Kusiluka awataka wakaguzi wa ndani kuheshimiwa

Dodoma. Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka, amezitaka taasisi za Serikali na binafsi kuwaheshimu wakaguzi wa ndani na kuwekeza katika maendeleo yao ili kukuza mchango wao.

Dk Kusiluka ameyasema hayo leo Ijumaa, Mei 2, 2025 jijini Dodoma, wakati wa kufungua mkutano wa mwezi wa ukaguzi wa ndani ulioandaliwa na Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani Tanzania.Amezihimiza taasisi zote za umma na binafsi kutumia muda kuwaheshimu wakaguzi wa ndani, kuwekeza katika maendeleo yao na kukuza mchango wao.

Pia amewataka kutumia ipasavyo vitengo vyao vya ukaguzi wa ndani viongozi wa Serikali, taasisi za umma, menejimenti na bodi kuwathamini.

Amesema kinyume chake, iwapo watawapuuza, kuwadharau au kuwanyanyapaa wakaguzi wao wa ndani, tija inakosekana.

“Uzoefu unaonesha kuwa matatizo mengi yanayoikumba Serikali na taasisi za umma kwa hoja za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), yanatokana na kupuuzwa kwa taarifa na tahadhari za mapema zinazotolewa na wakaguzi wa ndani,” amesema.

Aidha, amewataka wakaguzi kufanya kazi kwa weledi na si kuwatisha watu wala kuwafanya wawaogope

“Kumeibuka taarifa kuwa baadhi ya wakaguzi wa ndani wanaogopeka. Sasa, kama mnaweka hofu, hilo halisaidii. Ni wajibu wenu kuwaonesha waajiri na wenzenu kazini kuwa nafasi yenu ni muhimu kwa mafanikio ya taasisi,” amesema.

Pia amewataka watumie muda mwingi katika kujenga, kuimarisha na kudumisha mifumo ya udhibiti wa ndani kwa taasisi zao.

“Nasema haya kwa sababu imekuwa kawaida kuona baadhi ya wakaguzi wa ndani katika taasisi za Serikali wakijihusisha na kazi zisizo rasmi nje ya vituo vyao, jambo linalowanyima muda wa kushughulikia masuala ya msingi ya taasisi zao,” amesema.

Amesema taasisi zinafanya kazi kwa ufanisi, tija na uadilifu, na kuwa kupitia maboresho ya sheria na sera, Serikali imeweka msingi madhubuti kwa ajili ya kazi za ukaguzi wa ndani katika wizara, idara, mashirika na serikali za mitaa

Amesema Serikali imetambua viwango vipya vya kimataifa vya ukaguzi wa ndani, na kuwa hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuzingatia viwango bora vya kimataifa.

“Viwango hivi havibadilishi mbinu tu, bali vinaashiria mwelekeo mpya wa namna wakaguzi wanavyofanya kazi na taasisi zinavyoshirikiana nao. Vinahitaji ushirikiano mkubwa zaidi, kujenga uaminifu na ubora wa kitaaluma,” amesema.

Naye rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania, Dk Zelia Njeza, amesema katika kuimarisha taaluma ya ukaguzi wa ndani, wako katika hatua ya mwisho ya kukamilisha maandalizi ya sheria ya wakaguzi wa ndani, na kuwa kuanzia Juni itaanza kupokea maoni ya wadau.

Pia amesema wako katika hatua ya mwisho ya kukamilisha muundo wa utumishi na muundo wa mishahara.

Mmoja wa wakaguzi, Christine Victoria Mbonya, amesema watatumia mwezi huu (Mei) kutoa elimu ya umuhimu wa wakaguzi wa ndani katika kuleta maendeleo ya taasisi na Taifa kwa ujumla.

“Wakaguzi wa ndani wanatoa tahadhari za mapema, na kama taasisi zitafunga hoja za ukaguzi wa ndani, hata akija CAG hawezi kukuta matatizo yoyote.

“Hivyo taasisi za umma zinapaswa kuwa na ushirikiano na wakaguzi wa ndani na kuwawezesha kwa vifaa ili watekeleze majukumu yao ipasavyo, na hivyo kuondoa hoja za ukaguzi kwa taasisi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *