
Bukoba. Nani waliomlisha sumu Daud Francisco? Ni kitendawili kinachohitaji kuteguliwa na vyombo vya uchunguzi, baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba kuwaachia huru watu wawili waliokuwa wameshitakiwa kwa mauaji hayo.
Clemensia Karoli na Mazeyose Daud wameachiwa huru na Jaji Ferdnand Kiwonde katika hukumu aliyoitoa Novemba 21, 2024 akieleza sababu za kuwaachia huru ni upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya wawili hao.
Francisco, mkazi wa Kijiji cha Murulama wilayani Ngara mkoani Kagera, alifariki dunia Januari 22, 2023 na uchunguzi wa maabara uliofanywa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ulithibitisha uwepo wa sumu aina ya cypermethrin mwilini.
Sumu hiyo iliingia kwenye utumbo na baadaye kuhamia kwenye ini, ushahidi wa mazingira ulionyesha iliwekwa kwenye chakula aina ya ndizi, lakini hata hivyo polisi hawakuchukua sampuli ya chakula hicho kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara.
Kuachiwa kwa watuhumiwa hao kutokana na udhaifu wa ushahidi wa upande wa mashitaka kama alivyoeleza Jaji Kiwonde, kunaibua swali ambalo linapaswa kujibiwa na vyombo vya uchunguzi la nani hasa alimwekea sumu Francisco.
Ushahidi wa Jamhuri ulivyokuwa
Shahidi wa kwanza, Gordian Beyanga aliieleza mahakama kuwa Januari 24, 2023 alikwenda hospitali ya misheni ya Rulenge kufanya uchunguzi wa mwili wa marehemu na sababu za kifo zilikuwa zimeelezwa ni kula chakula chenye sumu.
Kwa hiyo, alipasua mwili wa marehemu na kuchukua sampuli za ini na utumbo, akieleza viungo hivyo vilikuwa si vya kawaida kwani vilikuwa na alama nyeusi na mwili ulikuwa na majimaji, ulikuwa na wekundu na aliandaa ripoti.
Shahidi wa pili, John Zacharia alisema alikwenda eneo la tukio na kujulishwa na mjumbe wa nyumba 10, William Elikana kuwa huenda marehemu amekufa kwa kula chakula kilichokuwa na sumu kitaalamu ‘food poisoning’.
Alieleza alikwenda mahali ambako chakula hicho kilikuwa kimemwagwa kulikokuwa na harufu inayofanana na iliyokuwepo katika chumba, ndipo wakawaweka chini ya ulinzi watuhumiwa wawili kuhusu tukio hilo.
Alidai kufanya mahojiano ya awali na watuhumiwa ambao mshitakiwa wa kwanza, Clemencia alidaiwa kukiri kwa mdomo kwamba alimpa pesa mshitakiwa wa pili kununua sumu na kwa kushirikiana, walimpa marehemu kupitia chakula.
Alieleza mshitakiwa wa pili, Daud, aliwaeleza kuwa kikopo au chupa iliyokuwa na sumu ilitupwa kwenye shimo la choo ambako walikwenda na kuchukua kielelezo hicho na kukikabidhi polisi pamoja na washukiwa hao.
Shahidi wa tatu, ambaye alikuwa mlinzi wa amani, alieleza namna alivyoandika maelezo ya ungamo ya mshitakiwa wa pili ambaye alidai alikiri kutenda kosa la mauaji na maelezo hayo yalipokewa kama kielelezo na Mahakama.
Shahidi wa nne, Constantine Mulima kutoka maabara ya Serikali, alieleza namna alivyopokea sampuli za ini na utumbo pamoja na kopo au chupa na katika uchunguzi wa kimaabara alibaini kuwa ni sumu ya ‘cypermethrin’.
Mashahidi wengine walikuwa ni askari wa Jeshi la Polisi ambao walieleza namna walivyopokea taarifa ya kifo, kuwakamata washukiwa, kuwahoji na kusimamia uchukuaji wa sampuli na baadaye kuwafikisha kortini kwa kosa la mauaji.
Katika utetezi wao, washitakiwa hao wawili walikana kumpa marehemu chakula chenye sumu, badala yake wakasema alikufa kifo cha kawaida, kutokana na maradhi ya muda mrefu ya ugonjwa wa uvimbe wa miguu na tumbo.
