Kumbe Dully Sykes aliazima ile suti kwa Kusaga!

Dar es Salaam. Kwa miaka zaidi ya 25, Dully Sykes amekuwepo katika muziki akifanya vizuri kwa nyimbo zake maarufu huku akitoa albamu tatu ambazo ni Historia ya Kweli (2002), Handsome (2004) na Hunifahamu (2005) zilizomtangaza vizuri.

Ukiachana na kuimba, Dully Sykes ana mchango mkubwa wa kuikuza Bongofleva kwa kuwasaidia wasanii wengi ambao sasa baadhi yao wana majina makubwa huku akianzisha studio ambayo alitoa mikwaju ya maana kabisa. Fahamu zaidi.

 Kwa mujibu wa Dully Sykes, yeye ndiye mwanzilishi wa Bongofleva kwa kuja na mtindo wa kuimba kupitia wimbo  wake ‘Julieta’ baada ya wasanii wengi hapo awali kufanya rap, huku akimtaja Alikiba kutokea Kings Music kama mfalme wa Bongofleva.

Anamtaja Alikiba kama mfalme wa Bongofleva kwa sababu ndiye msanii wa kwanza ambaye alikuwa bado hajatoka kimuziki, lakini akamuomba amshirikishe katika wimbo wakati tayari yeye alikuwa msanii mkubwa, kipaji cha Kiba ndicho kilichomvutia.

Kipindi Lady Jaydee anafanya kazi Clouds FM, ndiye alikuwa mtangazaji wa kwanza kuucheza wimbo wa Dully Sykes ‘Julieta’ redioni, ni wimbo uliobadilisha maisha ya Dully ni ndio unatajwa kama wa kwanza wa Bongofleva. 

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Uzalishaji na Vipindi, Clouds Media Group, hayati Ruge Mutahaba alipousikia tu wimbo wa ‘Julieta’ alivutiwa nao na kumpa Dully Sykes fedha kiasi cha Sh10,000 akanunue viatu maana hakuwa navyo wakati huo.

Wimbo wa Dully Sykes ‘Ulidhani Siri’ akimshirikisha Mike Tee kutoka katika albamu yake ya pili, Handsome (2004), aliutunga kwa ajili ya aliyekuwa mpenzi wake, Alice ambaye alimuacha na kwenda kwa Mr. Nice aliyekuwa maarufu wakati huo.

Hata hivyo, hapo awali wawili hao walikuwa ni marafiki kwani Mr. Nice ndiye mtu wa kwanza kumpeleka Dully Sykes Zanzibar, hiyo ilikuwa mwaka 2002 katika shoo.

 Msanii Bora wa Hip Hop duniani kwa Dully Sykes, ni rapa wa Marekani, Eminem ambaye ni mshindi wa tuzo 15 za Grammy. Kwa mujibu wa Dully, yeye anapenda sana Hip Hop ili aliimba kutokana ana kipaji hicho na anafuata biashara ilipo.

 Rapa Witness, mshindi wa Coca-Cola Popstar 2004, ni miongoni mwa waliokuwa wanampa nafasi Dully Sykes kuingia katika shoo, Dully alikuwa anatoka kwao na kwenda Bilicanas na kumuomba Witness amtafutie nafasi ya kutumbuiza.

Hata katika wimbo wa Witness, Zero (2008) aliomshirikisha Fid Q na kushinda tuzo ya Channel O, amezunguzia ukaribu wake na Dully kwa miaka hiyo.

Sasa wimbo maarufu wa Dully Sykes ‘Ladies Free’ aliutunga kwa ajili ya Club Bilicanas ambayo kila Alhamisi wanawake walikuwa wanaingia bure, ingawa katika wimbo huo kaitaja siku ya Ijumaa (Friday) ili kupata vina tu.

Jina la Misifa, Dully Sykes alipewa na mama yake maana alipokuwa mdogo alikuwa kiherehere sana, mathalani anaweza kununuliwa nguo za sikukuu ila akazivaa kabla ya hata ya sikukuu yenyewe na kwenda kuwaringia wenzake.

Hata hivyo, waliokuja kulileta jina hilo katika muziki ni Zig Zag Crew baada ya kwenda nyumbani kwa kina Dully na kumsikia mama yake akimuita Misifa, ndipo nao wakaanza kumuita hivyo, basi Dully akaona isiwe tabu bora ajiite tu Mr Misifa.

Suti aliyovaa Dully Sykes katika cover ya albamu yake ya pili, Handsome (2004), aliazima kwa Mkurugenzi wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga, hivyo baada ya kumaliza kupiga picha akarudisha suti ya Kusaga.

Kusaga aliamini sana katika kipaji cha Dully. Aliamini albamu hiyo itafanya vizuri sokoni pindi itakapotoka, basi akamuazima suti yake na kweli albamu hiyo aliyoizindua akiwa na TID ikawa na mafanikio zaidi ya ile ya mwanzo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *