Kushiriki Marekani kwa 70% katika jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel

Takwimu rasmi za makadirio zilizochapishwa zinaonyesha kuwa, Marekani imetoa zaidi ya dola bilioni 22 za silaha na misaada ya kijeshi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika kipindi cha mwaka mmoja tu uliopita.

Taasisi ya Masuala ya Umma na Kimataifa ya Watson, kwa kuzingatia makadirio ya Chuo Kikuu cha Brown, imeandika katika ripoti yake kuwa: Sehemu kubwa ya gharama za mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina yanayofanywa na Wazayuni hivi sasa zinatolewa na Marekani.

Marekani ikiwa ni mshirika wa kistratijia wa Israel, siku zote imekuwa muungaji mkono wake mkuu katika hali yoyote ile na imekuwa ikitoa misaada mingi zaidi ya kisiasa, kijeshi na kisilaha kwa utawala wa Kizayuni. Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa, kiwango cha misaada ya Marekani kwa utawala wa kibaguzi wa Israel katika kipindi chote cha uhai wa utawala huo bandia na vamizi ni zaidi ya dola bilioni 310 za Kimarekani.

Misaada hii ya Marekani imeongezeka mno hasa wakati wa vita na migogoro mbalimbali, kwani katika mwaka mmoja uliopita na tangu kuanza kwa vita vya Gaza, Washington imeisaidia Israel kwa kutuma silaha na misaada mbalimbali ya kijeshi.

Kimsingi ni kuwa, serikali ya Rais wa Marekani Joe Biden imechukua nafasi kubwa katika utoaji wa silaha kwa Israel tangu kuanza kwa vita vya Gaza. Ripoti mpya ya Taasisi ya Marekani ya “Watson” inaonesha kuwa, tangu kuanza vita vya utawala wa Kizayuni huko Gaza, Marekani imetoa msaada wa kijeshi wa zaidi ya dola bilioni 22 kwa utawala huo, ambao unajumuisha silaha na zana za kijeshi na meli za kubeba ndege za kivita. Katika muktadha huu, tunaweza kuashiria kutumwa Israel mabomu ya kuongozwa.

Marekani inaongoza kwa kuipatia misaada ya kijeshi Iisrael

Misaada ya Marekani kwa Israel inaendelea kutolewa huku jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wanaoishi Gaza zikiendelea kushuhudiwa, na sasa mauaji hayo yamegeuka na kuwa ya halaiki. Mwenendo huuu umeyafanya mashirika mengi ya kimataifa kuonya kuhusiana na hali hiyo na kutoa mwito wa kukomeshwa misaada ya Marekani kwa Israel.

Francesca Albanese ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa anasema kuhusiana na hilo: Mashambulio ya Israel dhidi ya Wapalestina wanaoishi Gaza yanatekelezwa kwa uungaji mkono wa nchi za Magharibi na silaha zao walizozitoa.

Msaada wa pande zote wa Marekani kwa Israel umefanya hata baadhi ya maafisa wa Marekani kutoa mwito wa kusitishwa msaada huu. “Bernie Sanders”, seneta wa kujitegemea wa Marekani sanjari na kubainisha kwamba, vyombo vingi vya habari vya Marekani vimejikita katika habari za uchaguzi wa rais wa nchi hiyo amesema: Haipasi kughafilika na kile kinachotokea hivi sasa hukko Gaza ambapo mzozo wa kibinadamu katika ukanda huo unazidi kuwa mbaya siku baada ya siku.

Sanders ameongeza kuwa: Katikati ya ugaidi huu ulioenea na ukiukwaji wa sheria za kimataifa, Marekani inaendelea kutuma mabilioni ya dola za msaada wa kifedha na maelfu ya mabomu na silaha nyinginezo kkatika fremu ya misaada ya kijeshi ili kuuunga mkono utawala wa Israel katika vita dhidi ya Gaza.  Suala la misaada kwa Israel hivi sasa limegeuka na kuwa changamoto kubwa katika jamii ya Marekani na kati ya vyama vya Democratic na Republican. Pamoja na hayo, vyama vyote hivyo viwili vinanasisitiza juu ya kuendelea kuunga mkono Israel katika fremu na kwa njia mbalimbali.

Maandamano ya kulalamikia sera za mauaji za Israel 

Hii ni katika hali ambayo, raia wengi wa Marekani pia wanalalamikia hali ya uchumi wa ndani wa nchi hiyo ambao umedorora na wanaona kwamba misaada hiyo ndiyo sababu ya kuzorota zaidi uchumi na kuongezeka matatizo ya kiuchumi ya nchi yao. Matokeo ya uchunguzi wa maoni yanaonyesha kuwa, theluthi mbili ya watu wa Marekani walioshiriki katika kura ya maoni ya CBS wanapinga misaada ya Washington kwa Israel.

Licha ya misaada yote ya Marekani na kuendelea jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wanaoishi Gaza lakini hakuna matarajio ya wazi yanayowasubiri Wazayuni. Eugene Kandel, mkuu wa zamani wa Baraza la Kitaifa la Uchumi la Israel alisema katika muktadha huu: Licha ya miongo minane ya misaada mikubwa ya Marekani kwa Israel, kuna uwezekano mkubwa kwamba Israel haitaweza kuwepo kama chombo huru cha Kiyahudi katika muongo mmoja ujao.

John Mearsheimer, Profesa wa Chuo Kikuu cha Harvard pia anaandika katika muktadha huu: Sera za ulinzi za Marekani kwa Israel sio tu kwamba zinahatarisha maslahi ya kitaifa ya Marekani, lakini pia zinachochea mivutano katika eneo la Asia Magharibi na hilo linaweza kusababisha kutengwa zaidi Washington ulimwenguni.