Rais wa Ukraine amesema, madai hewa yaliyotolewa na nchi za Ulaya dhidi ya Iran kwamba imeipelekea Russia makombora ya balestiki hayana ukweli.
Kwa kutegemea uzushi huo, Umoja wa Ulaya (EU) umeiwekea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ilhali Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine ametamka bayana mbele waandishi wa habari katika mkutano wa pamoja wa Ukraine na nchi za Nordic: “Iran na Russia zimekuwa na mazungumzo ya dhati kuhusu utumaji wa makombora, lakini kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, Iran bado haijaipatia Russia makombora”.
Nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ujerumani na Ufaransa zilidai huko nyuma, kuwa Iran imepeleka makombora ya balestiki nchini Russia na kwamba makombora hayo yametumiwa katika vita vya Ukraine. Kwa kutumia madai hayo ya uwongo, nchi hizo za Troika ya Ulaya zimeanzisha kampeni kubwa ya propaganda za vyombo vya habari dhidi ya Iran.

Kufuatia madai hayo, mnamo Jumatatu ya tarehe 14 Oktoba, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya waliokutana nchini Luxembourg waliidhinisha vikwazo zaidi dhidi ya mpango wa makombora wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Vikwazo hivyo vinajumuisha watu binafsi na mashirika yanayodaiwa kuhusika na utengenezaji na upelekaji makombora ya balestiki nchini Russia. Kwa mujibu wa tangazo rasmi la Baraza la Umoja wa Ulaya, watu saba na mashirika saba wamejumuishwa kwenye vikwazo hivyo vipya. Mashirika ya ndege ya Iran Air, Mahan Air na Saha Airlines pamoja na makampuni mawili ya vipuri pia, yamejumuishwa kwenye orodha hiyo ya vikwazo. Baada ya Russia kuishambulia kijeshi Ukraine, Umoja wa Ulaya ulianza kutekeleza sera za kihasama dhidi ya Iran kwa kutumia kisingizio cha ushirikiano wa kijeshi wa miongo kadhaa ambao umekuwepo kati ya Iran na Russia.
Na hii ni pamoja na kwamba, baada ya Wazayuni kuuvamia Ukanda wa Ghaza na kuwaua kwa halaiki Wapalestina, misimamo ya uadui ya serikali nyingi za Ulaya dhidi ya Iran imeongezeka. Marekani na nchi hizo hazikuweza kuchukua hatua ya wazi ya kivitendo dhidi ya uungaji mkono wa Iran kwa Muqawama wa Palestina na Lebanon wa kuzisaidia nchi hizo kukabiliana na uchokozi wa utawala wa Kizayuni.

Kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina na Lebanon na kuonyesha chuki kwa Wazayuni wachinjaji wa watoto, yamekuwa ndio mahubiri yaliyotanda sasa hivi kimataifa. Marekani na serikali za Ulaya ni washirika wa jinai zote zinazofanywa na Wazayuni huko Palestina na Lebanon. Nchi hizo zimetia ulimi puani kuhusiana na madai yao ya kutetea utu na haki za binadamu kwa kufumbia macho, bali hata kuunga mkono, jinai za utawala wa Kizayuni; na hazijabadilika hata chembe katika kuuunga mkono kwa hali na mali utawala bandia wa Israel.
Ili kuiwekea mashinikizo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, serikali za Ulaya zilijikita katika kubuni madai hewa dhidi ya Tehran kwa kuuandama ushirikiano wake wa kijeshi na Russia na athari zake katika mwenendo wa vita vya Ukraine.
Russia ni nchi kubwa, na kabla ya vita vya Ukraine, nchi nyingi duniani zikiwemo za Ulaya, zilikuwa na uhusiano mkubwa na nchi hiyo. Kabla ya vita vya Ukraine, kiwango cha ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Russia kilifikia karibu yuro bilioni 370. Wakati huo huo, washirika wengi wa Ulaya na Marekani katika kila pembe ya dunia waliendeleza, bali hata kupanua, kiwango chao cha ushirikiano wao na Russia.
Kuhusiana na suala hili, tunaweza kuitaja hapa Uturuki au Saudi Arabia na Muungano wa Falame za Kiarabu (UAE) au India, ambapo hakuna yoyote kati ya nchi hizi iliyokemewa au kuwekewa vikwazo na Ulaya na Marekani kwa sababu ya kuwa na uhusiano na Russia. Kwa hivyo ni wazi kabisa, kwamba serikali za Ulaya na Marekani zinatafuta sababu tu ili kuiwekea mashinikizo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na zimelitumia suala la ushirikiano wa Iran na Russia kama kisingizio cha kuiwekea vikwazo vipya. Katika mkakati wa kueneza hofu kuhusiana na Iran, Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya, hususan Troika ya EU zinatumia kila kisingizio ili kuendesha vita vya kisaikolojia na vya mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mashinikizo hayo inawekewa Iran katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu imeshatangaza mara kadhaa kuwa haipendelei upande wowote katika vita vya Ukraine na inatilia mkazo kutumiwa njia za kidiplomasia ili kuhitimisha mzozo huo. Kuhusiana na hilo, Iran imesisitiza mara kadhaa kwamba, haijapatia Russia makombora ya balestiki.
Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X akiashiria sisitizo alilotoa Zelensky kwamba hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa, kuna makombora ya balestiki yaliyopelekwa Russia na akazitaka nchi za Ulaya ziungame na kulisahihisha kosa zililofanya.

Araghchi ameandika: “Umoja wa Ulaya hivi karibuni ulipiga marufuku mashirika yetu ya ndege kuingia Ulaya, hatua iliyowalenga abiria wa kawaida wa Iran na wasio Wairan”.
Araghchi amekumbusha kwa kusema: “hatua hii imechukuliwa kutokana na madai ya uwongo na yasiyo na msingi kwamba Iran imeipatia Russia makombora ya balestiki ili kuyatumia nchini Ukraine”. Katika andiko lake hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameambatanisha video ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na kuandika: “sasa hata Rais Zelensky mwenyewe anasema waziwazi kwamba, hakuna kombora lolote la Iran ililopatiwa Russia”.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemalizia kwa kuandika: “sasa ni wakati wa Umoja wa Ulaya kuachana na kituko hiki. Kuwalenga Wairani wa kawaida kwa kutumia tuhuma zisizo na msingi wowote ni kitendo kilicho kinyume na maadili na ni kosa la wazi kabisa linalopasa kusahihishwa mara moja…/