Ushahidi uliopo ikiwa ni pamoja na utawala huo kueleza hamu yake ya kutaka kusimamisha vita kusini mwa Lebanon unaweka wazi uhakika huu kwamba harakati ya muqawama ya Hizbullah imeweza kudumisha uwezo wake wa kukabiliana na kuzuia mashambulizi ya adui dhidi yake licha ya kuuliwa viongozi wake.
Pamoja na kuuawa shahidi viongozi na makamanda kadhaa wa Hizbullah siku kadhaa zilizopita na kushambuliwa maeneo ya raia na kiuchumi huko Lebanon, lakini utawala wa Israel si tu umeshindwa kufikia malengo uliyokusudia katika vita vya nchi kavu bali umepata vipigo na hasara za kimaada na kibinadamu na hakuna siku ambayo Wazayuni hawajeruhiwi na kuuawa katika vita kati yao na harakati ya Hizbullah.

Mwenendo wa kukimbia na kukataa kuhudumu katika jeshi la Israel kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kudumu kwa muda mrefu vita katika Ukanda wa Gaza na Lebanon, uzembe na kuwepo mivutano na tofauti za kimtazamo ndani ya baraza la mawaziri la Netanyahu kuhusu hatima ya mateka wa Kizayuni wanaoshikiliwa na wanapambano wa Palestina; na wakati huo huo mashinikizo na taathira za kisaikolojia zinazosababishwa na vita hivyo yanazidi kuongezeka, na inatazamiwa kuwa kuendelea vita, itakuwa changamoto kubwa sana kwa muundo wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni.
Wizara ya vita ya utawala wa Kizayuni imetangaza kuwa wanajeshi na askari polisi 890 wa utawala huo wameuawa tangu Oktoba 7 mwaka jana hadi sasa.
Takwimu hizi zinaonyesha kuwa kwa wastani kila mwezi wanajeshi 540 wa Israel wanalikimbia jeshi kutokana na madhara ya kiakili na kisaikolojia waliyosabishiwa na vita. Vile vile katika kipindi cha miezi sita ya kwanza baada ya kuanza vita dhidi ya Gaza, wanajeshi 43 walioajiriwa rasmi kwa muda mrefu na 235 wa kikosi cha akiba waliwasilisha maombi wakitaka kuwa huru na kuacha kuhudumu jeshini.

Matukio ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni ya kukataa waziwazi kulitumikia jeshi la Israel, khususan katika kivuli cha kuendelea hali ya vita katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kutokana na taathira zinazoweza kusababishwa kutolewa adhabu ya kifungo cha hadi miezi 6 jela kwa mtu atakayepatikana na hatia, yamechukua sura mbalimbali katika mwaka uliopita.
Wakati huo huo, jinai za karibuni za jeshi la Kizayuni dhidi ya Lebanon mbali na kuwa ni radiamali ya kuchupa mipaka mkabala wa kushindwa na kupata vipigo mtawalia jeshi la utawala wa Kizayuni katika vita vya nchi kavu na wakati huo huo kufeli mfumo wake wa ulinzi wa anga kukabiliana na mashambulizi ya Hizbullah na wanamuqawama lakini lengo lingine pia la jinai hizo ni kuandaa mazingira ya kumuongezea nguvu mjumbe wa Marekani ili kufanikisha matakwa ya utawala huo haramu katika eneo.
Jinai za karibuni za jeshi la Israel ikiwa ni pamoja na kulishambulia eneo la al-Janah huko Beirut mji mkuu wa Lebanon na kuwaua shahidi raia 30 wa nchi hiyo na kutishia kuishambulia hospitali ya Sahel na bandari ya Al-Awazai ni katika hali ambayo kwa kawaida vituo hivyo vinatambulika kama ngome za wananchi za harakati ya Amal chini ya uongozi wa Nabih Berri.

Sambamba na ziara ya mjini Beirut ya Amos Hochstein Mjumbe Maalumu wa Rais wa Marekani anayeshughulikia faili la Lebanon na utawala wa Kizayuni; utawala wa Kizayuni umejaribu kutishia kuishambulia hospitali ya al Saheh na bandari ya al Awazai na kutuma ujumbe wa indhari kwa Nabih Berri Spika wa bunge la Lebanon ambaye ni mwakilishi wa muqawama katika mazungumzo ya kusitisha vita ili asalimu amri kwa matakwa na hatua za kujitanua za Israel. Nabih Berri ambaye ni mshirika wa harakati ya mapambano ya Hizbullah wiki jana aliiambia televisheni ya al Arabiya kuwa safari ya Hochstein ni fursa ya mwisho ya kufikia mapatano ya kusitisha vita kabla ya uchaguzi wa Marekani, na kwamba atapinga kufanyiwa marekebisho yoyote azimio nambari 1701.
Inapasa kuzingatia pia kuwa mashambulizi mtawalia ya angani na ya ardhini ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon na hatua yake ya kukiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo; hujuma ambazo zimesababisha watu zaidi ya milioni mbili kuhama makazi yao huko Lebanon ni kinyume cha sheria za wakati wa vita na wakati huo huo hujuma hizo zinakinzana na azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo linaipa haki Lebanon ya kuwalinda raia pamoja na harakati ya Hizbullah ambacho ni chama rasmi kilichoasisiwa kwa mujibu wa sheria za ndani ya nchi hiyo.
Kwa hakika, lau isingekuwa silaha na muqawama wa Lebanon kusimama imara hakuna shaka kuwa jeshi la Kizayuni lingesonga mbele hadi Beirut kufuatia kimya cha taasisi za kimataifa na hatua za upande mmoja za nchi za Magharibi, kwa uungaji mkono kamili wa Marekani.