
Mwanadiplomasia wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amelalamikia kimya cha wanaharakati wa haki za binadamu kuhusu wananchi wa Palestina.
Muhammad Safa Mwanadiplomasia wa Palestina katika Umoja wa Mataifa ameandika katika mtandao wa kijamii wa X Twitter ya zamani kuwa: Gaza imemfunza kuwa aghalabu ya watu ambao wanadai kuwa ni watetezi wa haki za binadamu wanachukua hatua chanya na wanakuwa wanaharakati pale walengwa wanapokuwa watu kutoka taifa au kabila fulani.
Muhammad Safa ameongeza kuwa: Kinachotokea Ukanda wa Gaza si vita bali ni mauaji ya kimbari.
Utawala wa Kizayuni tokea Oktoba 7 mwaka jana unatekeleza mauaji makubwa ya kinyama dhidi ya Ukanda wa Gaza na katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya raia wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina. Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa watu zaidi ya elfu 41 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya elfu 95 kujeruhiwa tangu kuanza vita na mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Gaza.