Kumekucha Hanang, mbunge aonya: Msisingizie mmetumwa na wazee, tukutane uwanjani

Hanang. Mbunge wa Hanang mkoani Manyara, Samwel Hhayuma amesema wanasiasa wanaojipitisha kutaka kugombea nafasi hiyo wasisingizie kutumwa na wazee ila waingie uwanjani muda ukiwadia.

Hhayuma ameyasema hayo kwenye kijiji cha Bassotughang kata ya Hidet, leo Machi 26, 2025 wakati akizungumza na wakazi wa eneo hilo.

Amesema baadhi ya wanasiasa wanapotosha watu wakidai kuwa wazee wamewaomba wagombee nafasi ya ubunge kwenye uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.

“Anasema amefuatwa na wazee, hapa Hanang’ tuna wazee wengi hao wa kwako umewatoa wapi, asilimia ngapi ya wazee wanakuomba, kama unahitaji jambo lako tangaza mwenyewe,” amesema Hhayuma.

Amesema kelele za wanasiasa walioongoza kwenye kura za maoni mwaka 2020 kisha wakashindwa kupitishwa kugombea zisiwatishe kwani hazina maana.

“Hao walioshinda kwa kulambisha watu asali, kwa kugawa fedha, kuwapeleka kwa viongozi wa dini na kufuta majina, unapaswa kusema ulikuwa mwizi na siyo kudai kuwa ulishinda,” amesema Hhayuma.

Ameeleza kuwa mwanasiasa anayesema anagombea ubunge mwaka 2025 ili aage jamii ni mlaghai kwani alishaacha ofisi na kuagana kwa makabidhiano rasmi.

“Huyu anataka tuagane nini tena ili hali hata umri wake unajulikana, kama kuagana tuliagana mwaka 2020 uchaguzi ulipomalizika anataka tuagane upya, wape salamu zao,” amesema Hhayuma.

Mkazi wa eneo hilo, John Saktai amesema wanasiasa wanaotaka kugombea jimbo hilo wanapaswa kujipanga kwani Hhayuma amefanya kazi kubwa kwa miaka mitano aliyoshika nafasi hiyo

“Mbunge Hhayuma amefanya kazi kubwa kwa miaka mitano kwenye sekta ya maji, afya, elimu na miundombinu, hivyo anayetaka hiyo nafasi ajipange kweli kweli,” amesema Saktai

Mkazi mwingine Emmanuel Nade amesema miaka mitano ya uongozi wa Hhayuma imekuwa kama miaka 20 ya uongozi kutokana na maendeleo yaliyofanyika.

“Pamoja na kuwa huwezi kujenga Hanang kwa siku moja ila miaka mitano ya Hhayuma kazi kubwa mno imefanyika na watu wameiona,” amesema Nade.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *