Kundi la “Ramstein” laapa kuendelea kuisaidia Ukraine

Waziri wa ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov amesema mjini Brussels Jumatano kwamba serikali yake inategemea kuongeza uzalishaji kwa kushirikiana na washirika wake wa Ulaya wa silaha na risasi, ili kuimarisha usambazaji katikatika ya vita kati yao na Urusi.

Umerov aidha amesema ipo nia ya kuwa na makampuni ya silaha ya Ukraine yatakayotengeneza mifumo mipya nje ya nchi hiyo. Alitoa maoni hayo baada ya mkutano uliowakutanisha kundi wanachama washirika wa kuisaidia Ukraine, ambalo pia linajulikana kama Kundi la Ramstein, huko Brussels. Ameongeza kuwa silaha hizo zitatakiwa kupelekwa Ukraine wakati wa vita.

Umerov, aliyetoa ripoti ya mkutano huo sambamba na Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius na Waziri wa Ulinzi wa Uingereza John Healey, alisema, wananuia kutengeneza ndege zisizotumia rubani, makombora, risasi na silaha nyinginezo na kuongeza kuwa sasa wataangazia kubadilisha jinsi nchi za Ramstein zinavyojiandaa kwa vitisho vya siku za usoni.

Healey kwa upande mwingine alilaani mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Urusi kwenye miji na dhidi ya raia nchini Ukraine licha ya juhudi za amani zinazoendelea kati yao, Urusi na Marekani, na kwa pamoja mawaziri hao walitoa wito wa kusitisha mapigano na kuhimiza amani.

Ujerumani Ramstein | Boris Pistorius, Waziri wa Ulinzi
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius ameahidi taifa hilo litabeba jukumu la kuisaidia Ukraine sambamba na UlayaPicha: Heiko Becker/REUTERS

Marekani haikuhudhuria mkutano huo

Licha ya Marekani kutokushiriki mkutano huo, mawaziri hao wamesema wataendeleza juhudi zilizoanzishwa na kundi hilo na nia yao ni kusonga mbele na si kurudi nyuma. Awali mkutano kama huo ulifanyika bila ya waziri wa ulinzi wa Marekani Pete Hegseth na kundi hilo bado lilitoa ahadi ya kuisaidia zaidi Ukraine.

Mazungumzo hayo ambayo awali yaliongozwa na Marekani, sasa yanaongozwa na Pistorius na Healey, lengo kubwa likiwa ni kuratibu na kuongeza msaada zaidi wa kijeshi kwa Kiev.

Waziri wa Ulinzi wa Uholanzi Ruben Brekelmans alitangaza msaada mpya wa usalama wa baharini wenye thamani ya yuro milioni 400.

Amesema kifurushi hicho kitajumuisha zaidi ya meli 100, ndege zaidi ya 50 zisizotumia rubani, mifumo ya silaha, mafunzo na mengineyo.

Shinikizo linazidi kuwaelemea washirika wa Ukraine barani Ulaya la misaada kwa taifa hilo linalopigana vita na Urusi kwa miaka mitatu sasa, baada ya Washington kusitisha msaada wa kijeshi kwa Kiev na kuibua sintofahamu kuhusiana na mwelekeo wa taifa katika suala zima la ulinzi barani Ulaya. Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, yeye anasema bado ana imani kwamba usitishwaji huo haumaanishi Marekani ndio imeondoa kabisa usaidizi. Akaongeza kuwa kama hali ni tofauti, Ujerumani na Ulaya wako tayari kubeba jukumu hilo.

Marekani inahimiza kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Ukraine na wanataka yafikiwe haraka iwezekanavyo. Lakini nchi nyingine zina mashaka kwamba huenda makubaliano hayo yakawa ni mzigo kwa Ukraine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *