Korea Kaskazini yafanyia majaribio kombora la kisasa zaidi la nyuklia

Korea Kaskazini imetangaza kuwa, imefanyia majaribio moja ya makombora yake mapya zaidi yanayokusudiwa kuimarisha vizuizi vyake vya nyuklia, likiwa jaribio la kwanza tangu taifa hilo lilipotuhumiwa kupeleka wanajeshi nchini Russia.

Seoul ilitoa onyo siku moja kabla kwamba Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia ilikuwa inajiandaa kufanya jaribio la kombora jingine la masafa marefu (ICBM) au hata kufanya jaribio la nyuklia kabla ya uchaguzi wa Marekani wiki ijayo.

Jaribio hilo limefanyika saa chache tu baada ya mawaziri wa ulinzi wa Marekani na Korea Kusini kuitaka Pyongyang kuondoa wanajeshi wake kutoka Russia, wakionya kuwa wanajeshi wa Korea Kaskazini wakiwa katika sare za Russia wanapelekwa kuupigana dhidi ya Ukraine.

Kombora hilo la kuvuka mabara la ICBM lilifanyiwa majaribio nchini Korea Kaskazini kwa mara ya kwanza miaka saba iliyopita, na kisha jaribio jingine mwaka 2022.

Korea Kaskazini imekuwa ikiendelea kustawisha uwezo wake wa silaha za makombora tangu yalipokwama mazungumzo ya kuishinikiza itokomeze silaha zake za nyuklia na makombora ya balestiki, mkabala wa kupunguziwa vikwazo vilivyolemaza uchumi wa nchi hiyo.