Kibaha.Wakati uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa ukitarajia kufanyika leo Aprili 2,2025 mjini Kibaha Mkoa wa Pwani, shamrashamra za tukio hilo zimepamba moto na kusimamisha baadhi ya shughuli mjini hapa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo anatarajia kuwa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.
Hafla za tukio hilo zinaendelea kwenye uwanja wa shirika la Elimu Kibaha.
Wakati shamrashamra zikiendelea, hali ni ya utulivu mjini hapa huku askari wa kutuliza ghasia na wale wa usalama barabarani wakiwa wametanda katika maeneo tofauti ambako misafara ya viongozi inapita.
Katika kutoa fursa ya wananchi kushiriki kikamilifu, shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Kibaha Mji zimefungwa kwa siku moja ya leo ili kupisha tukio hilo.

Mwananchi imepiga kambi eneo la tukio ambako shamrashamra zimeanza ikiwamo halaiki na burudani mbambali huku viongozi wa kitaifa wakianza kuwasili kwenye viwanja vya Shirika la Elimu inakofanyika hafla hiyo.
Baada ya kuwashwa, Mwenge huo utakimbizwa kwenye Halmshauri tisa za Mkoa wa Pwani kabla ya kukabidhiwa Mkoa wa Morogoro.

Matamanio ya wananchi mjini Kibaha ni kufahamu miradi gani ya maendeleo ambayo inawagusa moja kwa moja itakayozinduliwa katika tukio hilo. Miradi hiyo inatarajiwa kutajwa wakati ikisomwa taarifa ya tukio hilo.
Taarifa zaidi endelea kufuatilia Mwananchi