Kuimarisha uhusiano na Urusi ‘kipaumbele cha sera ya kigeni’ kwa Iran: Pezeshkian
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian (Kulia) na Katibu wa Baraza la Usalama la Russia Sergei Shoigu wanakutana mjini Tehran Agosti 5, 2024. (Picha na rais.ir))
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian ameitaja Russia kuwa ni “mwenzi wa kimkakati” wa Jamhuri ya Kiislamu, akisisitiza kwamba upanuzi wa uhusiano na Moscow ni kipaumbele cha juu cha sera za kigeni za serikali yake.
Pezeshkian ameyasema hayo jana Jumatatu alipokutana na Katibu wa Baraza la Usalama la Russia Sergei Shoigu ambaye alikuwa mjini Tehran kwa ziara ya siku moja ya kufanya mazungumzo na mamlaka ya Iran.
Amebainisha kuwa, Russia imekuwa mshirika thabiti katika nyakati za changamoto za Iran na kusisitiza ulazima wa kuharakisha utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya nchi hizo mbili.
“Tunaamini kwamba enzi ya kuegemea upande mmoja kwa madola fulani, ikiwa ni pamoja na Marekani, imekwisha,” alisema rais huyo. “Muunganisho wa misimamo na ushirikiano kati ya Iran na Urusi katika kukuza ulimwengu wenye pande nyingi bila shaka utaimarisha usalama na amani duniani.”
Ziara ya Shoigu inakuja huku kukiwa na mvutano mkubwa katika eneo hilo baada ya Israel kumuua Ismail Haniyeh, kiongozi wa kisiasa wa Hamas, mjini Tehran siku ya Jumatano, na kusukuma eneo hilo ukingoni.
Tehran imeapa kwamba kitendo cha uchokozi katika ardhi yake hakitapita bila jibu.
Rais wa Iran alisema siku ya Jumatatu kwamba mauaji ya Haniyeh ni ukiukaji wa wazi wa sheria na kanuni za kimataifa.
“Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaki kwa vyovyote kupanua wigo wa vita na mgogoro katika eneo, lakini kwa hakika utawala huu utapata jibu kwa jinai na uthubutu wake,” alisema.
Moscow pia imelaani vikali mauaji ya Haniyeh, ambaye alikuwa mpatanishi mkuu katika mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza. Maafisa wakuu wa Urusi wamesema kuwa wale waliohusika na mauaji hayo walikuwa wakitafuta kuvuruga matumaini yoyote ya amani katika eneo hilo na kuivuta Marekani katika makabiliano na Iran.
Wakati wa mkutano wa Jumatatu, Pezeshkian alilaani jinai za kutisha za Israel huko Gaza pamoja na juhudi zake za kueneza vita katika eneo zima.
Kwa upande wake Shoigu amempongeza Pezeshkian kwa mara nyingine tena kwa kuchaguliwa kuwa rais wa Iran na kuitaja Jamhuri ya Kiislamu kuwa mshirika mkuu wa kistratijia wa Russia katika eneo.
Akielezea kuridhishwa na juhudi za pamoja za Urusi na Iran za kuunda “ulimwengu wa pande nyingi” na kuhakikisha usalama wa kikanda, alisisitiza kwamba uhusiano kati ya washirika hao wawili unakua katika sekta zote.
Kabla ya kukutana na Pezeshkian, Shoigu aliketi na Mkuu wa Majeshi ya Jeshi la Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri.
Jenerali Bagheri aliutaja uhusiano wa Iran na Russia kama “wa kimkakati na wenye mizizi mirefu”, na akasema pande zote mbili zimeazimia kufanya kazi katika kupanua zaidi uhusiano wa pande mbili.
Alisema mabadiliko ya serikali hayatavuruga uboreshaji wa uhusiano kati ya Tehran na Moscow.
Jenerali huyo wa ngazi za juu wa Iran amebainisha kuwa Marekani sasa inafahamu kuwa zama za kuegemea upande mmoja zimepitwa na wakati. “Tutakaribisha ushirikiano wa pande tatu kati ya Iran, Russia na China,” alisema.
Shoigu, akijibu, alisema Russia inapenda kuimarisha ushirikiano wa pande zote na Iran katika masuala ya kikanda.
Ziara ya Shoigu mjini Tehran ilitokana na mwaliko wa mwenzake wa Iran, Ali Akbar Ahmadian, katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa, shirika la habari la Tasnim liliripoti.
Wawili hao walikutana mapema siku hiyo kujadili maendeleo ya kikanda.