Kuelekea uchumi wa kidijitali Tanzania kujiimarisha usalama mtandaoni

Arusha. Tanzania imeendelea kujiimarisha na kuongeza nguvu kwenye usalama mitandao ili kukuza uchumi wa kidijitali pamoja na kuvutia wawekezaji. kupitia Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU), imekuwa miongoni mwa nchi 47 bora zilizowekwa kwenye kundi la kwanza zenye mitandao bora salama.

Hayo yamesemwa jana Alhamisi Aprili 10, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama  (ICTC)  Dk Nkundwe Mwasaga , akizungumza katika Jukwaa la nne la usalama wa mtandao lililokutanisha wadau na wataalam wa masuala ya Teknolojia ya Habari (Tehama) wa ndani na nje ya nchi.

Amesema kupitia jukwaa hilo wataalamu na wadau hao watajadiliana namna bora ya kuboresha usalama wa kimtandao na kuwa Tanzania inapoelekea kwenye uchumi wa kidijitali imeendelea kujiimarisha kwani usalama wa mtandao una uhusiano na masuala ya kiuchumi ikiwemo uwekezaji.

“Tanzania imetathminiwa duniani kupitia taasisi ya umoja wa Mataifa ya ITU, inayokusaiana na mambo ya Tehama na  imewekwa katika kundi la kwanza la nchi 47 bora zenye mitandao salama bora duniani,” amesema

“Katika uchumi wa kidijitali, huduma nyingi zinatolewa kwa kutumia mitandao hivyo tunawaangalia walaji kwa makini na tunatumia wataalamu kuhakikisha mifumo yetu inakuwa madhubuti. Jambo mojawapo linalovutia wawekezaji wa kidijitali ni usalama mtandaoni,” ameongeza

Mkurugenzi huyo amesema usalama wa mtandao ni eneo ambalo linabadilika kila wakati, matishio ya mtandao nayo yanabadilika na kuwa usalama wa mtandao kidijitali haina mipaka.

“Duniani imeonekana kuna wakati unakuta kuna huduma inapotea kwa muda fulani inarudi hayo ni miongoni mwa mambo tunayotegemea kujadiliana kwenye jukwaa hili ili kujua ukipata changamoto kama hizo namna gani ya kutengeneza mifumo kwa haraka,”

“Ukiangalia mkakati wetu wa mapinduzi ya kidijitali una nguzo tano ikiwemo usalama mitandao, ulinzi wa taarifa binafsi na kumlinda mlaji, katika masuala haya yote tunamuangalia mlaji (mtumiaji wa mwisho) aweze kupata huduma vizuri,” ameongeza

Kuhusu masuala ya akili mnemba (AI), amesema Tume hiyo imekuwa ikihakikisha inapitia mitaala ya Vyuo Vikuu na kuwa vijana wa Kitanzania wameanza kuonyesha umahiri wao na kuichukua AI kama fursa kwani kumekuwa kukianzishwa kampuni changa za kibunifu zenye kuleta matokeo chanya kwa jamii.

Amesema suala la usalama wa mtandao kimataifa imeonyesha kuongezeka kwa ripoti za mashambulizi ya programu za huduma za serikali na sekta nyingine muhimu katika nchi nyingi pamoja na zile zinazoathiri watu binafsi.

Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Sarah Mwaisumo amesema Chuo hicho kina mpango wa kuanzisha maabara ya kisasa (smart lab) kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma yakiwemo ya usalama mtandaoni ili wakimaliza waweze kufanya mazoezi kwa vitendo.

“Ili kuendelea kuinua ujuzi IAA tuna mpango wa kuwa na smart lab ya masuala ya usalama mtandaoni kwa ajili ya wanafunzi wakimaliza waweze kufanya mazoezi kwa vitendo na itasaidia ujuzi wanaoupata kwenda kwenye jamii,” amesema

Mhadhiri huyo amesema Tume hiyo kuwakutanisha wadau mbalimbali kutachochea kuleta matokeo chanya katika jamii ikiwemo kuhamasisha vijana kutojihusisha na vitendo vya kihalifu mtandaoni na badala yake kutumia elimu walizonazo kujiingizia kipato kwa njia halali.

“Ni muhimu sana Tanzania ambayo tunaenda kwenye uchumi wa kidijitali kuwekeza kwenye smart lab ili kuwasaidia hawa vijana wetu,” amesema

Mtaalamu wa masuala ya usalama wa mtandao kutoka Benki ya CRDB, Robert  Karamagi, amesema  jukwaa hilo ni muhimu na linawasaidia kama wadau kuongeza uelewa katika masuala mbalimbali ikiwemo matishio ya usalama mitandaoni.

“Inatusaidia kufahamu na kuongeza uelewa wa masuala ya usalama wa mitandaoni ikiwemo namna wavamizi wa mitandaoni wanafanya kazi na namna ya kukabiliana na matishio hayo ya mitandaoni,” amesema

“Sisi kama watoa huduma za kifedha tuna mifumo mingi ya kidijitali, tuna sera ambazo zinatusaidia kupambana na mambo hayo ikiwemo kulinda taarifa binafsi za wateja na watumiaji,” amesema

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *