Kortini akidaiwa kutapeli kwa kujitambulisha kwa jina la Jakaya Kikwete

Dar es Salaam. Mkazi wa Mabwepande, Shembiu Shekilaghe (38) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam kujibu mashtaka 14 yakiwamo ya kujitambulisha kuwa ni Jakaya Mrisho Kikwete, wakati akijua ni uongo na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Mshtakiwa huyo amefikishwa mahakamani hapo leo Jumanne, Septemba 24, 2024 na kusomewa mashtaka yake na wakili wa Serikali Salma Jafari, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hawa Magesa.

Akisoma mashtaka yake, Jafar amedai kati ya mashtaka 14 yanayomkabili Shekilaghe, mashtaka matano ni ya kutumia laini iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, mashtaka matatu ni ya kutoa taarifa za uongo kinyume cha sheria, shtaka moja kujiwasilisha yeye ni Jakaya Mrisho Kikwete (Rais mstaafu wa Tanzania) na yaliyosalia ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Jafar amedai Septemba 2, 2024 mshtakiwa akiwa katika eneo lisilojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa taarifa za uongo kupitia akaunti ya mtandao wa kijamii wa Facebook yenye jina la Mrisho Jakaya Kikwete aliandika ujumbe unaosomeka, “Ukiweka akiba ya Sh49,000 utapata mkopo wa laki tatu marejesho ni Sh30,000 kila mwezi kwa muda wa miezi 10.”

Inadaiwa kuwa, kupitia akaunti hiyo alitoa taarifa inayosomeka, “ukiweka akiba ya Sh59,000 utapata mkopo wa Sh400, 000 marejesho ni Sh40,000 kila mwezi kwa muda wa miezi 10.”

Vile vile, kupitia akaunti hiyo alitoa taarifa inayosomeka, “ukiweka akiba ya Sh69,000 utapata mkopo wa laki tano marejesho ni Sh 50,000 kila mwezi kwa miezi 10.”

Shekalaghe pia anadaiwa Juni 7, 2024 eneo la Temeke, kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook kwa nia ovu alijitambulisha kama mama Salma Kikwete mke wa Rais mstaafu wa awamu ya nne, wakati akijua kuwa ni uongo.

Mahakama hiyo iliendelea kueleza, Juni 7, 2024 mshtakiwa kupitia akaunti iliyosajiliwa kwa jina la Salma Foundation, alitoa taarifa za uongo zinazosomeka, “ukiweka akiba 105,000 itapata mkopo wa milioni moja marejesho laki moja kila mwezi kwa miezi 10 na ukiweka 205,000 utapata mkopo wa milioni mbili marejesho laki mbili kila mwezi kwa miezi 10.”

Wakili Jafar amedai kuwa, katika mashtaka matano ya kutumia laini ya simu ambayo imesajiliwa kwa jina la mtu mwingine, mshtakiwa huyo anadaiwa Septemba 3, 2024 katika eneo la Mji Mpya Mabwepande, alikutwa akitumia namba ya simu iliyosajiliwa kwa majina ya Matias Ngowi, Modesta Marumi, Jane Mhanga, James Zephania na Amini Omary, bila kuwa na ruhusa ya mtoa huduma ambaye ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Shekalaghe anadaiwa Julai 31, 2024 kupitia namba iliyosajiliwa kwa jina la Tatu Sunzula, alijipatia fedha Sh49,000 kutoka kwa Albert Atanas kwa kudai atampa mkopo wa Sh 500,000 wakati akijua kuwa ni uongo.

Mshtakiwa huyo pia, anadaiwa Agosti 17,2024 kupitia namba hiyo hiyo alijipatia Sh100,000 kutoka kwa Samson Mwandawila kwa kudai atampatia mkopo wa Sh 800,000 wakati akijua si kweli.

Wakili Jafar amedai, Agosti 9, 2024 kupitia namba hiyo, mshtakiwa alijipatia Sh100,000 kutoka kwa Rudi Maduka akidai atampatia mkopo wa Sh1,000,000 kupitia taasisi yake ya Jakaya Kikwete Foundation, jambo alilojua ni uongo.

Mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili, alikana na upande wa mashtaka umedai upelelezi wa shauri hilo umekamilika, hivyo wanaomba Mahakama ipange tarehe kwa ajili ya kumsomea hoja za awali mshtakiwa huyo.

Hakimu Magesa ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 10, 2024 na mshtakiwa amerudishwa rumande kwa kukosa wadhamini.