Kurasini Heat kuongeza mashine mpya

BAADA ya kurudi Ligi ya Kikapu ya Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), mabosi wa Kurasini Heat, wamepanga kukisuka upya kikosi hicho kwa kuleta mashine za maana ili kurejesha makali katika ligi hiyo.

Kurasini iliwahi kubeba ubingwa wa BDL mwaka 2020, baada ya kuifunga JKT michezo 3-1, lakini ilishuka daraja msimu wa 2021 kutokana na kuondokewa na wachezaji nyota na msimu huu ilipambana Ligi Daraja la Kwanza Mkoa wa Dar es Salaam na kupanda daraja.

Mmoja wa viongozi wa timu hiyo, Mussa Kago alisema wamejipanga kuongeza wachezaji wenye uwezo mkubwa ili kurudisha heshima ya timu hiyo na uongozi unaendelea kutafuta wadhamini.

“Tunaomba wadau wa mchezo wa kikapu na kampuni kujitokeza kudhamini timu hii,” alisema Kago.

Mchezaji mkongwe wa timu hiyo, Domimic Zacharia alisema timu hiyo inaendelea vizuri na mazoezi kwenye Uwanja wa Bandari, Kurasini.

“Timu hii ina vijana wengi, inatakiwa wafanye mazoezi ya muda mrefu kwa ajili ya kujiweka fiti,” alisema Zacharia.

Alsema endapo wataongeza wachezaji wachache, ushindani katika ligi hiyo utakuwa mkubwa.

Kurasini ilipanda daraja pamoja na Polisi iliyoshika nafasi ya kwanza na Stein Warriors ikishika ya pili.