Kushindwa Wazayuni kukabiliana na oparesheni za kibunifu za Hizbullah ya Lebanon

Shambulio la ubunifu la Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon katika makao makuu ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, kwa mara nyingine tena limefichua kushindwa na udhaifu wa Wazayuni mkabala wa oparesheni za kijeshi za makundi ya muqawama.

Chumba cha oparesheni cha muqawama wa Kiislamu wa Lebanon leo Jumatatu kimetoa taarifa kikiutahadharisha utawala wa Kizayuni kwa kusema: “Tunamtahadharisha adui kwamba alichokishuhudia leo Jumatatu (shambulio dhidi ya brigedi ya Golani) ni sehemu ndogo tu ya mashambulizi ambayo anapasa kuyasubiri.” Hizbullah imesisitiza katika taarifa hiyo kuwa itashadidisha mashambulizi iwapo adui anataka kuendeleza hujuma zake dhidi ya watu wa Lebanon na Gaza. Chumba cha oparesheni cha muqawama wa Kiislamu wa Lebabon kimeongeza katika taarifa hiyo kuwa: “Oparesheni mpya na ya ubunifu ya makombora na ndege zisiso na rubani imetekelezwa katika maeneo ya Acre na Haifa ambapo droni zilizipita rada na kufika katika kambi ya mafunzo ya kikosi cha Golani huko Binyamina, kusini mwa mji wa Haifa. 

Shambulio la Hizbullah katika kambi ya Binyamina kusini mwa Haifa 

Makumi ya Wazayuni wamejeruhiwa na kuangamizwa katika oparesheni hiyo mpya ya Hizbullah katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimetoa ripoti nyingi vikithibitisha kufanikiwa oparesheni ya jana ya Hizbullah na kuripoti kuwa mlengwa mkuu aliyekusudiwa katika mashambulizi ya droni ya Hizbullah katika kambi ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni katika eneo la Binyamina huko Haifa alikuwa Herzi Halevi, mkuu wa majeshi ya utawala huo ghasibu. 

Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon Jumapili na Jumatatu wiki hii imetekeleza kwa mafanikio katika meneo mbalimbali oparesheni zake kubwa dhidi ya jeshi la utawala wa Kizayuni, na kuwasababisha Wazayuni kipigo kisichoweza kufidiwa huku viongozi wa utawala huo wakikiri wazi wazi kuwa na taathira mashambulizi hayo. 

Ripoti zilizotolewa hadi sasa zinaashiria kuongezeka idadi ya wanajeshi wa Kizayuni walioangamizwa na kujeruhiwa katika oparesheni hiyo. Wanamuqawama wa Kiislamu wa Iraq pia leo Jumatatu kwa mara nyingine tena wameshambulia kwa droni eneo nyeti huko huko Haifa kusini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Shambulio hili tajwa limetekelezwa saa chache baada ya kufanikiwa shambulio la Hizbullah ya Lebanon kwenye kambi ya kijeshi ya Wazayuni huko Haifa. 

Hizbullah yashambulia eneo nyeti la Wazayuni huko Haifa 

Duru mpya ya oparesheni za Hizbullah ya Lebanon imedhihirisha kuendelea kufanikiwa wanamuqawama hususan huko Lebanon katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni. Kwa oparesheni hii ya ubunifu, Hizbulllah kwa mara nyinginte tena imedhihirisha wazi uwezo wake wa kuathiri medani ya vita mkabala wa Wazayuni.

Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni uliweka mfumo wa ulinzi wa anga wa Kuba la Chuma au “Iron Dome” kwa kutumia kiasi kikubwa cha fedha na kwa kuungwa mkono na Marekani; na viongozi wa  Kizayuni siku zote wamekuwa wakidai kuwa mfumo huo wa ulinzi ni imara na usioweza kuathiriwa. Hata hivyo madai ya uwongo ya Tel Aviv kwamba mfumo wake wa Kuba la Chuma haupenyeki yamebainika wazi baada ya kujiri oparesheni ya Kimbunga cha al Aqsa na kushirikiana makundi ya muqawama na wanapambano wa Palestina dhidi ya utawala wa Kizayuni katika kutekeleza mashambulizi makubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).  

Makundi ya muqawama huko Yemen, Iraq na Lebanon mara kadhaa yalivuka mfumo ghali wa ulinzi wa anga wa utawala wa Kizayuni kwa kuvurumisha makombora na kutekeleza mashambulizi ya ndege zisizo na rubani jambo ambalo limeweka wazi udhaifu wa mfumo huo wa ulinzi. Oparesheni mpya ya ubunifu ya Hizbullah ya Lebanon imetekelezwa kwa umakini na kasi ya hali ya juu kwa namna ambayo mifumo ya rada ya utawala wa Kizayuni imegonga mwamba na kushindwa kuzuia mashambulizi hayo. 

Operesheni hii tajwa ya Hizbullah ya Lebanon imetekelezwa katika hali ambayo vyombo vya habari vyenye mfungamano na Marekani na utawala wa Kizayuni vimechapisha ripoti kadhaa kuhusu kutumwa mfumo wa ulinzi wa makombora wa THAAD kutoka Marekani hadi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel). Oparesheni mpya ya Hizbullah ni dhihirisho jingine la uwezo na nguvu ya makundi ya muqawama katika eneo ambapo kinyume na propaganda za vyombo vya habari vya Magharibi yana uwezo wa kuushinda kirahisi utawala wa Kizayuni kwa ubunifu wao kupitia oparesheni za kushtukiza.