Korti yabariki kifungo cha maisha jela kwa kumbaka mwanafunzi

Arusha. Juhudi za Dickson Mbadame, mkazi wa Songwe kujinasua katika kifungo cha maisha jela baada ya kutiwa hatiani kwa kumbaka shemeji mwenye umri wa miaka 10, zimegonga mwamba.

Mwathirika wa tukio hilo aliyekuwa akisoma dara la nne katika moja ya shule za msingi wilayani humo, alienda nyumbani kwa dada yake, aliyekuwa akiishi na Dickson kuomba Sh500 za mchango wa rambirambi kwa ajili ya mwanafunzi mwenzao, aliyekuwa amefiwa na baba.

Ilidaiwa siku ya tukio, Mei 29, 2023, mwanafunzi huyo alipofika nyumbani kwa mshtakiwa hakumkuta dada yake, badala yake alimkuta shemeji yake na baada ya kumweleza ameenda kuomba rambirambi, mrufani alimbaka kabla ya kumpa Sh500 alizoomba.

Mrufani huyo alikata Rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, akipinga hukumu iliyotolewa Mahakama ya Wilaya ya Songwe, ilimyomhukumu adhabu hiyo na fidia ya Sh1 milioni.

Juhudi za mkazi huyo kujinasua katika adhabu hiyo zimegonga mwamba baada ya Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mbeya kutupilia mbali rufaa yake.

Hukumu hiyo ya Februari 10, 2025 imetolewa na Jaji Musa Pomo, aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo, ambapo baada ya kupitia mwenendo wa kesi ya msingi, sababu tano za rufaa zilizowasilishwa na mrufani, amebariki adhabu iliyotolewa na mahakama ya awali baada ya kujiridhisha kesi ilithibitishwa bila kuacha shaka.

Awali Desemba 30, 2024 Mahakama hiyo ya wilaya ilimtia hatiani kwa kosa la ubakaji kinyume na kifungu cha 130(1)(2)(e) na 131(1) cha Kanuni ya Adhabu na kumhukumu adhabu hiyo.

Ilidaiwa Mei 29, 2023 eneo la Majengo Mkwajuni, alimbaka shemeji yake aliyekuwa na umri wa miaka 10 na  mwanafunzi wa darasa la nne.

Ilidaiwa mwanafuzni huyo alimfuata mrufani nyumbani kwake kuomba fedha za rambirambi za mwanafunzi mwenzake aliyekuwa amefiwa na baba yake.

Ilidaiwa na upande wa mashtaka kuwa mwanafunzi huyo alipofika nyumbani kwa bahati mbaya hakumkuta dada yake na badala yake alimkuta shemeji yake (mrufani),ambaye alimbaka kabla ya kumpa Sh500 alizoomba za rambirambi hiyo.

Ilidaiwa kuwa wakati mwanafunzi huyo anarejea shuleni,aliona vitu vyeupe kwenye sare yake ya shule (sketi),mwanafunzi mwenzake alimshauri kuripoti suala hilo kwa Mwalimu ambaye alitoa taarifa polisi.

Shahidi wa pili Joyce Modestus  na shahidi wa tano, PF.22511 Inspekta Msaidizi Stella  Rwekamwa wa kituo cha polisi Mkwajuni, walifika eneo la tukio ila hawakumkuta mrufani na badala yake wakamkuta mkewe (shahidi wa pili),ambaye aliwaeleza polisi kuwa mumewe ameenda kazini.

Shahidi huyo wa pili alitoa namba ya simu ya mumewe ambaye alitakiwa kufika Kituo cha Polisi na mwanafunzi huyo alipochunguzwa katika Hospitali ya Mwambani,alibainika kuwa amebakwa hali iliyopelekea mrufani kushitakiwa kwa kosa la ubakaji.

Baada ya uamuzi huo wa mahakama ya chini, Dickson alipinga uamuzi huo akiwa na sababu tano za rufaa ikiwemo hakimu kukosea kisheria kumtia hatiani na kumhukumu kwa kuzingatia ushahidi usio na uthibitisho kutoka kwa shahidi wa kwanza hadi wa tano.

Nyingine ni hakimu alikosea kisheria kwa kushindwa kutathmini ushahidi kwani maelezo yalidai amefanya kosa hilo hilo Mei 25,2023 huku mashahidi wa mashtaka wakitoa ushahidi wao walidai kosa alimetendeka Mei 29, 2023 hivyo ushahidi ulikinzana.

Sababu nyingine ni kuwa hakimu alikosea kisheria kushikilia kuwa kosa lilithibitishwa bila shaka baada ya kushindwa kutathmini ipasavyo ushahidi wa mashtaka na mahahidi wote.

Katika rufaa hiyo, mrufani huyo alijitetea mwenyewe bila uwakilishi wa wakili huku upande wa jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali James Mwenda.

Akiwasilisha sababu zake za rufaa mahakamani hapo, mrufani huyo alianza na hoja ya nne kuwa mwathirika (shahidi wa kwanza) alitoa ushahidi wa ajabu kwani upande wa mashtaka ulishindwa kumwita mwanafunzi mwenzake anayedaiwa kumshauri aripoti suala hilo kwa mwalimu, pamoja na mwalimu huyo.

