunge la Iran akizungumzia kuuawa shahidi Mohammad Afif Al Nabulsi, amesema, kuchukua wigo mpana mijadala na mazungumzo ya muqawama katika eneo na dunia ni mdaiwa wa muongo wa jitihada zake za kijihadi katika Hizbullah.
Ahadian ameongeza: Hii leo, Hizbullah si mahususi tena kwa Lebanon, na bendera ya Hizbullah imetundikwa na inapepea kwa fahari katika sehemu mbalimbali za dunia.
Sayyid Mohammad Hosseini, Waziri wa zamani wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu wa Iran, na Mehdi Torabi, mchezaji wa mpira wa Iran, walikuwa miongoni mwa watumiaji wengine mashuhuri wa Iran wa mtandao wa kijamii wa X wameonyesha radiamali zao kuhusiana na kuuawa shahidi Mkuu wa Vyombo vya Habari vya habari na msemaji rasmi wa Hizbullah nchini Lebanon.
Hosseini amemtambulisha Shahidi Mohammad Afif Al Nabulsi kama Mujahidi asiyechoka wala kutetereka, sauti kubwa na msimuliaji wa muqawama wa mashujaa wanaume na wanawake wa Lebanon.
Mehdi Torabi, mchezaji wa mpira wa miguu wa timu ya taifa ya soka ya Iran, pia ameandika kuhusu hili kwenye X: Alikuwa msimulizi wa jinai za utawala wa Kizayuni kwa sauti yake mwenyewe.
Katika ujumbe mwingine katika mtandao wa kijamii wa X, “Mohammed Mahdi Rahimi”, mtaalamu wa masuala ya kimataifa ameandika: “Majaribio ya mara kwa mara ya utawala wa Kizayuni kutaka kumuua Mohammad Afif yanaonyesha hali chungu ya operesheni za vyombo vya habari vya Hizbullah dhidi ya utawala huo.”
Rahimi ameongeza kuwa: Tangu mwanzo muqawama wa Kiislamu wa Lebanon uliweka nafasi maalumu kwa vyombo vya habari, na kadiri muundo wake unavyoendelea, uelewa wake wa vyombo vya habari na uanaharakati katika uwanja huu ulipanuka.