
Dar es Salaam. Fukuto la kamari linaendelea kuwanyemelea baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu, uongozi wa Pamba ya Mwanza tayari imedai baadhi ya wachezaji wake wanabeti.
Kama haitoshi, mashabiki wamekuwa wakilitumia neno hilo kuwakebehi wachezaji wa timu pinzani pale inapotokea wamefanya makosa hata ya bahati mbaya uwanjani, jambo ambalo wachezaji jana waligusia namna linavyowaathiri.
Katika muendelezo wa makala hii leo, wadau wa michezo wameonyesha ‘bomu’ ambalo Watanznaia wanalitengeneza katika soka kwa kisingizio cha upinzani na utani wa jadi.
Si ajabu leo hii shabiki kumkebehi mchezaji uwanjani, akimshutumu kubeti au kupanga matokeo pale anapofanya kosa la bahati mbaya.
Kama haitoshi, ni kawaida hususani zinapocheza timu za Simba na Coastal au Yanga dhidi ya Singida, upande fulani kuukebehi mwingine kwamba wanaocheza ni ‘mtu na mdogo wake’, hakuna mechi zaidi ya bonanza.
Kauli hizi ambazo zina viashiria za upangaji wa matokeo, huwa zinatolewa na mashabiki kwa muktadha wa utani wa jadi, jambo ambalo kwa upande mwingine linachukua sura ya upangaji matokeo.
Aliyewahi kuwa mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sunday Kayuni anasema nyuma ya kauli hizo, aidha ziwe zina ukweli au vinginevyo, zinaweza kutumiwa na wajuzi wa mambo kuonyesha picha hasi ya soka la Tanzania.
Anasema utamaduni ulioibuka katika soka la Tanzania hivi sasa la baadhi ya mashabiki kutumia maneno aliyoyaita ni ya kipuuzi kuwa yanakwenda kutengeneza bomu ambalo likilipuka taswira ya mpira wa Tanzania nayo itachafuka.
“Kutumia maneno ya hovyo sio utani wa jadi, hivi sasa ni kama tumetoka kwenye utani wa kistaarabu na kuingia kwenye utani wa kipuuzi, sijui ni nini tutafanya kutoka huko, lakini tunakwenda kubaya,” anasema.
Alisema kitendo cha wachezaji kuzomewa na kushutumiwa kubeti, mashabiki kuzihusisha timu fulani kuwa na ‘vina saba’ na timu nyingine zinazoshiriki Ligi moja na kuona timu A haiwezi kuifunga timu B zikikutana kwa kuamini wana ‘undungu’ ni taswira chafu inayokwenda kuharibu mpira wa Tanzania.
“Bahati mbaya tunazifurahia hizi kauli, haziishii ndani, hata wajuzi wa mambo haya huzitumia kwa kuchukulia kinachozungumzwa ndicho kinatokea na kutia doa hata hii Ligi ambayo tunaiona ni bora Afrika,” alisema.
Anasema kauli hizi na nyingine zinazoibuka hivi sasa si ajabu kutumiwa na watu wanaofanya tathimini ya soka kubaini soka la Tanzania linaendeshwaje.
“Watu wanaona kauli hizi zinaishia hapa ndani, lakini wajuzi wa mambo wanapotaka kukuelewa wewe wanakufuatilia kwa vitendo na kauli zako.
“Tunaweza kuwa tunasema kama mzaha, kwamba timu hii ikicheza na timu hii haishindi hadi ipange matokeo, kwa wenzetu hizi ni nyenzo za kukujua,” anasema.
Anasema upangaji wa matokeo ni kama kamari, na katika mpira ni kosa akibainisha kwamba itafika mahali fukuto linaloendelea nchini litaishusha hadi Ligi tunayoisifiwa kuwa ni bora.
“Wanaofuatilia wakija kutathimini, hiki kilichopo, kinachosemwa na kinachofanyika mwisho wa siku watasema tunachokisikia ni hiki, tunawezaje kuiweka hiyo nchi kwenye ubora huo? Anasema.
Akielezea madai ya kamari, Kayuni anasema kama mhusika wa mchezo akianza kujihusisha au kuhisiwa, maana yake soka la Tanzania linapokwenda si kuzuri.
“Hakuna jambo baya kama wahusika wa mpira kubeti, kwa kufanya hivi atasababisha kitu ambacho hakiruhusiwi cha kupanga matokeo na anyebainika anapaswa kuondoshwa mara moja kujihusisha na masuala ya soka,”.
Akimtolea mfano ya Andrés Escobar Saldarriaga (Gentleman), beki wa zamani wa timu ya taifa aliyeuwawa kwa kupigwa risasi ambaye kisa chake tulikigusia katika makala ya jana, Kayuni anasema huo ni mfano wa madhara ya kuhusishwa, kuhisiwa au kubeti kwa wachezaji.
“Escober alijifunga goli kwa bahati mbaya sana kwenye fainali za kombe la dunia, ilikuwa ni bahati mbaya na kwa mchezaji yoyote inatokea lakini alihisiwa kujifunga makusudi, hivyo hiki kinachoendelea nchini kwetu iwe kipo au hakipo kinapaswa kudhibitiwa mapema.” Anasema.
Kayuni pia amegusia mmoja wa marefarii Ujerumani aliyefungiwa kuchezesha maisha kwa kuwa alihusika kubeti.
“Ilikuwa ni skendo mbaya, yule refarii ilikuwa akipewa mechi, anabeti timu hii itashinda magoli kadhaa na kweli akichezesha hiyo mechi atahakikisha kile alichobeti ndicho kinatokea na baada ya mechi anachukua pesa zake.
