
Korea Kaskazini imetangaza leo Ijumaa kuwa imefanyia majaribio mfumo mpya wa makombora ya kutungulia ndege chini ya usimamizi wa kiongozi wake Kim Jong Un, ambaye amempokea Katibu wa Baraza la Usalama la Urusi Sergei Shoigu huko Pyongyang siku hiyo.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Ziara hii ya afisa mkuu wa Urusi, waziri wa zamani wa ulinzi iliyotangazwa na mashirika ya habari ya Urusi ya Tass na RIA Novosti, inaonyesha kasi ya maelewano kati ya Moscow na Pyongyang, haswa katika nyanja ya kijeshi, tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo mwezi wa Februari 2022.
Nchi hizo mbili zilitia saini makubaliano ya ulinzi wa pande zote wakati wa ziara ya nadra ya Rais wa Urusi Vladimir Putin nchini Korea Kaskazini mwaka jana.
Pyongyang baadaye ilishutumiwa na Korea Magharibi na Kusini kwa kutuma wanajeshi kupigana dhidi ya Ukraine kwa kulisaidia jeshi la Urusi. Korea Kaskazini au Urusi hazijawahi kuthibitisha kutumwa kwa wanajeshi hao nchini Ukraine.
Mashirika ya kijasusi ya Korea Kusini na Magharibi yanakadiria kuwa zaidi ya wanajeshi 10,000 wa Korea Kaskazini wametumwa nchini Urusi ili kuisaidia kuliteka tena eneo la Kursk, ambalo lilishikwa kwa mshangao wengi na Ukraine katika majira ya joto ya mwaka 2024.
Kwa kuongezea, kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini, kutakuwa na uwasilishaji wa makombora, vipande 200 vya silaha za masafa marefu na risasi.
Majaribio ya silaha kabla ya kusafirishwa nje
Shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini KCNA pia limetangaza siku ya Ijumaa kwamba Bw. Kim amehudhuria, kwa tarehe ambayo haikutajwa, majaribio ya makombora mapya ya kutungulia ndege. Shirika hilo limetoa picha za makombora yaliyorushwa kutoka kwa njia ya ndege ya uwanja wa ndege na milipuko baharini.
“Jaribio hili lilmethibitisha kuwa jeshi la Korea Kaskazini sasa lina silaha nyingine kuu za ulinzi zenye utendaji wa kustaajabisha wa kivita,” Kim Jong Un amenukuliwa akisema na KCNA.
Jaribio hilo lilitangazwa siku moja baada ya kumalizika kwa mazoezi ya kijeshi ya kila mwaka ya Ngao ya Uhuru “Freedom Shield” nchini Korea Kusini, yaliyofanywa kwa pamoja na Marekani, na kulaaniwa siku ya Ijumaa na Wizara ya Ulinzi ya Korea Kaskazini kama “mazoezi ya vita vya uchokozi.”
Mwaka huu, “Freedom Shield” ililenga kujibu vitisho vya nyuklia, kibaolojia na kemikali vya Korea Kaskazini, kulingana na Seoul.
Mnamo Januari 10, siku ambayo zoezi hilo lilianza, Korea Kaskazini ilirusha makombora kadhaa ya balestiki kuelekea Bahari ya Manjano. Mwishoni mwa mwezi Februari, Pyongyang pia ilifanya majaribio ya kombora ili kuonyesha “uwezo wake wa kushambulia.”
Ahn Chan-il, mwasi wa Korea Kaskazini ambaye amekua mkurugenzi wa Taasisi ya Dunia ya Mafunzo ya Korea Kaskazini huko Seoul, amesema kurushwa kwa makombora ya kuzuia ndege siku ya Ijumaa kunaonekana kuwa “jaribio la silaha zilizokusudiwa kusafirishwa kwenda Urusi kwa matumizi nchini Ukraine.”
Bw. Ahn, akihojiwa na shirika la habari la AFP, amesema kuwa Pyongyang inatumia mazoezi ya kijeshi katika eneo la Kusini kama kisingizio cha kutengeneza silaha kwa ajili ya Moscow.
Korea mbili kitaalamu zimesalia katika vita kwa zaidi ya miongo saba, huku mzozo kati yao kutoka mwaka 1950 hadi mwaka 1953 ukiishia kwa kusitishwa kwa mapigano, sio kwa mkataba wa amani.