Hatimaye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) baada ya miezi kadhaa ya utafiti na uchunguzi imetoa hukumu ya kukamatwa Benjamin Netanyahu na Yoav Gallant, Waziri Mkuu na Waziri wa Vita wa zamani wa utawala katili wa Israel kwa kutenda jinai za kivita huko Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, watenda jinai wawili hao wa Kizayuni wanasakwa katika nchi 120 wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC). Kutolewa hukumu hii tajwa kumekabiliwa na radiamali na hisia mbalimbali duniani kote.

Marekani na Ulaya pande mbili washirika wa kistratejia wa utawala bandia wa Israel zimedhihirisha radiamali tofauti kabisa mkabala wa hati ya kukamatwa iliyotolewa dhidi ya Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa kizayuni na Waziri wa Vita wa zamani wa utawala huo Yoav Galant.
Rais Joe Biden wa Marekani ametoa taarifa na kuitaja hatua iliyochukuliwa na mahakama ya ICC yenye makao yake mjini Hague Uholanzi kuwa ya “kidhalimu.” Biden amesema: “Siku zote tuko pamoja na Israel dhidi ya vitisho vya usalama wake. Marekani katika kipindi cha siku tatu tu imedhihirisha radiamali mbili muhimu za kuuhami na kuukingia kifua utawala wa Kizayuni unaotekeleza mauaji ya watoto huko Gaza. Hatua ya kwanza iliyochukuliwa na Marekani ni kura yake ya turufu dhidi ya azimio la karibuni lililopendekezwa kwa ajili ya kustisha vita Ukanda wa Gaza ili kuzuia kuendelea mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina. Hii ni katika hali ambayo nchi kumi na nne kati ya kumi na tano wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zilipiga kura ya kuunga mkono rasimu ya azimio hilo. Ni Marekani pekee ambayo ilipiga kura kupinga rasimu ya azimio hilo kwa ajili ya kusitisha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Marekani si mwanachama wa mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kutokana na kuogopa kwake kufunguliwa mashtaka wanajeshi wake watenda jinai na vile vile viongozi wa utawala wa Kizayuni katika mahakama hiyo. Marekani hata imesaini makubaliano ya pande mbili na baadhi ya nchi ambayo yanawapa kinga wanajeshi wa Marekani ya kutofuatiliwa na kushtakiwa na taasisi za kimataifa. Aidha licha ya ushawishi ilionao katika taasisi za kimataifa, lakini Marekani inakabiliwa pia na vikwazo katika baadhi ya taasisi duniani.
Lau Marekani ingekuwa na haki ya kupiga kura ya turufu katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, basi ingepinga hukumu ya mahakama hiyo dhidi ya viongozi wa utawala wa Kizayuni watenda jinai na wauaji watoto huko Gaza. Serikali ya Marekani ni mshirika mkubwa wa jinai za Wazayuni katika mauaji ya halaiki na kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza. Wazayuni wasingekuwa, bali hawana uwezo peke yao wa kukabiliana na muqawana na istiqama ya Wapalestina huko Gaza bila ya kuungwa mkono kwa pande zote na Marekani. Mauaji ya kimbari na halaiki dhidi ya Wapalestina ni matokeo ya udhaifu na kiburi cha Wazayuni ambacho kinawapelekea watekeleze jinai za kutisha huko Ukanda wa Gaza.

Matamshi na radiamali za serikali za Ulaya mkabala wa waranti wa ICC ni tofauti na radiamal iliyodhihirishwa na Marekani. Josep Borrel Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema kuhusu waranti uliotolewa na Mahakama ya ICC kwa ajili ya kukamatwa Netanyahu na Galant kuwa “uamuzi huu ni wa lazima kutekelezwa, na nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya zitautekeleza.” Wakati huo huo Msemaji wa serikali ya Uingereza ameielezea hati hii ya ICC kwamba: “Tunaheshimu uhuru wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.” Taasisi hii ina jukumu kuu la kuchunguza na kufuatilia uhalifu mkubwa zaidi kimataifa. Hata hivyo, serikali za Ulaya zimeongeza maneno ya ziada kwenye hukumu hii tajwa ili kutodhoofisha wajibu wao wa kuunga mkono utawala bandia wa Israel, kwa kudai kuwa una haki ya kujilinda.
Radiamali ya nchi za Ulaya mkabala wa waranti wa ICC dhidi ya vongozi watenda jinai wa Kizayuni imeathiriwa na mashinikizo ya fikra za waliowengi katika nchi za Magharibi. Suala la muqawama na kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina na kushuhudiwa kuongezeka chuki dhidi ya Wazayuni watenda jinai limegonga vichwa vya habari na kuakisiwa pakubwa duniani kote. Nchi za Magharibi haziwezi tena kukandamiza uungaji mkono mkubwa wa watu katika nchi mbalimbali duniani kwa watu wanaodhulumiwa wa Palestina kwa kisingizio cha chuki dhidi ya Uyahudi. Ni wazi kuwa serikali za Ulaya zimethibitisha kuwa mauaji ya kimbari yamejiri katika Ukanda wa Gaza kwa hatua yao ya kuunga mkono hukumu ya ICC. ICC imetoa hukumu hii katika hali ambayo Marekani na Ulaya hazijapunguza kivyovyote vile uungaji mkono wao kwa utawala wa Kizayuni na zimepinga utaratibu wote wa kimataifa wa kuzuia kuendelea mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina. Ndio maana Bi Agnès Callamard, Katibu Mkuu wa Shirika la Amnesty International akautaja uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuwa hatua muhimu ya kihistoria.
