
Dar es Salaam. Inspector Haroun ni miongoni mwa wasanii wa mwanzo kabisa Bongo kufanya vizuri upande wa Hip Hip, alifunika na kundi la Gangwe Mobb liloanza mwaka 1993/94 akiwa na mwenzake, Luteni Kalama baada ya kuvutiwa zaidi na LWP Majitu.
Inspector Haroun ametoa albamu na kutengeneza nyimbo kubwa ambazo zipo kwenye orodha ya nyimbo bora za Bongofleva kwa muda wote.
Mwanzo alikuwa anatumia jina la Shakur (2Pac) ila DJ Boniluv akampa jina la Inspector Haroun, pia DJ Boniluv ndiye aliyewapa jina la kundi la Gangwe Mobb kutokana na ustahimilivu wao katika muziki, na hata jina la Luteni Kalama kalitoa yeye.
Baada ya kushiriki mashindano ya Rap na kuibuka washindi viwanja vya Don Bosco, Upanga ndipo DJ Boniluv waliwaona Gangwe Mobb na kuwapa nafasi ya kurekodi. Hata hivyo, tayari walikuwa wameshaenda sana studio kwake kwa miguu bila mafanikio, walipomueleza hilo ilibidi awanunulie chips yai ili kuwapoza.
Wimbo uliowatoa Gangwe Mobb unaoitwa ‘Ngangari’ uliotoka mwaka 1999, ulitengenezwa na Maprodyuza watatu DJ Boniluv, Rajab Marijani na P Funk Majani, ila wimbo wao wa kwanza kuachia ni ‘Mauzauza’ uliorekodiwa Mawingu Studio.
Sebastian Maganga ndiye alitoa wazo kwa Gangwe Mobb kutengeneza wimbo wao maarufu ‘Vidonge Vyao’ chini ya Master J, ngoma hii ilichochea sana mauzo ya albamu yao ya kwanza, Simulizi la Ufasaha.
Vidonge Vyao, wakimshirikisha Nasma Hamisi ndio wimbo wa kwanza wa Bongofleva kuchanganya Hip Hop na Taarab.
Licha ya wimbo wake, Mtoto wa Geti Kali, kufanya vizuri na kumpatia fedha zaidi sio moja ya nyimbo zake anazozikubali sana, Inspector Haroun wimbo wake anaukubali zaidi ni Bye Bye.
Gangwe Mobb waliamua mwenyewe kujiita ‘Rap Katuni’ kutokana na ina ya muziki wao, mchora katuni maarufu Tanzania, Masoud Kipanya ndiye aliyechora ‘artwork’ ya wimbo wao, Vidonge Vyao.
Inspector Haroun aliandika wimbo wake ‘Mtoto wa Geti Kali’ kwa siku moja tu, wazo la kufanya wimbo huo lilikuja baada ya kupendwa na mrembo mmoja alipokuwa akikatiza City Garden akielekea studio kwa DJ Boniluv.
Muziki umempatia mke Inspector Haroun, alichoimba kwenye wimbo wake ‘Asali wa Moyo’ ni kisa cha kweli na mwanamke huyo ndiye mke wake hadi sasa ikiwa ni takribani miaka 20 tangu wafunge ndoa na tayari wana watoto watatu.
Bifu la Inspector Haroun na Juma Nature lilianza kutokana na kushindanishwa na mashabiki wakiamini kuna mmoja wapo anamuiga mwenzake, ila baada ya kufanya pamoja wimbo ‘Mzee wa Busara Remix’ ukawa mwisho wa bifu hilo maana utofauti ulionekana.
Sauti ya mwanamke inayosikika kwenye wimbo wa Inspector Haroun ‘Mtoto wa Geti Kali’ ni ya Queen Darleen, aliyewakutanisha ni Dully Sykes pande za Ghorofani Kariakoo, Inspector alikuwa na mazoea ya kwenda huko ili kukutana na kwa DJ G Lover (Guru) wa G Records.
Kipindi hicho Queen Darleen alikuwa bado binti mdogo ambaye alipenda muziki, hivyo wakaenda kuomba ruhusu kwa Mama yake ili aweze kushiriki katika wimbo huo.