Kwa maoni yake alidai hao walikuwa mashahidi muhimu ambao wangeweza kuthibitisha ushahidi huo wa shahidi wa kwanza huku akitolea  mfano wa kesi ya Hemed Said dhidi ya Mohamed (1984) na Azizi Abdallah dhidi ya Jamhuri (1991).

Akiwasilisha kwa pamoja sababu ya pili, tatu na tano za kukata rufaa,mrufani huyo alidai kosa hilo halikuthibitishwa bila kuacha shaka na kuwa kulikuwa na kushindwa katika tathmini ya ushahidi wa mashtaka ambao ulikuwa chini ya kiwango kinachohitajika na sheria.

Akijibu hoja hizo, Wakili James alidai mahakama ya chini ilimtia hatiani mrufani huyo baada ya ushahidi wa mwathiriwa (shahidi wa kwanza) ulithibitishwa,uliaminika na mashahidi wote muhimu waliitwa mahakamani kutoa ushahidi kwa ajili ya mashtaka.

Alieleza kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha mrufani dniye alitenda kosa hilo na kuwa hakuna ukinzani wa mashahidi waliotoa ushahidi katika kesi hiyo hata walipopishana kuhusu suala la muda,kwani ulishapita muda mrefu hivyo wasingeweza kutaja muda kamili.

Kuhusu malalamiko kwamba mahakama ya mwanzo haikuzingatia ushahidi wa upande wa utetezi, wakili huyo alionyesha mahakama ukurasa wa sit awa hukumu iliyopigwa chapa, hivyo ushahidi wa utetezi ulizingatiwa na mahakama ya mwanzo

Uamuzi Jaji

Jaji Pomo amesema baada ya kuzingatia mawasilisho yanayopingana na pande zote mbili,sababu za kukata rufaa pamoja na kupitia upya rekodi ya mahakama, suala ambalo mahakama hiyo inaangalia ni iwapo rufaa hiyo inafaa au vinginevyo.

Amesema chini ya msingi wa kwanza, malalamiko ya mrufani ni kwamba ushahidi wa mwathiriwa  haukuwa na uthibitisho na wa ajabu huku ushahidi wa shahidi wa pili hadi wa tano ulikuwa ni tetesi, katika kusuluhisha hilo amesema ataongozwa na msimamo wa kisheria.

Amesema msimamo wa kisheria uliofafanuliwa katika mashauri mbalimbali Jaji huyo amesema ni kanuni iliyothibitishwa kuwa makosa ya kujamiiana ushahidi bora unatoka kwa mwathiriwa.

Jaji amesema mwathiriwa wa tukio hilo,alitoa ushahidi mahakamani Agosti 31,2023 kama inavyoonekana kutoka ukurasa wa saba hadi tisa wa mwenendo wa kesi, na kuwa baada ya kusoma ushuhuda wake, alisimulia yaliyompata Mei 29, 2023.

Jaji amesema mwanafunzi huyo alisimulia asubuhi ya siku hiyo alivyokwenda nyumbani kwa dada yake akihitaji kupewa Sh500 kwa ajili ya rambirambi ya mwanafunzi mwenzake aliyefiwa na baba yake ila hakukutana na dada yake na kusimulia alivyovutwa ndani ya nyumba na mrufani,kuvuliwa nguo, kulazwa chini na kubakwa.

“Kwa hivyo, kwa maoni yangu, huu ni aina ya ushahidi unaothibitisha kosa la ngono kama ilivyofafanuliwa na mahakama katika kesi ya Emmanuel Kabelele (supra),”

Jaji huyo amesema kinyume na uwasilishwaji wa mrufani, hakuna chochote alichofafanua mrufani kuhusu ushahidi wa mwathirika zaidi ya kudai ushahidi haukuthibitishwa.

Kuhusu utofauti wa tarehe ya kosa Jaji amesema wakati wa usikilizwaji wa awali uliofanyika Mei 31,2023 miongoni mwa mambo ambayo hayakupingwa ni kipengele cha nne na tano ambapo mrufai alikiri kukutana na mwathirika wa tukio hilo nyumbani kwake Mei 29,2023.

Kuhusu hoja hiyo amesema kutokana na ushahidi wa mwathirika wa tukio hilo,anatupilia mbali sababu hiyo ya kwanza ambayo inasuluhisha pia sababu za pili,tatu na nne za rufaa ambazo nazo zinatupiliwa mbali.

Kuhusu sababu ya tano kuwa ushahidi wa utetezi haukuzingatiwa, Jaji huyo amesema kwa upande wake amepitia hukumu iliyotolewa na mahakama ya awali na anachoona ni kwamba ushahidi wa upande wa utetzi ulizingatiwa kama inavyoonekana kwenye ukurasa wa sita,hivyo kutupilia mbali sababu hiyo.

Baada ya kuchambua mwenendo wa shauri la awali na sababu za rufaa hiyo Jaji Pomo alihitimisha kwa kueleza kuwa anatupilia mbali rufaa hiyo.