Kula vyakula hivi kukabiliana na maumivu ya hedhi

Dar es Salaam. Wakati wa hedhi kuna baadhi ya wanawake hupitia changamoto ya kupata maumivu makali hali inayosababisha kushindwa kufanya shughuli zao mbalimbali.

Kwa mujibu wa wataalamu, maumivu hayo hutokana na kitendo cha misuli ya uterasi kukaza na ambacho huratibiwa na homoni ya ‘prostaglandins’.

Waathirika wa maumivu hayo hutumia njia mbalimbali wanazoamini zitawasaidia kupunguza maumivu hayo ikiwemo matumizi ya dawa za maumivu ya tumbo.

Hata hivyo, wataalamu mbalimbali wa afya na lishe wanashauri kabla ya kufikia kutumia dawa za maumivu, mhusika anaweza kutumia vitu mbalimbali ikiwemo vyakula ili kupunguza maumivu hayo.

Lakini pia wanashauri katika kipindi hicho, mwanamke anashauriwa kuacha kutumia baadhi ya vyakula ikiwemo vile vyenye mafuta kwa wingi.

Akizungumza na Mwananchi, Daktari wa binadamu kutoka Hospitali ya Anglikana, Rachel Mwinuka amesema mwanamke anapoingia katika hedhi hupata mabadiliko ya homoni ambayo husababisha wengine kutapika, kuharisha, kutoka chunusi, kuharibika ngozi na hata kupata maumivu ya tumbo na kiuno.

Amesema kwa wale wanaopata maumivu ya tumbo katika kipindi hicho, wanashauriwa kutopendelea kutumia vyakula au vitu vyenye sukari au chumvi kwa wingi pamoja na kujiepusha na vinywaji vyenye wingi wa kiambata cha caffein katika kipindi hicho.

“Unaweza  pia ukakabiliana na tatizo la maumivu ya hedhi kwa  kula matunda na mboga za majani kwa wingi, kupunguza au kuacha kabisa kula vyakula vya mafuta, unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara,”amesema.

Pia amesema inashauriwa kula vyakula vyenye nyuzinyuzi (fiber) ambavyo husaidia katika kupunguza maumivu hayo.

Ameongeza kuwa baadhi ya huduma za kuchua mwili kama vile kuchua tumbo pamoja na ufanyaji wa mazoezi mepesi, kunasaidia kupunguza maumivu hayo.

Mtaalamu wa lishe kutoka shirika la Word Vision Tanzania, Dk Daudi Gambo amesema kuwa katika kipindi hicho, inashauriwa pia kwa anayepata maumivu ya tumbo katika kipindi cha hedhi,  kupendelea kunywa tangawizi pamoja na kutumia vitu vyenye asili ya viungo kama vile vitunguu swaumu.

Vilevile katika tovuti ya medicinenewstoday inaelezwa kuwa ulaji wa samaki na vyakula vya baharini, husaidia kupunguza maumivu hayo kwa kuwa vina wingi wa virutubisho vya Omega- 3 fatty acid ambayo inasaidia kupunguza maumivu hayo.

Kwa mujibu wa tovuti hiyo vyakula vingine vyenye kirutubisho hicho ni mbegu za chia, maziwa pamoja na mtindi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *