
Dar es Salaam, Wiki iliyopita mitandaoni vita ilikuwa ni moja kati ya Lady Jaydee na Zuchu nani mkali wa kuandika ngoma.
Kundi la waliokuwa wakisema Zuchu ni mkali waliwaponda wanaompa pointi Jide kwa kusema wanasumbuliwa na ile tabia ya watu wa kizazi kilichopita kudhani kizazi chao kilikuwa bora kuliko kilichofuata.
Kwa hiyo hawataki kumpa sikio Zuchu hata kidogo kwa sababu wanaamini ni wa kizazi hiki, hana jipya.
Wale waliokuwa wanampa pointi Komando Jide walikuwa wanasema Zuchu kwanza haandiki mwenyewe anaandikiwa, pili mistari yake ya kitoto mara aandike Dulla anataka chapati, mara nakula nauli yako na siji.
Kisha waligongelea msumari kwamba kumfaninisha Komando Jide na Zuchu ambaye hana hata albamu moja ni kumtukana Jide.
Mimi nasema, kumfananisha Jide na Zuchu ni kuwatukana wote wawili. Nitakuambia kwanini.
Watu wanaomchukulia poa Zuchu ni watu ambao ngoma pekee za Zuchu wanazozifahamu ni Honey, Chapati na Siji. Yaani ngoma flani hivi za kiwaki ambazo Zuchu huzifanya makusudi kwa ajili ya kuhudumia soko la Gen Z, vijana wa kisasa ambao wanapenda kelele na nyimbo zisizokuwa na maneno mengi.
Lakini hakuna anayeongelea ngoma ya kwanza ya Zuchu ya kuitwa Wana. Hakuna anayeongelea Hakuna Kulala, Raha, Utaniua, Sukari na zaidi. Ngoma ambazo zimekuwa ni uthibitisho mkubwa Zuchu ni mmoja wa wasanii wanaojua kuandika kwelikweli, labda tuambiwe hajaandika mwenywe, ameandikiwa.
Kwenye ngoma hizo Zuchu anatumia Kiswahili fasaha miksa nahau, methali, misemo na kadhalika. Niambie unapata wapi nguvu ya kuwa na shaka na uandishi wa msanii anayeandika mistari kama hii “Namvuta faraghani, tumo tupu tupu ndani, namtazama simwishi, namkanda mambavuni, kayainua majeshi, vita nichague mimi, aanze Bangladesh amalizie Sudan.”
Na kwa upande wa Jide haina ubishi kwamba ni mmoja wa waandishi wazuri kuwahi kutokea Tanzania. Lakini uandishi wake una utofauti kubwa sana na Zuchu.
Komando hatumii maneno magumu ya Kiswahili, wala vimethali na nahau. Nguvu ya Jide ipo kwenye maana ya ndani ya mada anayoimba. Mistari kama hii; “Tega sikio kwa makini nikueleze, hakuna penzi tamu kama la milele, muda unaenda mwenzenu ninagundua, moyoni mwangu katu halitapungua, nimeumizwa mara nyingi nakumbuka, kuna hatua ilifika mi’ nikajuta, lakini sasa nina imani yuko wa kumpa.
Ninachohitaji ni muda aweze tokea, siwezi sema kuwa sitopenda tena, kwani nitakuwa naidhulumu yangu nafsi, moyoni najua ninalo penzi la milele, halitakwisha nakwambia labda wa kumpa asizaliwe.”
Ukisikiliza mistari kama hiyo utagundua imeandikwa kwa kutumia maneno ya kawaida ya kila siku. Hakuna ujanja wa ziada unaoonekana kwenye uandishi wa Jide ukiachana na vina na mizani, lakini nguvu kubwa iko kwenye mada anayoiimba na jinsi anavyoiwasilisha kupitia uimbaji wake.
Hii ni sawa na kusema, Zuchu na Jide ni wasanii wa aina mbili tofauti linapokuja suala la uandishi. Kwa hiyo kuwashindanisha ni sawa na kushindanisha ugali na wali kipi chakula kizuri. Kuna watu watasema ugali kwa sababu wanapenda ugali, kuna watu watasema wali kwa sababu wanapenda wali.
Pia, hakuna ubaya tukisema wote ni wazuri kwenye uandishi. Ili mtu mmoja kuwa mzuri sio lazima mwingine awe mbaya. Tuache kutukana sanaa za hawa malkia wetu.