Hukumu ya Jaji
Katika hukumu, Jaji Kiwonde alisema hakuna ubishi kuwa Daud Francisco ni marehemu na kiini cha kifo chake kutokana na ushahidi uliopo, kilikuwa si cha asili na kilisababishwa na sumu iliyofanya viungo visifanye kazi.
Alieleza ushahidi wa mchunguzi kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ilionyesha kifo chake kinaweza kuwa kilisababishwa na kiuatilifu (sumu) aina ya cypermethrin ambayo aliibaini kutokana na uchunguzi wa kimaabara.
Jaji alisema swali muhimu ni kama washitakiwa ndio waliofanya kitendo hicho haramu na kwamba, wajibu wa upande wa mashitaka si kuthibitisha tu kifo, bali ushahidi wao ni lazima uwaunganishe washitakiwa na mauaji hayo.
“Katika kesi hii, mashahidi wote saba wa Jamhuri hakuna hata mmoja aliyewaona washitakiwa wakimuua kwa kumpa sumu. Ushahidi wa Jamhuri unaegemea maelezo ya ungamo ya mshitakiwa wa pili na ushahidi wa mazingira,” amesema.
Jaji Kiwonde amesema upande wa Jamhuri unashikilia ushahidi wa kimazingira kuwa washitakiwa walikuwa na marehemu wakati anakufa na ndio walimhudumia kwa chakula ambacho wanadai kilikuwa na sumu inayotajwa.
Katika kesi hiyo, Jaji amesema kuna maelezo ya mshitakiwa wa pili yaliyoandikwa Januari 25, 2023 wakati inaelezwa walikiri mbele ya mwenyekiti wa kitongoji Januari 22, 2023 na wakapelekwa kituo cha Polisi Rulenge Januari 23, 2023.
“Katika sheria hakuna muda maalumu wa kuandika maelezo ya ungamo lakini lazima yaandikwe kwa muda mwafaka au mapema iwezekanavyo na kama yaliandikwa kwa kuchelewa lazima Jamhuri itoe maelezo,” amesema Jaji.
Amesema kutokuwepo kwa maelezo ya kwa nini maelezo hayakuchukuliwa mapema kadri iwezekanavyo, kunafanya maelezo hayo yasiaminike na kwamba, katika kesi hiyo, hakuna maelezo yenye mashiko ya ucheleweshaji huo.
Katika utetezi wake, mshitakiwa wa pili alieleza alipigwa na mwenyekiti wa kitongoji, William Elikana na mgambo ambao walitumia fimbo na mapanga kumtisha, hivyo kulazimika kukiri kosa ili kuokoa maisha yake.
Jaji amesema katika usikilizwaji wa kesi, shahidi wa pili, John Zakaria alitoa maelezo ya jumla tu kuwa hawakuwapiga washitakiwa lakini alipododoswa na mawakili wa utetezi akakiri kweli Elikana alikuwepo, hali ambayo inaibua mashaka.
Jaji amesema kitendo cha Polisi kushindwa kuchukua sampuli ya chakula kilichokuwa kimemwagwa nje walichodai kilikuwa na harufu ya sumu, kilifanya kusiwepo ushahidi kuthibitisha kama chakula hicho kilikuwa na sumu iliyotajwa.
Jaji amesema kosa la mauaji ni kubwa ambalo adhabu yake ni kifo mtu anapopatikana na hatia, hivyo inatarajiwa polisi wafanye uchunguzi makini na pia Jamhuri inapaswa kubeba jukumu la kuthibitisha shitaka hilo.
“Ikizingatiwa kuwa washitakiwa walikanusha kumuua marehemu, upande wa mashitaka ulikuwa na jukumu zito la kuthibitisha mashitaka katika viwango vinavyokubalika katika mashauri ya jinai,” amesema.
Jaji amesema kwa kuwa haijathibitishwa kuwa washtakiwa ndio waliomuua marehemu, hoja ya uwepo wa nia ovu inakufa, hivyo Mahakama inaona Jamhuri imeshindwa kuthibitisha shitaka hilo hivyo anawaachia huru washitakiwa.