Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Jumatatu ya jana aliwasili Muscat, mji mkuu wa Oman katika muendelezo wa safari zake za kieneo.
Kabla ya hapo siku ya Jumapili Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwasili Baghdad, mji mkuu wa Iraq na kukutana na rais, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na kujadili masuala ya pande mbili na matukio ya kieneo. Jana Jumatatu, Araghchi alikutana na kushauriana na waziri wa mambo ya nje wa Oman na pia maafisa wa Ansarullah ya Yemen huko Muscat, mji mkuu wa Oman. Araghchi kabla ya hapo pia alisafiri hadi Lebanon, Syria, Saudi Arabia na Qatar kwa lengo la kuchunguza matukio ya kikanda.
Safari za kikanda za Seyyed Abbas Araghchi zina jumbe kadhaa muhimu. Ujumbe wa kwanza ni kwamba ijapokuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikaribishi kupanuka kwa vita katika eneo la Asia Magharibi, lakini iko makini kabisa kujilinda dhidi ya vitisho vya utawala wa Kizayuni na Marekani, na katika nafasi ya ulinzi, haogopi kupanuliwa vita.
Kwa hivyo, inawezekana kusema kuwa, safari za kikanda za Araghchi zina mwelekeo wa kumfanya adui asiweze kushambulia. Stratejia hii ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaonyesha kuwa, Tehran imeachana na siasa za subira ya kistratijia na haiogopi kukabiliana moja kwa moja na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ujumbe wa pili wa safari za kieneo za Seyed Abbas Araghchi ni kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ingali imesimama pamoja na makundi ya muqawama na uungaji mkono wake kwa harakati hizo ni katika ajenda zake kuu na ambazo inazipa kipaumbele. Kimsingi ni kuwa, safari za kieneo za Araghchi zenye lengo la kuyaunga mkono makundi ya muqawama zinasambaratisha propaganda zinazofanywa na vyombo vya habari vya Kizayuni na vya Magharibi zenye lengo la kuibua pengo kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na makundi ya muqawama.
Safari za kieneo za Sayyed Abbas Araghchi zinaonyesha kivitendo uwongo wa aina hii ya propaganda na inabainisha simulizi za kweli za siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa makundi ya muqawama. Mazungumzo ya Araghchi na maafisa wa Ansarullah huko Muscat, mji mkuu wa Oman, pia yanatathminiwa katika mwelekeo huo huo.
Ujumbe wa tatu muhimu wa safari ya Seyyed Abbas Araghchi katika nchi za eneo hili ni kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimsingi inataka amani na utulivu katika eneo la Magharibi mwa Asia, na utawala wa Kizayuni ndio mhusika kivita katika eneo hili. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kuweko juhudi zaidi kutoka kwa nchi za eneo hili ili kuzuia kuenea kwa vita.

Moja ya sababu za kuendelea kushuhudiwa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza na Lebanon ni udhaifu wa wazi wa nchi za Kiarabu mbele ya utawala huo ghasibu na mtenda jinai.
Nukta ya mwisho ni kwamba, safari za kieneo za Sayyid Abbas Araghchi na vilevile safari iliyofanywa na Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Baraza la Kiislamu mjini Beirut Lebanon zinaonyesha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wakati mmoja inatumia diplomasia na vita kwa ajili ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel na vilevile kukomesha jinai za utawala huo ghasibu na kuzuia kuenea kwa vita katika eneo hili.
Kwa hakika hii inaonyesha wigo mpana wa diplomasia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na uwezo wake wa kijeshi.