
Hizbullah ya Lebanon inatekeleza vyema operesheni zake za kijeshi dhidi ya jeshi la Kizayuni katika nyanja mbalimbali.
Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon umetangaza kutekeleza operesheni tatu muhimu za makombora katika maeneo na vituo vya utawala wa Kizayuni. Katika operesheni ya kwanza ambayo imetekelezwa leo Jumatatu asubuhi, Hizbullah imeshambulia kwa makombora makazi ya Wazayuni ya Ilit Hashahar. Katika operesheni ya pili, muqawama wa Kiislamu wa Lebanon umelenga kwa maroketi vitongoji vitatu vya walowezi wa Kizayuni vya Sha’al, Hatsur na Delton. Katika operesheni yake ya tatu, Hizbullah imelenga na kuharibu kwa makombora kadhaa kambi ya Meron (kituo cha vita vya kielektroniki cha utawala wa Kizayuni) kaskazini mwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Mabomu yaliyorushwa kutoka kusini mwa Lebanon pia yamepiga moja kwa moja maeneo kadhaa ya Tel Aviv.
Siku ya Jumapili tarehe 3 Novemba pia Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon ulifanya operesheni 28 tofauti dhidi ya shabaha, zana, vikosi, vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kambi za kijeshi za utawala huo wa Kizayuni. Duru za Lebanon zimetangaza kulazimika kukimbia jeshi vamizi la Israel kutoka mji wa Al-Khayam” ulioko kusini mwa Lebanon kufuatia mafanikio ya operesheni za wapiganaji wa Hizbullah. Redio na Televisheni ya Kizayuni imetangaza kwamba ndege isiyo na rubani ilipiga moja kwa moja kiwanda kimoja kilichoko kaskazini mwa mji wa Nahariya. Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni pia vimeripoti kutokea milipuko kadhaa katika kambi ya Ramat David iliyoko mashariki mwa Haifa kutokana na kurushwa ndege kadhaa zisizo na rubani kutoka Lebanon.
Hizbullah imeutahadharisha utawala wa Kizayuni kupitia mkanda wa video ambapo imeuonya kwamba hautabakia na hata kifaru kimoja. Kituo cha Habari za Mapambano cha Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon kimeonyesha picha za kuzinduliwa silaha mpya ya kijeshi ya Hizbullah, ambapo Shahid Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa zamani wa Hizbullah amenukuliwa akisema kwamba ikiwa vifaru vya utawala wa Kizayuni vitaingia Lebanon, basi utawala huo hautabakia na hata kifaru komoja.
Hizbullah haijafumbia macho mashambulizi ya kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni na kulengwa raia wa Lebanon, bali imekuwa ikilenga vikali maeneo ya walowezi wa Kizayuni kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Duru mpya ya mashambulio ya Hizbullah pia imelenga vituo vya kijeshi na kijasusi vya utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Kufuatia operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa mnamo tarehe 7 Oktoba 2023, viongozi wa utawala ghasibu wa Israel wamekuwa wakishuhudia kushindwa mfululizo kwa jeshi la utawala huo mkabala wa makundi ya muqawama ya Palestina huko Ghaza, suala ambalo limewapelekea kulipiza kisasi na kufunika kushindwa huko kwa kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Lebanon kwa lengo la kueneza mgogoro na mvutano unaoongezeka katika eneo.
Mpango wa Tel Aviv wa kupanua vita katika eneo unatekelezwa katika hali ambayo baadhi ya makamanda wa kijeshi wa utawala huo walikuwa wametahadharisha kuhusu kushadidi mgogoro huo na kutoweza Wazayuni kukabiliana na makundi ya muqawama katika eneo, likiwemo la Lebanon.
Vitendo vya kigaidi vya baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni vya kuwaua shahidi makamanda wa muqawama wa Lebanon na Palestina havikusaidia malengo na njama za Wazayuni dhidi ya muqawama bali vikosi vya muqawama katika eneo vimeingia kwenye medani ya vita vikiwa na mshikamano na umoja na kuweza kupata mafanikio makubwa katika uwanja huo. Operesheni mseto za makundi ya muqawama angani na katika nchi kavu dhidi ya utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zimeukatisha tamaa kabisa na kuwapelekea watawala wa Kizayuni kukiri kuwa hawana tena uwezo wa kuendeleza vita dhidi ya makundi ya muqawama.
Kuendelea kwa operesheni za kijeshi za muqawama wa Lebanon dhidi ya jeshi la Kizayuni kumethibitisha wazi utayari wa vikosi vya muqawama na nafasi muhimu ya vikosi hivyo ya kukabiliana vilivyo na hali zote za uadui Mzayuni, huku Tel Aviv daima ikinufaika na uungaji mkono kamili wa serikali za Marekani na nchi nyingine za Magharibi.