Kupaa kwa bei ya samaki kwamwibua mbunge, ajibiwa

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema mapendekezo ya kupunguza tozo na kodi za uingizaji wa samaki kutoka nje ya nchi yatafanywa kulingana na matokeo ya tathmini itakayofanywa na Kamati ya Maboresho ya Mfumo wa Kodi.

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande ameyasema hayo leo Jumatano Aprili 9, 2025 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Jacqueline Msongozi ambaye amehoji Serikali ina mpango gani wa kupunguza tozo na kodi za uingizaji wa samaki toka nje ya nchi.

Akijibu swali hilo,  Chande amesema Serikali kupitia Kamati ya Maboresho ya Mfumo wa Kodi (Task Force on Tax Reforms) katika vikao vyake, inaendelea kupokea mapendekezo yanayowasilishwa na wadau kuhusu maboresho ya mfumo wa kodi, ada na tozo mbalimbali ikiwa ni pamoja na eneo la uingizaji wa samaki kutoka nje ya nchi.

“Tathmini ya kina hufanyika ili kubaini hali ya soko, tabia za walaji, mahitaji, gharama, athari kwa mapato ya Serikali na kuzingatia umuhimu wa kulinda walaji na wafanyabiashara wa ndani ili kuongeza mchango wa thamani katika mnyororo wa uchumi,” amesema.

Hivyo, amesema uamuzi na mapendekezo ya kupunguza tozo na kodi za uingizaji wa samaki kutoka nje ya nchi, yatafanywa kulingana na matokeo ya tathmini husika.

Katika maswali ya nyongeza, Msongozi amesema samaki ni bidhaa muhimu hasa kutokana na kuwa na protini zinazohitajika kwa wajawazito, hivyo kwa nini  Serikali inachelewesha mchakato huo wa kuhakikisha samaki wanauzwa kwa wingi ikiwemo kuingizwa kutoka nje ya nchi.

Pia amesema bei za samaki imekuwa ghali na kukifanya kitoweo hicho kuwa anasa, hivyo kuihoji mkakati wa Serikali kuhakikisha inaondoa tozo kwa chakula cha samaki ili wapatikane  kwa wingi na bei nafuu.

Akijibu swali hilo, Chande amesema sio kwamba Serikali inachelewesha kufanya tahmini ya tozo mbalimbali na kuwa iko katika mchakato.

“Na pendekezo lake tumelichukua baadaye tutaleta hapa na Bunge lako tukufu kupitisha mapendekezo hayo kutoka kwa wadau mbalimbali,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *