Kumekucha Ramadhani Cup

MASTAA wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), wanatarajia kuunda timu zao zitakazoshiriki katika mashindano ya Kombe la Ligi ya Ramadhani, yatakayoenda kwa jina la Ramadhani Star Ligi na kufanyika kwenye Uwanja wa Spide.

Akiongea na Mwanasposti kwenye Uwanja wa Spide, mratibu wa mashindano hayo, Mohamed Yusuph, alisema mashindano hayo yatakayokuwa yakifanyika mara mbili kwa wiki, yataanza Machi 14.

“Tumepanga michezo itakayofanyika, ianze baada ya wachezaji wote kufuturu uwanjani hapo,” alisema Yusuph.

Kwa mujibu wa Yusuph, mastaa watakaokuwapo wataunda timu kwa kushirikiana na yeye mwenyewe.

“Shindano hili la kikapu la Ramadhani Star Ligi, ni la kwanza kufanyika katika mkoa wa Dar es Salaam na litakuwa likifanyika kila mwaka,” alisema Yusuph.

Yusuph ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya Mchenga Star, alisema kwa upande mwingine mashindano hayo yatakuwa ni moja ya maandalizi mazuri ya wachezaji katika Ligi ya BDL.

Aliwataja baadhi ya mastaa wanaotarajia kuwapo siku ya ufunguzi kuwa ni Baraka Sadiki, Mwalimu Heri, Amin Mkosa, Tyrone Edrward, Omary Sadiki na Jonas Mushi.