‘Kosa kubwa’ la Israel la kumuua mkuu wa Hamas halitapita bila jibu: Rais wa Iran
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian (Kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan Ayman Safadi wanakutana mjini Tehran Agosti 4, 2024. (Picha na rais.ir)
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian anasema mauaji ya utawala wa Israel dhidi ya Ismail Haniyeh mjini Tehran yalikuwa “kosa kubwa” ambalo halitakosa jibu.
Katika kikao na Ayman Safadi Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan mjini Tehran siku ya Jumapili, Pezeshkian alisema kitendo cha utawala wa Israel cha mauaji dhidi ya Haniyeh, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya muqawama ya Hamas, kinakiuka kanuni zote za kimataifa.
“Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatarajia nchi zote za Kiislamu na mataifa huru duniani kulaani vikali uhalifu huo,” aliongeza.
Amesisitiza kuwa, maadui wakubwa na wakiukaji wa uhuru, demokrasia na haki za binadamu wanatumia uwezo wao mkubwa wa kisayansi na kiutendaji kutekeleza vitendo vya kigaidi na jinai za kutisha.
“Wanadai kutetea uhuru, demokrasia na haki za binadamu na kumtambulisha yeyote ambaye anajiepusha kuwafuata adui wa kanuni na maadili hayo,” rais wa Iran alisema.
Utawala wa Israel siku ya Jumatano ulimuua Haniyeh, ambaye alikuwa mjini Tehran kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa rais mpya wa Iran. Chifu huyo wa Hamas aliuawa pamoja na mlinzi wake aliyetambulika kwa jina la Wasim Abu Shaaban.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei ameuonya utawala wa Israel kuhusu “jibu kali” kwa mauaji ya Haniyeh na kusema kuwa ni jukumu la Jamhuri ya Kiislamu kulipiza kisasi damu ya kiongozi huyo wa mapambano ya Palestina.
Kwingineko katika matamshi yake, Pezeshkian alisema sera ya mambo ya nje ya utawala wake itazingatia kukuza amani na utulivu katika eneo na dunia.
Amesisitiza ulazima wa kubuniwa ushirikiano baina ya nchi za Kiislamu ili kukomesha ukatili na jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Palestina.
Pezeshkian ameeleza matumaini yake kuwa mazungumzo kati ya wajumbe wa kidiplomasia wa Iran na Jordan kuhusu kurejeshwa uhusiano wa pande zote yataleta matokeo haraka iwezekanavyo ili nchi hizo mbili za Kiislamu ziweze kunufaika na uwezo wa pande zote mbili.
Amebainisha kuwa uhusiano wa kindugu na ushirikiano wenye kujenga kati ya Tehran na Amman pia utahudumia maslahi ya nchi za eneo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan kwa upande wake, alisema Amman analaani mauaji ya Haniyeh na anayachukulia kama hatua inayoendana na juhudi za Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu za kueneza mvutano katika eneo hilo.
Safadi ameongeza kuwa Jordan pia ilishutumu mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza tangu yalipozuka mwezi Oktoba.
Amesisitiza kuwa, Jordan inataka kurejesha uhusiano na Iran na kufanya juhudi za pamoja za kuweka utulivu, usalama na amani katika eneo hili.
Takriban Wapalestina 39,583, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake, wameuawa na watu 91,398 kujeruhiwa katika vita ambavyo Israel ilianza tarehe 7 Oktoba 2023, kufuatia operesheni ya kulipiza kisasi ya vuguvugu la muqawama wa eneo la Palestina.
Kabla ya kukutana na Rais Pezeshkian, Safdari alifanya mazungumzo na Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Bagheri Kani.