Matukio ya hivi karibuni katika vita vya Ukraine, yaani uamuzi wa nchi za Magharibi wa kutoa ruhusa kwa Ukraine kuishambulia Russia kwa kutumia silaha za masafa marefu za Marekani na Ulaya kwa upande mmoja, na Russia kutumia w kombora jipya la masafa ya kati lenye kasi ya zaidi ya sauti dhidi ya Ukraine kama tahadhari kali kwa Magharibi, kumeibua mgogoro mkubwa na usio na kifani kati ya Russia na NATO.
Suala hili limekosolewa hata katika nchi za Ulaya ambazo ni wanachama wa NATO.
Waziri Mkuu wa Slovakia, Robert Fico, amekosoa uamuzi wa Rais wa Marekani Joe Biden wa kutoa kibali kwa Ukraine kulenga ardhi ya Russia kwa makombora ya masafa marefu ya Marekani, na kuutaja kuwa ni uamuzi wa kushangaza ambao utazidisha mvutano wa kimataifa. Robert Fico amesisitiza kwamba, hata Marekani haitakuwa salama kutokana na taathira za suala hilo.

Afisa huyo mkuu wa Ulaya amekosoa hatua za makusudi zilizochukuliwa na Rais wa Marekani, Joe Biden za kuitumbukiza Marekani kadri inavyowezekana katika vita vya Ukraine ambazo hatimaye zitamfanya Donald Trump rais mteule wa nchi hiyo ambaye atachukua kiti cha urais mnamo Januari 20, 2025, akumbane ana ana na mgogoro huo. Mikhail Malov, mchambuzi mkuu wa zamani wa sera za usalama za Wizara ya Ulinzi ya Marekani, anasema: Utumiaji wa Ukraine wa makombora ya masafa marefu ya ATACMS hautabadili mkondo wa vita, kinyume chake utazidisha mgogoro. Ameongeza kuwa: Hatua hizi mbaya za Biden zina sababu za kisiasa; na serikali mpya ya Donald Trump, rais mteule wa Merekani, itafeli katika siku zijazo, kwa sababu ikiwa hataunga mkono uamuzi huu wakati wa urais wake, nafasi ya serikali yake itakuwa dhaifu.
Pamoja na hayo, Ulaya, ambayo ina wasiwasi kuhusu mabadiliko ya sera ya sasa ya Marekani kuhusu vita vya Ukraine na kupunguzwa kwa kasi kwa misaada ya nchi hiyo kwa Ukraine, imekaribisha uamuzi wa Biden. Vilevile baada ya Washington kutoa ruhusa kwa Ukraine kushambulia ardhi ya Russia kwa kombora la ATACMS linaloweza kupiga umbali wa kilomita 300, Uingereza na Ufaransa pia zilikubali kutoa idhini kwa Kiev kushambulia maeneo ya Russia kwa makombora ya Storm Shadow / SCALP yanayopiga umbali wa kilomita 500.
Rais wa Russia, Vladimir Putin, alitangaza siku ya Alhamisi katika hotuba muhimu kwa watu na vikosi vya jeshi vya nchi hiyo kwamba Ukraine ilitumia silaha za masafa marefu za Magharibi kushambulia ardhi ya Russia.

Kwa kuzingatiwa kuwa hapo awali Russia iliwaonya Wamagharibi juu ya hatua ya nchi za Magharibi ya kuiruhusu Ukraine kushambulia ardhi ya Russia kwa kutumia silaha za masafa marefu za Magharibi, Moscow imechukua hatua tofauti kutoa onyo kali kwa nchi za Magharibi na NATO. Katika hatua ya kwanza, Rais Vladimir Putin alitia saini Mwongozo Mpya wa nyuklia wa nchi hiyo, ambao unashusha chini masharti ya kutumia silaha za nyuklia. Amri ya Rais Putin inaipa Moscow ruhusa ya kutumia silaha za nyuklia dhidi ya “nchi isiyo na silaha za nyuklia” ilimradi nchi hiyo iwe inaungwa mkono na nguvu za nyuklia.
Katika hatua yake ya pili ya kuzionya nchi za Magharibi na NATO katika hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa, Russia kwa mara ya kwanza ilitumia kombora jipya la balestiki la masafa ya kati lenye kasi kubwa zaidi ya sauti kushambulia ardhi ya Ukraine. Rais wa Russia Vladimir Putin ametangaza kuwa wanajeshi wa nchi hiyo wamefanya mashambulio ya pamoja kwenye kituo cha kijeshi cha ulinzi na viwanda cha Ukraine kujibu shambulio dhidi ya ardhi ya Russia ambapo makombora ya masafa marefu ya Marekani na Uingereza yalitumika. Putin amebainisha kuwa: “Katika mashambulio hayo, moja ya mifumo mpya ya makombora ya masafa ya kati ya Russia yaani kombora la ultrasonic lisilo la nyuklia lenye kasi ya zaidi ya sauti kwa jina la “Oreshnik”, limefanyiwa majaribio kwa mafanikio.

Mkabala wake Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine ameashiria hotuba ya Putin kuhusu kufanikiwa kutumiwa kombora lisilo la nyuklia la balestiki kulenga taasisi ya kijeshi ya ulinzi na viwanda ya Ukraine na kusisitiza kuwa Rais wa Russia anataka kushadidisha vita.
Hatua ya Russia ya kutumia kombora jipya la masafa marefu kuishambulia Ukraine ni onyo kali kwa nchi za Magharibi hasa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wa NATO kwamba zinapaswa kusubiri makombora hayo kutua katika nchi zao iwapo hatua za uchochezi na za kivita dhidi ya Russia zitaendelea.