Kumbukizi ya Profesa Kairuki: Urithi wa maono ya maendeleo katika sekta ya afya na elimu Tanzania

Miaka 26 imepita tangu Profesa Hubert Clemence Kairuki, muasisi wa Kairuki Hospital, alipotutoka. Hata hivyo, urithi wake uliojikita katika uimarishaji sekta ya afya, elimu, na viwanda nchini bado unaishi na utadumu kwa vizazi vingi vijavyo.

Tunasherehekea mafanikio aliyoyapata na maono aliyoyaacha nyuma, ambayo sasa ni msaada kwa kila Mtanzania anayetamani kuwa na afya njema.

Hospitali ya Kairuki, iliyoanzishwa mwaka 1987, ilikuwa ni hatua ya kwanza katika kuanzisha hospitali binafsi. Profesa Kairuki aliona namna hospitali za umma zilivyokuwa zikielemewa na wagonjwa, hali hiyo ilimpa shauku ya kuanzisha hospitali itakayotoa huduma bora za matibabu na kuweza kuwafikia Watanzania wa kila rika na hali ya kiuchumi.

Uongozi wake wa kipekee na namna yake ya kusimamia shughuli za hospitali, iliifanya hospitali hiyo kuwa moja ya vituo bora vya afya nchini, ikitoa huduma za afya zinazozingatia ubora, uharaka, na kufuata miongozo ya wizara ya afya.

Pamoja na mafanikio haya, Profesa Kairuki alijua kwamba sekta ya afya bado inahitaji pia wataalamu wa afya waliobobea wa kutosha ili kuwa na huduma bora na endelevu.

Hii ndiyo sababu iliyomfanya aanzishe Chuo Kikuu cha Kairuki (KU) mwaka 1997 ambapo kiliitwa Mikocheni International University na baada ya kifo chake jina hilo lilibadilishwa na kuwa Hubert Kairuki Memorial University (HKMU) ikiwa ni ishara ya kumuenzi.

Mwaka 2024 jina hili pia lilibadilishwa na kuwa Kairuki University ili kuendana na majina ya taasisi zingine zilizopo chini ya taasisi mama ya KHEN. Chuo kikuu cha mafunzo ya utabibu na afya, ambacho kimeendelea kutoa elimu bora ya kiwango cha kitaifa na kimataifa kwa wanafunzi wanaotaka kuwa madaktari, wauguzi, na wataalamu wa afya kwa ujumla.

Profesa alijua kuwa hatua ya kuanzisha chuo hiki ilikuwa muhimu kwa kuendeleza sekta ya afya nchini na kuandaa wataalamu wa afya wa baadaye. Aliwekeza katika kutoa elimu ya kisasa, inayozingatia ufanisi na matumizi ya teknolojia mpya katika matibabu kama ilivyo sasa hospitali imeanza kutoa huduma ya kuondoa uvimbe mwilini bila ya upasuaji inayojulikana kama HIFU (High-Intensity Focused Ultrasound), technolojia hii ni bora na ya kisasa.

Aidha, kwa kuwa uuguzi ni sehemu muhimu sana katika utoaji wa huduma za afya, Profesa Kairuki alianzisha Shule ya Uuguzi, inayolenga kutoa mafunzo ya kiwango cha juu kwa wauguzi. Leo hii, shule hii imeendelea kutoa wataalamu wa uuguzi wanaoongoza katika maeneo mbalimbali ya huduma za afya ndani na nje ya nchi.

Mafanikio ya Profesa Kairuki hayakuishia tu kwenye hospitali na elimu. Aliwaza kuwa sekta ya afya inahitaji pia kuwa na huduma za kisasa za uzazi, ambazo zingeweza kusaidia familia nyingi zinazokutana na changamoto za kupata watoto.

Hivyo, Muanzilishi mwenza Mama Kokushubira Kairuki, kwa kushirikiana na Bodi ya Wakurugenzi, walianzisha Kituo cha Uzazi Pandikizi, kitengo kinachotoa huduma za kisasa na msaada mkubwa kwa wanandoa wengi walioshindwa kupata ujauzito kwa njia ya kawaida.

Kitengo hiki kimeleta mapinduzi katika huduma za uzazi nchini, na kimekuwa chombo muhimu na cha mfano katika kutoa tiba za kisasa za uzazi, kikiwasaidia watu wengi kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi. Zaidi ya hayo, Profesa aliona umuhimu wa viwanda vya dawa ili kuhakikisha sio tu dawa bora zinapatikana, lakini kila Mtanzania amudu kuzipata.

Kiwanda cha uzalishaji dawa cha Kairuki (Kairuki Pharmecuticals Industry Limited – KPIL) kilianzishwa mwaka 2022 huko Kibaha, mkoa wa Pwani. Kiwanda hiki kimeleta mabadiliko makubwa katika tasnia ya dawa, kikiimarisha uzalishaji wa dawa za ndani na kupunguza utegemezi wa madawa kutoka nje ya nchi.Hakupendelea tu kufanya kazi ya kiutawala, bali pia alipenda kushirikisha na kutia moyo watu wa karibu yake, akijua kuwa maendeleo hayawezi kuletwa na mtu mmoja tu, bali ni lazima iwe ni jitihada za pamoja za jamii nzima.