“Ulifanyika uchunguzi, akakamatwa na alifunguliwa mashtaka, aliishia kubaya na kufugiwa maisha kujihusisha na soka, kwa hiyo hii sintofahamu ya kamari inayofukuta idhibitiwe mapema,” amesema.
Kwa waamuzi ipo hivi
Japo hakuna uthibitisho wa moja kwa moja unaowahusisha baadhi ya waamuzi na kamari, kauli za mashabiki pia dhidi yao zinawaingiza kwenye shutuma hizo.
Mwamuzi mkongwe, Isihaka Shirikisho anasema iwe kuna ukweli, au sivyo ni makosa makubwa mwamuzi kujihusisha na kubashiriki.
“Mtu anaweza kuingia kwa tamaa, lakini athari yake ni kubwa, kama fukuto limeanza, ichunguzwe atakayebainika aadhibiwe iwe mfano kabla hatujafika hatua mbaya zaidi huku mbele kwa kuwa kuna michezo inamalizika inakuwa na malalamiko mengi.
“Ingawa ninachokiona kwenye soka letu hivi mashabiki wengi wana mihemko, hizi kelele zinasababishwa na hizi timu zetu kubwa zinapocheza,” anasema.
Anasema katika soka kuna makosa ya kimchezo na ya kiufundi yanatokea kwa mwamuzi uwanjani, hayapaswi kuhusishwa na kamari wala upangaji mwingine wa matokeo.
Nini kifanyike
Mchezaji wa zamani wa Yanga, Ally Mayay anasema suala la kubashiriki katika soka ni changamoto, si Tanzania tu katika ligi mbalimbali duniani lipo.
“Hapa kwetu limeanza kufukuta, ni jambo baya na halipaswi kufumbiwa macho, tunapaswa kuwa na kamati ya maadili kusimamia ili ikiwezekana hata kwenye mikataba watakayoingia wachezaji kuwe na kipengele cha kuzuia kucheza kamari, sijui kama kuna timu zina kitu hicho.
“Hivi sasa mpira ni biashara na kuna watu wanatengeneza faida kupitia soka, hivyo inapothibitika mchezaji, kiongozi, refarii au mtu anayejihusisha na soka amebeti hatua kali zichukuliwe,” amesema.
Kuhusu sintofahamu ya wachezaji kuhusishwa na kamari hata pale inapotokea amefanya kosa la kimchezo, Mayay anasema maneno ya mashabiki inategemea na mhusika anayachukuliaje.
“Kama huwezi kuya-control, yatakutesa na kisaikolojia yatakuvuruga, katika soka huwezi kumzuia shabiki kuzungumza, kwa kuwa anazungumza kwa hisia, akiwa anazungumza si akili yake bali ni moyo.
“Vitu vipo vitaendelea kuwepo, hizi kejeli za timu hii ikicheza na timu hii zinapanga matokeo na nyinginezo haziwezi kuzuilika wala kuepukika kwa mashabiki, uzuri mpira wa miguu ni mchezo wa wazi.”
Anasema inapotokea makosa ya kujirudia ni tatizo, lakini kama mechi itachezwa na makosa yasiwepo, maneno hayawezi kuepukika.
“Hata wakaguzi wa CAF (Shirikisho la Soka Afrika) wanafuatilia ligi mbalimbali, kuna makosa ambayo ni ya kibinadamu hayaepukiki, lakini kukiwa na muendelezo wa makosa ya aina moja hilo litakuwa ni tatizo.”
Mayay anasema, utani wa jadi kwa maana ya timu za Simba na Yanga ndiyo chanzo cha yote, lakini ni utani ambao ulikuwepo na utaendelea akibainisha kwamba maneno ya mashabiki huwa yana mchango na matokeo hasi au chanya kwa upande mwingine.
“Timu pinzani ikikuandalia mkakati ukauchukulia ‘serious’ ananufaika. Nakumbuka kuna mwaka nikiwa nahodha wa Yanga tukijiandaa kucheza na Simba, tuliweka kambi Kigamboni.
“Wakati ule Kigamboni usafiri wa Panton mwisho ilikuwa ni saa 2 usiku, wazee wa Yanga waliwezaje lakini walipata panton saa 6 usiku wakaja kambini usiku wa kuamkia siku ya mechi,” anasema.
Akielezea mfano huo, Mayay anasema waliamshwa na kocha Raul Shungu. Wale wazee wakiwa na mwenyekiti wakasema kuna wachezaji hawatakiwi kucheza mechi ile.
“Wote waliowataja walikuwa ni wa kikosi cha kwanza, wakasema kwa taarifa ambazo wamezipata hatakiwi kucheza.
“Kocha Shungu hakulala siku hiyo, asubuhi saa 4 tukakutana kutaja kikosi, akaniita mimi nahodha nikamwambia kile tulichokiamua kabla ndicho hicho, hakuna mchezaji ambaye hatacheza,” anasema Mayay.
Anasema walipofika uwanjani, wazee walivurugwa huku viongozi wakiwa na wasiwasi, dakika za mwanzo Thomas Kipese akaifungia Simba bao la kuongoza baada ya Peter Manyika kutoka golini akipangua krosi na kufungwa.
“Wazee waliongea wakisisitiza kile walichotueleza usiku kambini kwamba hatukutakiwa kucheza ile mechi, hata hivyo tulisawazisha na kuongeza mabao mengine mawili, mechi ikaisha tumeshinda 3-1.
“Wale wazee walitufuata kutuomba radhi, hivyo maneno kwenye mpira hasa katika mechi za Simba na Yanga hayawezi kumalizika, ni vile tu wachezaji mtayapokeaje na kutoruhusu yawaathiri kisaikolojia,” anasema.